Hadija Omary, Lindi
Naibu waziri wa Maliasi na utalii, Constantine Kanyasu, amewashauri Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Mkoa wa Lindi kuanzisha mashamba maalumu ya ufugaji wa Nyuki ikiwa ni pamoja na kuyalinda ili kuweza kupata mazao Mengi ya asali kwaajili ya mahitaji ya soko.
Kanyasu ameyasema hayo alipotembelea banda Wizara yake katika maonyesho ya nane nane kanda ya Kusini yanayoendelea katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.
Kanyasu amesema hivi Serikali imepata soko kubwa la kuuza asali nchini Marekani ambayo mpaka sasa hawajaweza kukidhi mahitaji ya wingi wa asali inayotakiwa hivyo ni fursa kwa wakala hao kujikita katika ufugaji wa nyuki.
“Tunasoko kubwa tumepewa sisi hapa Tanzania la kuuza asali yetu nchini China, ambayo mpaka sasa hatujapeleka kwa hivyo nilitarajia nyie TFS muwe dira ya kuzalisha asali nyingi kuliko watu wengine kwa sababu pesa mnazo na wataalamu wapo na huku ndiko tunakokutengemea kwa sababu hatuna visingizio kwa kuwa nyuki wapo wa kutosha” amesema.
Amesema ili mashamba hayo ya ufugaji wa Nyuki yaweze kuwa endelevu ni vyema kukawa na usimamizi wa kutosha katika maeneo watakayoyachagua kwa ajili ya ufugaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha vyanzo vya maji yatakayoweza kutumika na nyuki hao.