Na Munir Shemweta, Songwe
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula amemuagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Songwe Suma Mwakasitu kwenda katika wilaya ya Songwe kushughulikia migogoro ya ardhi ndani ya mwezi mmoja.
Hatua hiyo inafuatia Naibu Waziri Mabula kubaini uwepo wa mogogoro mingi ya ardhi ambayo baadhi yake aliipata fursa ya kuisikiliza akiwa katika ziara yakeya kikazi wilayani Songwe kusikiliza na kuipatia ufumbuzi migogoro ya ardhi.
Dk. Mabula ambye yuko katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi kwenye mikoa mbalimbali nchini alimtaka Kamishna wa Ardhi  mkoa wa Songwe kwenda na timu yake katika wilaya hiyo ili ikazipatie ufumbuzi changamoto za ardhi ambazo Naibu Waziri wa Ardhi hakupata fursa ya kuisikiliza na kuipatia ufumbuzi katika mkutano wake.
Alisema, hayuko tayari kuagiza mambo ambayo hayatekelezwi hivyo alimtaka Kamishna kukaa kwenye wilaya hiyo ya Songwe na timu yake katika kipindi cha mwezi mmoja na kuitafutia ufumbuzi migogoro yote ya ardhi katika wilaya hiyo.
Awali wananchi wa wilaya ya Songwe waliwasilisha malalamiko kwa Naibu Waziri wa ardhi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Kikwajuni wakitaka kutatuliwa kwa migogoro yao ambayo kwa muda mrefu ilishindwa kupatiwa ufumbuzi.
Baadhi ya migogoro hiyo ni kutopatiwa fidia kwa maeneo yaliyochukuliwa, kukosa maeneo ya kufanyia shughuli za kilimo kutokana na muingiliano na hifadhi, migogoro ya mipaka pamoja na urasimishaji makazi holela
Mbunge wa Jimbo la Songwe Philipo Mulugo ametoa ofisi yake kwa ajili ya kufanyia shughuli changamoto za ardhi ardhi wakati kamishna wa ardhi na timu yake watakapokwenda wilyani Songwe kuzipatia ufumbuzi changamoto za ardhi katika wilaya hiyo.