MUNICH, UJERUMANI
KANSELA wa Ujerumani, Angela Merkel ametetea sera ya ushirikiano katika masuala ya kimataifa pamoja na mkataba wa nyuklia uliofikiwa na Iran.
Merkel alitamka hayo kwenye mkutano wa 55 wa masuala ya usalama uliofanyika hapa.
Merkel aliwaambia wajumbe waliohudhuria mkutano huo kuwa anauelewa wasiwasi wa Marekani juu ya mipango ya Iran ya kuimarisha nguvu zake.
Lakini ameutetea mkataba wa kuizuia Iran kuunda silaha za nyuklia, akisema mkataba huo ndiyo njia muhimu na ya pekee ya kuwasiliana na nchi hiyo pamoja na kuzuia kitisho chochote kinachoweza kutokea.
Hata hivyo, Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence, alitumia fursa ya mkutano huo kuzikosoa zaidi nchi za Ulaya juu ya Iran.
Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na Umoja wa Ulaya zimekuwa zinafanya juhudi za kuudumisha mkataba na Iran, tangu rais Donald Trump alipofanya uamuzi wa peke yake wa kuiondoa Marekani kutoka kwenye mkataba huo.