26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kamati yaikataa ripoti ya Tume ya Uchaguzi

Jonas Mushi na Bethsheba Wambura, Dar

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeikataa ripoti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) baada ya kubaini kasoro katika hesabu zake za fedha.

Pia Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), imeikataa ripoti ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kutokana na kutokuwa na maelezo yanayojitosheleza.

Taasisi hizo za serikali, jana zilijikuta katika wakati mgumu mbele ya kamati hizo ambako  ilidaiwa kuwa taarifa ya hesabu za NEC  inajichangana na inatia shaka.

Akihoji suala hilo, Mbunge wa Magomeni, Jamal Kassim Ali (CCM), alisema taarifa za fedha zinaonyesha   Sh bilioni 11.7 zilitumika   mwaka 2014 huku mchanganuo wake ukionyesha fedha zilizotumika  ni Sh bilioni 8.7 tu.

“Hapa taarifa inaonyesha matumizi ya mwaka 2014 ni Sh bilioni 5.9 pamoja na deni la mwaka 2013 la Sh bilioni 2.8,   jumla ikiwa  ni Sh bilioni 8.7 lakini kwenye hesabu za jumla inaonekana zilitumika Sh bilioni 11.7,” alihoji mbunge huyo.

Pia Kamati ilihoji malipo ya Sh bilioni 1.8 yaliyofanyika kwa wazabuni ambao hawakuwasilisha risiti za elektroniki (EFD’s) kwa mujibu wa sheria.

NEC pia ilihojiwa kuhusu upotevu wa Dola za Marekani 9,000 zilizolipwa kwa wazabuni kwa makosa. Mkurugenzi wa NEC Dk. Ramadhani Kailima alikiri makosa hayo na kila mara aliomba radhi na kuahidi   uzembe huo hautatokea tena.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hillary aliipa Tume hiyo wiki mbili   kurekebisha ripoti yake   na akaitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuthibitisha kama ilipata kodi yake kutokana na mauzo ya wazabuni ambao hawakutumia risiti za EFD.

Kuhusu REA, wajumbe wa Kamati ya PIC hawakuridhishwa na ripoti yake kutokana na kutotoa maelezo ya kutosha kuhusu hali ya miradi yake na changamoto zake.

Akitoa maagizo kwa Wakala huyo, Mwenyekiti wa PIC, Richard Ndassa (CCM) alisema ripoti hiyo haielezi ukweli na   inaweza kumponza waziri mwenye dhamana wakati wa Bunge la Bajeti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles