31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mattaka ashtakiwa tena kwa uhujumu uchumi

David MattakaNA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka, amefikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 71.

Mattaka alifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Respicius Mwijage.

Wakili wa Serikali Mkuu, Timony Vitalis, akisoma mashtaka alidai kuwa washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya Umma, Ramadhan Mlinga na Mwanasheria wa mamlaka hiyo, Bertha Soka.

Mattaka anakabiliwa na mashtaka matano, ambapo katika shtaka la kwanza anadaiwa kuwa Oktoba 9, 2007 katika ofisi za ATCL, alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini makubaliano ya kukodisha ndege A320-214 iliyotengenezwa kwa namba 630 kati ya kampuni hiyo na Wallis Trading Inc bila kufuata sheria ya manunuzi ya mwaka 2004.

Vitalis alidai katika shtaka la pili, Mattaka anadaiwa kuwa Oktoba 27, 2007 katika ofisi za ATCL Ilala, alisaini makubaliano ya kukodisha ndege hiyo bila kufuata ushauri wa kiufundi.

“Shtaka la tatu, Mattaka anadaiwa kati ya Oktoba 27, 2007 na Aprili 24, 2008 kwa kusaini makubaliano ya kukodisha ndege bila kufuata ushauri wa kiufundi aliisababishia Serikali hasara ya dola za Marekani 772,402.08 kwa kuilipa gharama za matengenezo Kampuni ya Aeromantenimiento ya Afrika Kusini.

“Katika shtaka la nne, Mattaka anadaiwa kati ya Oktoba 27 na Oktoba 29, 2007 katika ofisi za ATCL kwa kutofuata ushauri wa kiufundi, aliisababishia Serikali hasara ya dola za Marekani 35,984.82 zilizolipwa kwa Kampuni ya Lanta Textiles, Inc kwa ajili ya vifaa vya ndege hiyo.

“Shtaka la tano, Mattaka anadaiwa kati ya Oktoba 9 na 26, 2011 katika ofisi za ATCL Ilala, kwa uzembe alisaini mkataba kati ya Wallis Trading Inc ya Liberia na ATCL kwa ajili ya ndege hiyo kitendo kilichosababisha Serikali kupata hasara ya dola za Marekani 42,459,316.12,” alidai Vitalis.

Katika shtaka la mwisho, washtakiwa Mlinga na Soka wanadaiwa kuwa Machi 19, 2008 katika ofisi za PPRA walighushi muhtasari wa kikao cha kupitisha ukodishaji wa ndege hiyo.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu baadhi ya mashtaka yamefunguliwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi.

Vitalis alidai upelelezi wa kesi haujakamilika na kwa upande wa dhamana hawana pingamizi kwa mshtakiwa wa pili na wa tatu.

Vitalis alidai Mattaka ameshtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi na hasara aliyosababisha ni zaidi ya dola za Marekani 42,459,316.12.

Hakimu Mwijage alikubali kuwapa dhamana washtakiwa wengine wawili, Mlinga na Soka kwa masharti ya kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini dhamana ya maandishi ya Sh. milioni 10.

Washtakiwa hao, wa kwanza na wa pili walitimiza masharti ya dhamana, na Mattaka alirudishwa rumande hadi hapo atakapowasilisha maombi ya dhamana Mahakama. Kesi itatajwa Machi 29, mwaka huu.

Aidha, Mattaka anakabiliwa na kesi nyingine katika mahakama hiyo iliyofunguliwa mwaka 2011 akituhumiwa kutumia madaraka yake na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni moja kwa kununua magari chakavu katika kampuni hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles