26.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 30, 2022

Kamilisheni utaratibu wa bei kikomo ya saruji-Majaliwa

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara ikamilishe utaratibu wa kuwa na bei kikomo ya saruji ili kuuwezesha kila mkoa kujua bidhaa hiyo inapaswa kuuzwa kwa bei gani kwa nia ya kuondoa upandishwaji holela unaofanywa na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.

Pia, Waziri Mkuu ametoa onyo kwa mawakala wa saruji kutoficha bidhaa hiyo kwa lengo la kupandisha bei kwa sababu kitendo hicho ni sawa na uhujumu uchumi, hivyo watakaobainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Desemba 7, 2020) alipozungumza na Wakuu wa Mikoa, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Maafisa Biashara wa Mikoa, Mawakala wa saruji walioko mikoani na Wakurugenzi wa viwanda vya saruji. Kikao hicho ambacho Waziri Mkuu alikiongoza kwa njia ya televisheni akiwa ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma kilihusu suala la bei na mwenendo wa upatikanaji wa saruji.

Waziri Mkuu amesema lazima utaratibu wa kuwa na bei kikomo ya saruji ukamilike ili kujua kila mkoa bidhaa hiyo inapatikana kwa kiasi gani. “Mfano saruji inazalishwa Tanga au Dar es Salaam alafu Morogoro inauzwa kwa Sh 28,000 sasa Kigoma itauzwaje lazima kuwe na bei kikomo.”

Ameongeza kwa kusema kuwa suala hilo halihitaji kuundiwa bodi kwa sasa kwani vyombo vya kusimamia biashara vipo, wizara husika ipo, hivyo amewataka wahusika wote wahakikishe wanasimamia suala hilo kikamilifu ili kuwawezesha wananchi kupata bidhaa hiyo kwa bei nafuu.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuiagiza Tume ya Ushindani (FCC) ifanye ukaguzi ili kubaini kama bei za bidhaa hiyo ni shindani na zina tija kwa wananchi kwa sababu katika maeneo mengine hazina uhalisia na zinasababisha usumbufu nchini.

“…Mawakala badilikeni na acheneni na tabia ya kuficha bidhaa kwa ajili ya kuzipandisha bei, ukikutwa unatengeneza mazingira ya kuifanya bidhaa isipatikane kwa lkengo la kuipandisha bei huo ni uhujumu uchumi. Ukikamatwa na bidhaa ambayo inatafutwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yako,”.

Pia, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa Wizara ya Viwanda na Biashara watembelee viwanda mbalimbali ili kusikiliza matatizo yanayowakabili wenye viwanda na kushirikiana nao katika kuyapatia ufumbuzi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema licha ya bei ya saruji kuanza kupungua nchini, amewataka wakuu wa mikoa waendelee kufanya ukaguzi na kufuatilia mwenendo wa bei ya saruji ili kubaini kama bei wanayouziwa wananchi ni halali na wahakikishe bei ya bidhaa hiyo inaendelea kushuka.

Amesema viwanda vya saruji havina budi kupanua wigo kwa kuwa na mawakala wengi hadi vijijini ili kumudu kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa sababu mahitaji ya saruji nchini ni makubwa kwani Watanzania wanaboresha makazi yao kwa kujenga nyumba bora hadi vijijini.

Licha ya bei ya saruji kuanza kushuka katika mikoa mbalimbali nchini, imeelezwa kuwa katika baadhi ya mikoa kama Dodoma, Ruvuma, Simiyu, Tabora bado upatikanaji wa bidhaa hiyo hauridhishi na inauzwa kwa bei kubwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,335FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles