Na WINFRIDA MTOI, Mtanzania Digital
KITENDO cha Klabu ya Gofu ya Lugalo kuendelea kuwa juu katika mchezo huo,Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) Luteni Jenerali Mathew Mkingule, amempongeza Ofisa Habari wa klabu hiyo. Kapteni Seleman Semunyu na askari wengine wanaocheza gofu kwa mafanikio waliyopata katika kulitangaza Jeshi michezoni.
Luteni Jenerali Mkingule alizungumza hayo jana usiku wakati wa hafla ya ufungaji na mashindano ya gofu ya Kombe la Mkuu wa Majeshi ‘CDF Trophy’ ambapo baadhi ya askari waliibuka washindi.
Amesema Jeshi linatambua uwezo wa Kapteni Semunyu, ndiyo sababu likampa majuku hayo na ubora wameuona katika majukumu yake ya kuitangaza JWTZ na nchi kwa ujumla kupitia vyombo vya habari.
“Nimpongeze Kapteni Semunyu, hamjui umahiri wake ulianza kuonekana akiendesha kipindi cha dakika 45 ITV na sasa tunajivunia kuwa na mtu wa aina yake,” amesema Luteni Jenerali Mkingule.
Ameongeza kuwa kutokana na jitihada za kulitangaza jeshi na nchi hasa katika michezo atafikisha kwa Mkuu wa Majeshi taarifa ya kazi nzuri inayofanywa na wachezaji wa gofu askari walioshinda kwenye mashindano hayo.
“Askari mlioshinda mmefanya kazi kubwa ya kuletea sifa JWTZ na Taifa kwa ujumla hakuna budi kupongezwa sambamba na Mwenyekiti kwa kuwalea vizuri kimchezo mpaka kufikia hapo,” amesema.
Aidha amesema JWTZ ipo katika mpango wa kuhakikisha inajenga viwanja vya gofu katika mikoa mingine vile Arusha na Mafinga, Iringa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu ya Lugalo Brigedia Jenerali Mstaafu Michael Luwongo, ameomba Jeshi kukamilisha ahadi ya Ujenzi wa Uwanja Jijini Dodoma.
Amesema klabu imejiandaa kutengeneza wataalamu watakaofundiaha mchezo huo mahali popote watakapohitajika.
Katika michuano hiyo iliyofanyika kwa siku tatu, yakishirikisha wachezaji wa kulipwa na ridhaa, mshindi wa jumla wa alikuwa ni Victor Joseph kutoka klabu ya Dar es Salaam Gymkhana.