28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

KARIA AANIKA VIPAUMBELE 11 AKIMRITHI MALINZI

MGOMBEA wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), amezindua kampeni zake kwa kutaja vipaumbele 11 alivyoviita ‘First Eleven’, atakavyovifanyia kazi endapo atachaguliwa kushika wadhifa huo.

Kampeni za uchaguzi wa TFF, utakaofanyika Agosti 12, mjini Dodoma, zilizinduliwa jana kwa wagombea wa nafasi mbalimbali kuanza kunadi sera.

Karia, ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa TFF, kabla ya kuteuliwa kukaimu nafasi ya Rais Jamal Malinzi, ambaye kwa sasa yuko mahabusu kutokana na tuhuma za kutakatisha fedha, alisema  endapo atapewa nafasi ya kuliongoza shirikisho hilo, atahakikisha anatatua changamoto zilizoshindikana huko nyuma.

Avitaja vipaumbele hivyo kuwa ni nidhamu ya muundo wa mfumo wa TFF, maendeleo ya soka la vijana, wanawake na ufukweni pamoja na mafunzo ya kujenga uwezo kwa watendaji wake kuanzia ngazi za chini.

Vingine ni kuboresha mapato na nidhamu ya fedha, maboresho katika Bodi ya Ligi, ushirikiano na wadau, udhamini na masoko, ubora wa mashindano, kuimarisha mfumo wa soka na  kuimarisha  sekta ya tiba pamoja na kuondoa changamoto ya waamuzi.

“Kuna changamoto ya waamuzi na vipo viashiria vya rushwa, licha ya kuwa havijathibitika, nitapambana navyo kama nitapewa nafasi ya kuwa Rais wa TFF. Pia suala la viwanja limekuwa ni tatizo kubwa linalotakiwa kutafutiwa ufumbuzi,” alisema.

Karia alisema endapo atashindwa kutekeleza ahadi zake hizo, atakuwa  tayari kung’tuka bila msukumo wa wadau wa soka.

“Hata Rais wa Tanzania, Mheshimiwa John Magufuli, alikuwa waziri  katika utawala wa marais watatu na anachokifanyia kazi kwa sasa ni zile changamoto alizoziona wakati  huo, hivyo hata mimi uongozi wangu utakuwa wa uwajibikaji, ” alisema Karia.

Wakati huo huo, mgombea wa nafasi ya makamu wa rais wa TFF katika uchaguzi huo, Mulamu Nghambi, ameahidi kuendeleza programu za vijana walio na umri  kuanzia miaka 13 kupitia shule za msingi na sekondari.

Akizindua kampeni zake jijini Dar es Salaam jana, Nghambi alisema atashirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kuhakikisha programu hiyo inafanikiwa mashuleni.

“Tutaandaa mfumo maalumu kupitia Kamati ya Ufundi ya TTF kusimamia programu za vijana itakayosaidia kutengeneza timu bora za taifa ambazo zitashiriki katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

“Hivyo hivyo kwenye soka la wanawake  tutashirikiana na TFWA (Chama cha Soka cha Wanawake) kuanzisha taratibu mahsusi za kupata wasichana wanaoweza kucheza soka tangu wakiwa shule pamoja na walimu na waamuzi wa kike,” alisema Ng’ambi.

“Pia kuna tatizo la ubadhirifu wa udhibiti wa fedha, hapa tutahakikisha tunaziba mianya ya upotevu na matumizi yasiyo ya lazima na kuongeza uwazi kwenye mapato na matumizi.

“Lazima tutumie njia za kisasa za mawasiliano (Digital platforms) kwa kuandaa ‘application’ ambayo itatengenezwa.

“Nitashauriana na viongozi wenzangu kuongeza timu zinazoshiriki ligi kuu kutoka 16 mpaka 20 kusaidia timu, TFF pamoja na mikoa kupata faida kiuchumi kutokana na uwapo wa mechi nyingi na wadhamini kujitangaza zaidi,” alisema Nghambi.

Nghambi alisema mpango wake mwingine ni kuifanya Bodi ya Ligi kuwa na mamlaka kamili kama kampuni isiyo na hisa chini ya shirikisho, hivyo kuzifanya klabu kuendesha ligi zenyewe pasipo kuingiliwa.

“Hii itasaidia kutoa mgongano ambao umekuwa ukitokea katika maamuzi mbalimbali na kuifanya bodi kujiendesha kiweledi na kutafuta wadhamini zaidi ili ligi iweze kuboreshwa kwa ushirikiano na nchi zilizoendelea,” alisema Nghambi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles