25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

‘KARIAKOO DERBY’ OMOG ALIMZIDI AKILI PLUIJM

48Na SAMWELI SAMWELI, DAR ES SALAAM

MSIMU uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC ilimaliza nafasi ya tatu nyuma ya Yanga SC na Azam FC, zikishika nafasi mbili za juu katika msimamo wa ligi hiyo. Yanga waliibuka mabingwa wa ligi hiyo na Azam FC ikishika nafasi ya pili.

Kwenye Kombe la Shirikisho, Simba SC iliishia robo fainali, wakati Yanga SC wakiibuka mabingwa na Azam FC mshindi wa pili. Kila kombe Simba SC iliambulia patupu.

Udhaifu huu ndio umewafanya Simba SC kuja kivingine  msimu huu, wakifanya usajili mzuri na tayari wametoa onyo kwa klabu zote bora Ligi Kuu, ikiwapiga 2-0 Mtibwa Sugar ambao hawa ni mabingwa wa zamani wa ligi kuu, pia kwa ubora wao wana heshima kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi  kule Zanzibar wakiwa pamoja kwenye kaliba ya  klabu kongwe za Simba na Yanga.

Simba pia wamewachapa 1-0 Azam FC, washindi wa pili ligi kuu msimu uliopita na kombe la FA. Ni nani asiyejua ubora wa Azam FC, mabingwa Kombe la Kagame wakiwa na nguvu nzuri kiuchumi nchini. Uwezo wa kuifunga Azam kama washindi namba mbili wa msimu uliopita inawapa hesabu nzuri kimbinu na kiufundi Simba SC kuelekea safari ya ubingwa wa ligi kuu msimu huu mpya wa 2016-17.

Hali ya kujiamini mbele ya Mtibwa Sugar na Azam FC iliwaingiza Simba SC kwenye mtanange wa Jumamosi dhidi ya watani wao wa jadi wakiwa na ari kubwa ya kusaka ushindi na kujidhihirisha ubora wao juu ya vigogo hao wa soka nchini wakilibeba kombe hilo mara 26.

Mchezo ulianza kwa kasi, timu zote zikisomana kwa zamu lakini ufundi mwingi ukionekana eneo la kiungo ambapo Simba SC walimsimamisha Jonas Mkude kama kiungo mkabaji na Mzamiru Yassin kama mchezeshaji, wakikinzana na Mbuyu Twite kwa upande wa Yanga kama mkabaji na Thabani Kamusoko mchezeshaji.

Omog aliweza kuzichanga vyema karata zake eneo hili la kiungo kuliko Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm. Kabla ya kutolewa kwa kadi nyekundu, dakika ya 26 Jonas Mkude aliweza kumpoteza Mbuyu Twite, hali iliyomfanya mara kwa mara Deus Kaseke kuingia kati kusaidia nafasi ya kiungo.

Goli la Yanga SC dakika ya 26 lililotiwa kambani na Mrundi Amis Tambwe ndilo lililovuruga mipango ya awali ya Josep Omog, Kocha wa Simba SC kuivuruga ngome ya Yanga kwa kutegemea kiungo.

Ni dhahiri kwa marudio ya picha za runinga Amis Tambwe aliunawa mpira ule kabla ya kufunga, hali iliyowafanya mashabiki wa timu hiyo kufanya fujo kwa kuligomea goli hilo na Mkude kutolewa nje kwa lugha chafu.

Baada ya kutoka Mkude na Simba kubaki tisa uwanjani, hapo ndipo ulipogundulika ubora wa kikosi cha Simba msimu huu kimbinu na kiufundi.

Simba walifanikiwa kurudi uwanjani kisaikolojia na kuwabana Yanga ambao walikuwa wamekamilika uwanjani kwa kucheza kwa kasi muda wote. Msingi wa mashambulizi hayo ukitokea pembeni kwa Shiza Kichuya ambaye aliweza kuichachafya ngome ya Yanga kwa krosi zake maridadi kwa wenzake ambazo kama Laudit Mavugo angekuwa vyema kimchezo, basi mchezo ule ungekwisha mapema.

Yanga, licha ya kuwa mbele kwa goli moja, ni lazima mwalimu Hans van Pluijm ajilaumu mwenyewe kwa kuzidiwa mbinu na Omog, ambaye alifanya mabadiliko mapema kuwakataa Yanga kumshambulia kwa udhaifu wa Novat Lufunga, baada ya kumwingiza Jjuuko Murshid na kuongeza kasi ya mashambulizi kwa kumtoa Mavugo na kumwingiza Fredrick Blagnon.

Kwa muda mrefu Juma Mahadhi alionesha kuchoka na kushindwa kuumudu mchezo ule, hali ambayo ingemlazimu Hans kumwingiza Msuva mwanzoni mwa kipindi cha pili, lakini alichelewa kufanya mabadiliko na kuwarudisha mchezoni Simba, ambao walikuwa wakilishambulia lango la Yanga muda wote. Goli la kusawazisha la Simba lililofungwa dakika ya 88 na Shiza Kichuya ni matokeo ya Simba kushambulia kwa kasi baada ya kuwamudu Yanga kati.

Kama Omog aliweza kuwarudisha mchezoni wachezaji wake baada ya goli la utata la Yanga na kadi nyekundu ya nahodha wao na kusawazisha goli, ni dhahiri Omog ameweza kukisoma vyema kikosi chake na hii ni hatari kwa bingwa mtetezi, Yanga SC na mwenzake Azam FC.

Ushindi dhidi ya Azam FC, Mtibwa Sugar na sare kwa bingwa mtetezi ni faida sana kimbinu kwa timu hiyo ambayo imecheza mechi saba bila kupoteza, ikishinda michezo mitano na kwenda sare michezo miwili.

Ni dhahiri sasa timu zote 15 katika ligi zitaanza kuitazama Simba SC kama timu tishio inayosaka ubingwa. Omog itampasa kujiandaa kwa upinzani mkali kutokana na dhana hii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles