22.1 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Usichokijua kuhusu hali ya maisha Ujerumani

MWANDISHI WETU

UNAPOIZUNGUMZIA Ujerumani, inakujia taswira ya taifa tajiri kabisa barani Ulaya, kwa maana linaloongoza kwa uchumi mkubwa.

Kiwango cha ukosefu wa ajira kiko chini ya asilimia sita, bei za nishati na vyakula kwa wastani ziko chini kulinganisha na mataifa mengi ya Ulaya.

Mwanachama huyo namba moja kwa nguvu na ushawishi katika Umoja wa Ulaya (EU), mbali ya kuwa nchi yenye uchumi imara, pia ni ya pili duniani kwa usafirishaji wa bidhaa ng’ambo na ya nne kwa ukubwa wa uchumi duniani.

Wakati mdororo wa uchumi ulipoiathiri dunia ukianzia Marekani katika miaka ya mwisho ya utawala wa Rais George Bush, kabla ya kusambaa hadi Ulaya mwanzoni mwa mwongo huu, Ujerumani ilikuwa moja ya mataifa machache duniani yaliyobakia imara.

Ilihali mataifa mengi kama vile Ugiriki, Ureno, Italia na mengine mengi yakitikisika vibaya kiasi cha kukaribia kufilisika na kuufanya Umoja wa Ulaya kuyumba na kuelekea kumeguka.

Kwa kushirikiana na mataifa mengine wanachama, hasa yanayoifuatia kwa ukubwa wa uchumi barani humo kama vile Ufaransa, Ujerumani ikachukua hatua mbalimbali kujaribu kunusuru hali. Juhudi hizo zimeweza kulituliza jahazi la EU lililiokuwa likienda mrama kiasi cha kuifanya Uingereza ambayo imekuwa haikikubali chombo hicho kuchekelea hali hiyo, kwamba ilikuwa sahihi kukipinga.

Moja ya mamia kwa maelfu ya familia zinazoishi bila umeme Ujerumani

Lakini kwa sasa ni EU inayochekelea si Uingereza, ambayo mwaka 2016 ilipiga kura ya kujiondoa kutoka chombo hicho, lakini baadae ikaonekana kujuta kuchukua uamuzi huo.

Ndio maana haishangazi, kwa hili wimbi linaloitikisa dunia kwa sasa la wahamiaji wanaojaribu kusaka maisha bora Ulaya limevuma zaidi Ujerumani kuliko hata Italia, ambako ni lango kuu la kuwapokea wakitokea Afrika au Asia.

Wakimbizi hawa wengi wao huishia kufa kwa kuzama baharini au kwa maradhi ama kuishia makambini wakiomba msaada au kuteseka utumwani huelekeza macho Ujerumani.

Huvutiwa zaidi na Ujerumani kwa sababu ya utajiri, uimara wa uchumi na ubora wa maisha walionao, kulinganisha na mataifa mengine wanachama wa EU.

Lakini licha ya taswira hiyo njema inayoonesha neema na ustawi wa taifa hilo, kuna upande wa pili wa shilingi wa taifa hilo.

Kwamba, umasikini upo nchini Ujerumani, licha ya kwamba hakuna makazi duni au holela kama yale tunayoyaona hapa kwetu.

Ni upande hasi, ambao maelfu ya Wajerumani wanaishi maisha ya udhalili, hushindwa kumudu kulipia bili za umeme na hata kupata mlo na mahitaji mengine kutokana na umasikini.

Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi ya Shirika la Misaada la Caritas, maelfu ya Wajerumani wanaishi bila huduma ya umeme kwa sababu hawana uwezo wa kuilipia licha ya kuwa hili ni taifa tajiri kabisa Ulaya.

Ripoti hiyo ilikuja huku Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) likisema kuna ongezeko la umasikini miongoni mwa watoto kwa asilimia 2.7 nchini humo.

Aidha, inakuja huku Chama cha Kusaidia wasio na Makazi (BAG W.) kikisema watu zaidi ya 800,000 wanaishi mitaani kwa kukosa makazi rasmi nchini humo.

Kwa ushirikiano na Shirika la Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi Barani Ulaya (ZEW), Caritas limelivalia njuga suala hili na kulifanyia utafiti wa kina.

Matokeo ya uchunguzi, ambayo yametolewa rasmi hadharani yameonesha hali ilivyo ya kutisha.

Kwa mujibu wa utafiti huo, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, familia 328,000 zimelazimika kukatiwa huduma za umeme na nyingine milioni 6.6 zikiwa hatarini kufungiwa huduma hiyo muhimu.

Kimsingi kukatiwa umeme ni jambo la mwisho kabisa linalofanywa na kampuni ya kutoa huduma hizi ikiwa mtu anashindwa kulipia gharama hizo.

Kwanza, mtu hupewa muda wa kulipia gharama ya umeme aliotumia endapo alibakisha deni la zaidi ya Euro 100 sawa na zaidi ya Sh 300,000 za Tanzania.

Kwa kawaida, hutumiwa mara kadhaa barua ya kumpa onyo na baadaye kutahadharishwa kwamba atakatiwa umeme.

Kwa wengi waliokutwa na hali hiyo, walifungiwa huduma hizi pale tu gharama zilipokuwa zimefikia kiwango kikubwa mno.

Si tu wanatakiwa kulipia deni hilo kabla ya kurudishiwa umeme, bali pia wanatakiwa kulipia tena gharama za kurudishiwa huduma hizo.

Ada ya kurudishiwa huduma ya umeme inaweza kufikia hadi Euro 200 sawa na zaidi ya Sh 600,000.

Lakini kwa wengi ambao ni watu wanaopokea ruzuku kutoka serikalini ya kuwasaidia kuishi na wale wenye kipato cha chini kabisa nchini Ujerumani, hata kiwango hicho bado ni kikubwa kwao na mara nyingi hawawezi kukimudu.

Idadi ya watu waliofungiwa huduma ya umeme kwa kipindi cha mwaka mmoja imebakia katika kiwango kile kile, ikimaanisha hawakuweza kujikomboa kuilipia.

Lakini hadi sasa haijawa wazi ni kina nani hasa ndio waathirika zaidi wa janga hili.

Suala la kufungiwa huduma za umeme nchini Ujerumani linazitia hofu familia nyingi ambazo ziko hatarini.

Walio wengi kabisa wanaokabiliwa na kitisho hiki ni familia zenye mzazi mmoja – nyingi zikiwa ni zile zenye kipato kidogo zikiishi chini ya mpango wa ‘Herz Vier’, yaani posho kwa  watu wasio na ajira.

“Kundi kubwa kabisa lililoingia katika hali hiyo ni la watu wenye elimu ndogo na ambao wanazongwa na mzigo mkubwa wa madeni na wameshindwa kuelewana katika utatatuzi wa suala hilo na idara za serikali zinazohusika,” unasema utafiti huo wa Caritas.

Kwa  mujibu wa utafiti huo, hata familia inayoishi na mtoto mchanga wa miezi sita inakatiwa umeme na kusababisha malezi ya mtoto kuwa magumu.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba kwa wengine wanaoishi katika hali hii hulazimika kuachia mtoto kama huyo kuchukuliwa na familia nyingine itakayomudu kumlea.

Ushauri uliotolewa na ZEW ni kwamba watu wanaoandamwa na madeni inawabidi kutafuta uwezekano wa haraka wa kupata usaidizi.

Inabidi kuanza kutafuta ushauri wa kupambana na madeni. Juu ya yote, watu wanapaswa kujifunza kuanza kujisaidia wenyewe kabla ya kuomba msaada.

Licha ya suala la umeme, kuna idadi kubwa ya watu wanaoshindwa kula vizuri kwa sababu ya umasikini wao, wakiwamo wastaafu, wazee, wakimbizi, wasiokuwa na ajira za kudumu na wasio na kazi kwa muda mrefu.

Kanisa Katoliki la Mtaa wa Holweide mjini Bonn ni miongoni mwa vituo vingi vinavyotoa msaada wa chakula, matunda na hata nguo kwa wenye uhitaji.

Kituo hicho hukusanya mabaki ya vyakula kutoka katika maduka ya vyakula na masoko ya bidhaa nyingine za jumla na rejareja.

Mchungaji Michael Mombartz anasema hali ya umasikini imekuwa ikiongezeka katika miaka ya hivi karibuni, jambo linalopunguza kasi ya ugawaji wa chakula.

“Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, watu hawa wenye uhitaji walipata chakula kila Jumatatu, lakini kutokana na ongezeko la idadi yao, hivi sasa hupata mara moja kila baada ya siku 10,” anasema Mchungaji Mombartz, ambaye amekuwa akisimamia ugawaji wa chakula kwa muda wa miaka 20 sasa.

Watu wengi wanashindwa kupata mlo kamili kwa siku kutokana na kutokuwa na ajira za kudumu na wengine wakiwa hawana ajira kwa muda mrefu.

Kituo hicho huandaa pia mikutano kwa watu wasiokuwa na makazi maalumu na kuwagawia mavazi pamoja na vyakula.

Kituo cha Holweide hutumia kiwango cha pato la mtu mwenye uhitaji ili kufanya mgawo huo kuwa sawa.

Kwa mujibu wa maelezo yake, kulikuwa na ongezeko kubwa la wahitaji mwaka 2014, tangu wakati huo hali haijabadilika ikimaanisha imeendelea kubaki palepale au kukua zaidi.

Kituo hicho kilianza kugawa misaada ya chakula mwaka 2014 kikiwa na watu 10 tu, lakini hadi kufikia mwaka 2017 walifika 120, wengi wa walioandikishwa ni kina mama wanaoishi peke yao, wastaafu na wale wasiokuwa na ajira kwa muda mrefu.

“Lakini sasa kuna wakimbizi wanaoishi kwenye vyumba vya kupangisha, ambao nao huchukua chakula na kwenda kupika kwenye makazi yao,” anasema Mchungaji Mombartz.

Naye Vesna Tomic, anayesaidia shughuli ya ugawaji chakula kituoni hapo anasema: “Kuongezeka kwa wakimbizi hao hakujaleta shida yoyote ya msaada. Wote wanaelewa kwamba sasa na hawa wapo, tunajua kwamba hawaji hapa kujifurahisha bali kwa sababu wanahitaji msaada.”

Mchungaji Mombartz anaona hali ni tofauti kidogo kwa sasa. Awali watu waliona aibu kufika kituoni hapo, kitu kilichomtia uchungu hasa akiwaona wazee waliofanya kazi kwa muda mrefu na sasa wanahitaji msaada lakini wanaogopa kujitokeza.

Maisha ya ugenini bila kuwa na elimu nzuri ya kukupatia ajira, ni mateso makubwa. Wakati kukiwa na wenyeji wanaoishi katika udhalili, inakuaje kwa mgeni asiye na mbele wala nyuma kumfanya atoke kimaisha?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles