27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

Kampuni ya Kyem General yawashika mkono watoto yatima kituo cha Buloma Foundation

Na Gustafu Haule, Pwani

KAMPUNI ya Kyem General Supplies Limited ya Kibaha Mailimoja inayojishughulisha na masuala ya uuzaji na usambazaji wa vyuma chakavu pamoja na vifaa vya ujenzi imetoa msaada wa vyakula mbalimbali kwa watoto yatima wa kituo cha Buloma Foundation kilichopo Kata ya Sofu katika Halmashauri ya Mji Kibaha.

Msaada uliotolewa ni pamoja na mchele kilo 100, unga kilo 100, sukari, mafuta ya kupikia, sabuni na mbuzi mmoja ambapo lengo la msaada huo ni kusaidia watoto hao katika Sikukuu ya Pasaka.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Josephu Mwakasyuka amekabidhi msaada huo leo Aprili 8, 2023 katika hafla fupi iliyofanyika katika kituo hicho huku akisema kampuni itaendelea kutoa misaada hiyo katika makundi mbalimbali ya jamii inayoishi katika mazingira magumu.

Mwakasyuka amesema kuwa kampuni ya Kyem inatambua kuwa watoto yatima ni jamii inayopaswa kuishi kama binadamu wengine hivyo lazima wasaidiwe katika mahitaji yao ya kila siku.

“Leo tumeona tuje kuwaona watoto yatima wa kituo hiki cha Buloma na tumewaletea vyakula mbalimbali kama vile mchele, unga, sukari, sabuni na mbuzi mmoja ili kwa pamoja viwasaidie katika sikukuu ya Pasaka,” amesema Mwakasyuka.

Aidha, Mwakasyuka amesema kampuni imeweka mipango endelevu ya kusaidia yatima pamoja na jamii inayoishi katika mazingira magumu kama vile wajane, walemavu na wazee bila kuangalia kabila wala dini.

Hata hivyo, Mwakasyuka amewaomba wadau wengine kujitokeza katika kusaidia watoto yatima waliopo katika kituo hicho na hata jamii nyingine inayoishi katika mazingira magumu kwakuwa na wao wanamahitaji sawa na binadamu wengine.

Kwa upande wake msimamizi wa kituo hicho, Baraka Peter, ameishukuru kampuni ya Kyem General Supplies kwa msaada huo kwani kiwango cha msaada walichotoa ni kikubwa na kitaweza kuwasaidia mwezi mzima.

Peter amesema kituo hicho kwasasa kina watoto 46 ambapo kati yao wakiume ni 24 na wakike 22 nakusema wengi wao wanasoma Shule ya awali, Msingi, Sekondari na watoto watatu wanasoma vyuo vikuu.

“Ninatumia fursa hii kuishukuru kampuni hii kwa msaada huu mkubwa maana inawezekana mkaona ni kidogo lakini kwa moyo wa dhati mlichotoa ni kikubwa sana na kitawasaidia watoto hawa kupata chakula cha mwezi mzima,” amesema Peter.

Hata hivyo, baadhi ya watoto yatima wa kituo hicho akiwemo, Lilian Masawe na Yohana Almasi wameishukuru kampuni hiyo kwa hatua kubwa ya kuwakumbuka katika sikukuu ya Pasaka na kuomba wasichoke kuisaidia kwakuwa changamoto zao ni nyingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles