27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

NIYONZIMA, OKWI WAIBEBA ‘SIMBA DAY’ LEO

CLARA ALPHONC

KIUNGO Haruna Niyonzima na mshambuliaji Emmanuel Okwi leo wanatarajia kuwa vinara wa shamra shamra za tamasha la ‘Simba Day’, ambalo limepangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Klabu ya Simba imekuwa ikifanya tamasha hilo kila mwaka, lengo likiwa kuwatambulisha wachezaji iliowasajili kwaajili ya msimu mpya.

Hata hivyo, hamu na matamanio ya mashabiki wa Simba katika tamasha hilo ni kuwaona Niyonzima na Okwi wamevaa jezi zenye rangi nyekundu na nyeupe.

Niyonzima kwa kipindi kirefu alikuwa gumzo miongoni mwa mashabiki wa soka nchini, ikiwa ni baada ya kuachana na timu yake ya zamani ya Yanga, aliyoichezea kwa misimu sita na kujiunga na Simba katika usajili wa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Sababu ya kiungo huyo raia wa Rwanda kujadiliwa kwa muda mrefu ni kutokana na vuta nikuvute iliyokuwapo kati ya waajiri wake wa zamani, Yanga na Simba, ambazo zilikuwa zikitunishiana msuli, kila moja ikijigamba kumsajili kabla ya vijana wa Jangwani kuamua kunawa mikono na Wekundu hao kushinda vita kwa kumsajili.

Lakini kiu nyingine waliyonayo mashabiki wa Simba kwa kiungo huyo ni soka la ufundi wa hali ya juu, ambao hapo awali walikuwa wakiushuhudia akiwa kwa mahasimu wao, Yanga.

Kwa upande wa Okwi, mashabiki wa klabu hiyo wanataka kuona ujio mwingine wa mshambuliaji huyo, aliyerejea Msimbazi kwenye dirisha la usajili wa msimu ujao, baada ya kuachana na timu hiyo na  kutimkia Denmark na kujiunga na SonderjysjkE, kisha SC Villa ya nyumbani kwao Uganda.

Mganda huyo ana rekodi ya kuiwezesha Simba kutinga hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2011, huku akikumbukwa kwa kuchangia ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Yanga, katika mchezo wa Ligi Kuu ambapo pia alifunga mabao mawili.

Ukiwaweka kando nyota hao wawili, Simba pia itamtambulisha kinara wa mabao katika Ligi Kuu, Nichalaus Gyan, aliyesajiliwa na klabu hiyo wakati wa dirisha la usajili la msimu ujao.

Gyan, mwenye umri wa miaka 28, hadi sasa amefunga mabao 11 katika mechi 22 za timu yake, akiwa anaongoza orodha ya wafungaji katika Ligi ya Ghana, akiwa na kikosi cha Ebusua Dwarfs.

Baadhi ya wachezaji wengine wapya waliotua Simba kwaajili ya msimu ujao watakaotambulishwa leo ni pamoja na Erasto Nyoni, John Bocco, Shomari Kapombe, Aishi Manula (Azam FC), Ali Shomari, Salim Mbonde (Mtibwa Sugar).

Simba vs Rayon Sports

Katika tamasha hilo, kikosi cha Simba kilipiga kambi ya wiki mbili nchini Afrika Kusini, kabla ya kurejea nchini mwishoni mwa wiki, kitashuka dimbani kwenye uwanja huo  kukabiliana na mabingwa wa Rwanda, Rayon Sports, katika pambano la kirafiki.

Akizungumzia maandalizi ya tamasha hilo, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema kila kitu kiko shwari, ikiwamo hali ya kikosi cha timu hiyo kitakachoumana na Rayon.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles