Mwandishi Wetu-Tabora
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amelaani vikali vitendo vya baadhi ya watu walioanza kuvamia maeneo mapya ya hifadhi za misitu kwa kuwazingira maofisa misitu kwa kuwapiga na wakati mwingine kuwasababishia vifo wakati wanapotekeleza majukumu yao.
Akizungumza jana, wakati alipotembelea kukagua ujenzi wa ofisi na nyumba saba za watumishi zinazojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 1.3 katika shamba la miti Biharamulo lililopo katika Wilaya ya Chato mkoani Geita, Kanyasu alisema Serikali imejipanga vilivyo kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Alisema mauaji ya askari wawili yaliyofanywa na wafugaji mwishoni kwa mwaka jana katika msitu wa Hifadhi wa Isawima wilayani Kaliua mkoani Tabora kuwa yanarudisha nyuma juhudi za uhifadhi nchini
Alisema ameeleza tabia nyingine iliyozuka kwa baadhi ya watu kuanza kupiga mwano wanapowaona wahifadhi ikiwa ni ishara ya wananchi kujikusanya ili kuwadhuru wahifadhi hao kuwa vitendo vinachagiza chuki baina ya wananchi na wahifadhi, badala ya kujenga mahusiano mazuri baina yao.
“Nimeutaka uongozi wa mkoa Tabora kuwasaka watu waliohusika na mauaji hayo popote walipo ili sheria ichukue mkondo wake,”alisema.
Alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Chato, Charles Kabeho ambaye ni pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kuhakikisha wanawakamata wananchi wote waliovamia eneo la Nyabengo ndani Shamba la Miti la Biharamulo na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Alisema Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), haina misitu yake bali inalinda misitu hiyo kwa niaba ya wananchi kwa ajili ya manufaa ya watu wote.
Katika hatua nyingine, Kanyasu amewataadhalisha watu hao kuacha tabia ya kuwazingira maofisa misitu kuwa ni hatari kwa vile maofisa hao wanakuwa na bunduki na pindi wanapozingirwa cha kwanza wanalazika kuilinda silaha na pili kujilinda wenyewe.
“Tumeamua kuwapeleka maofisa misitu wote katika mafunzo ya kijeshi kwa muda wa miezi sita ili waweze kupambana na watu wanaodhani kila sehemu wanaweza kulima na kuanzisha makazi.
“Katika kipindi cha uongozi wangu sitaki kusikia maofisa waliojitoa kulinda na kuhifadhi misitu yetu wakiendelea kuuawa na wananchi wenye tamaa ya kutaka kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi, hakikisheni hali haijitokezi tena,”alisema.
Katika hatua nyingine, Kanyasu alionesha kusikitishwa na kasi ya ukataji miti kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini unaofanywa na wachimbaji wadogo mkoani Geita hali, itayosababisha ukame na endapo hatua za makusudi hazitachuliwa misitu mingi itatoweka.
Alisema athari za ukataji miti hiyo kwa ajili ya matimba,baada ya kumalizika mkoani humo wachimbaji hao wamelazimika kuanza kuvamia misitu ya hifadhi iliyopo Mkoa wa Kigoma na kusafirisha hadi Geita.