Na JUDITH NYANGE
KAMPUNI zinazochimba visima virefu vya maji katika mikoa ya Kanda ya Ziwa zimetakiwa kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchimbaji wa visima.
Kanuni hizo ni pamoja na kuwa na leseni na vibali kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.
Wito huo ulitolewa juzi na Kaimu Ofisa wa Maji Bonde la Ziwa Victoria, Ogoma Nyamuhanga, katika warsha ya wadau wa maji kuhusu sera na sheria za maji.
Alisema kampuni hizo zinapaswa kufuata kanuni na sheria za uchimbaji wa visima zilizowekwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Alisema zipo baadhi ya athari ambazo huwapata wachimbaji wa visima ikiwamo mgogoro baina yao na wasimamizi wakuu wa rasilimali za maji.
Nyamuhanga alisema athari hizo hujitokeza hasa wanapowataka kuonyesha leseni zinazowawezesha kutoa huduma hiyo na kuhakikisha wanaowachimbia visima wanakuwa na kibali cha matumizi ya maji.
Aliwataka wadau hao kuwa mabalozi wazuri katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa miongozo na sheria za wizara kwa kuwaelimisha wateja wao kuwa na vibali vya kutumia visima hivyo vinavyotolewa na ofisi ya maji bonde la Ziwa Victoria
Naye Mhaidorolojia wa Bonde la Maji Ziwa Victoria, Renatus James, alisema mwitikio wa watu na kampuni kuchukua leseni na vibali kwa ajili ya uchimbaji wa visima vya maji siyo mzuri.
Alisema bado kuna jitihada za kuwahamasisha waweze kuendana na matakwa hayo ya sheria.
“Utoaji wa vibali na leseni unashughulikiwa na ofisi ya Mkurugenzi Idara ya Rasilimali za Maji wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
“Mtu binafsi au kampuni anatakiwa kujaza fomu maalumu zilizopo katika tovuti ya wizara hiyo na kuziwasilisha katika ofisi hizo na atapatiwa leseni hiyo ndani ya siku 30,” alisema James.
Mhaidrolojia wa Ofisi ya maji Bonde la Ziwa Victoria, Isabela Tenganiza, alisema ofisi hiyo inashughulika na kukusanya, kuchakata na kutunza takwimu za ubora na wingi wa maji hivyo wananchi wote wamatakiwa kuilinda miundombinu ya kuchukulia takwimu hizo.
Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo, Meneja wa Utawala wa Kampuni ya Nyehunge, Anuari Said, alisema alikuwa hana uelewa na changamoto za watumiaji maji na utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira.
Alisema sheria hiyo ni nzuri kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji katika Ziwa Victoria lakini kupitia warsha hiyo amepata elimu ya kutosha.