30.4 C
Dar es Salaam
Saturday, December 2, 2023

Contact us: [email protected]

KAMPUNI ZINAZOCHIMBA VISIMA ZAASWA KUWA NA LESENI

 

Na JUDITH NYANGE

KAMPUNI zinazochimba visima virefu vya maji katika mikoa ya Kanda ya Ziwa zimetakiwa kufanya kazi  zao kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchimbaji wa visima.

Kanuni hizo ni pamoja na kuwa na leseni na  vibali kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.

Wito huo ulitolewa  juzi na Kaimu Ofisa wa Maji Bonde la Ziwa Victoria, Ogoma Nyamuhanga, katika warsha ya wadau wa maji   kuhusu sera na sheria za maji.

Alisema kampuni hizo zinapaswa kufuata kanuni na sheria za uchimbaji wa visima zilizowekwa na Wizara ya  Maji na Umwagiliaji.

Alisema zipo baadhi ya athari ambazo huwapata wachimbaji wa  visima ikiwamo mgogoro baina yao na wasimamizi wakuu wa rasilimali za maji.

Nyamuhanga alisema athari hizo hujitokeza   hasa   wanapowataka  kuonyesha leseni   zinazowawezesha kutoa huduma hiyo na kuhakikisha wanaowachimbia visima wanakuwa na kibali cha matumizi ya maji.

Aliwataka wadau hao kuwa mabalozi wazuri katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu  wa miongozo na sheria za wizara kwa kuwaelimisha wateja wao kuwa na vibali vya kutumia visima hivyo vinavyotolewa na ofisi ya maji bonde la Ziwa Victoria

Naye Mhaidorolojia wa Bonde la Maji Ziwa Victoria, Renatus James, alisema mwitikio  wa watu na kampuni kuchukua leseni na vibali kwa ajili ya uchimbaji wa visima vya maji siyo mzuri.

Alisema  bado kuna jitihada za   kuwahamasisha   waweze kuendana na matakwa hayo ya sheria.

“Utoaji wa vibali na leseni unashughulikiwa na ofisi ya  Mkurugenzi Idara ya Rasilimali za Maji  wa Wizara  ya  Maji na Umwagiliaji.

“Mtu binafsi au kampuni anatakiwa kujaza fomu maalumu  zilizopo katika tovuti ya wizara hiyo na kuziwasilisha katika ofisi  hizo na atapatiwa leseni hiyo ndani ya siku 30,” alisema James.

Mhaidrolojia wa Ofisi ya maji Bonde la Ziwa Victoria, Isabela Tenganiza, alisema ofisi hiyo inashughulika na kukusanya, kuchakata na kutunza takwimu za ubora na wingi wa maji hivyo wananchi wote wamatakiwa kuilinda miundombinu ya kuchukulia takwimu hizo.

Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo, Meneja wa Utawala wa Kampuni  ya Nyehunge, Anuari  Said, alisema  alikuwa hana  uelewa na changamoto za watumiaji  maji na utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira.

Alisema  sheria hiyo ni nzuri kwa ajili ya kutunza vyanzo vya maji katika Ziwa Victoria lakini kupitia warsha hiyo amepata elimu ya kutosha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles