27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

Kamati ya Zitto yawabana walioingiza ndege mbovu

Pg 3Na Elizabeth Mjatta,

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC), imeagizwa kufikishwa mahakamani kwa watumishi wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) waliohusika na mkataba wa ukodishaji ndege mbovu.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha taarifa ya PAC kwenye kikao kilichopokea taarifa ya ATCL, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe, alisema ukodishwaji wa ndege kutoka Kampuni ya Wallis Trading Inc. ya China kulikofanywa na wataalamu wa Tanzania kuliisababishia serikali deni la dola milioni 42.4.

Alisema hadi sasa waliofanya madudu hayo hawajachukuliwa hatua, wakati serikali inalipa hasara hiyo kuanzia Oktoba mwaka jana na kwamba hadi sasa imekwishalipa dola milioni 26.1.

“Utaratibu huu wa kuwaacha watu wanaohujumu waendelee na utumishi serikalimi haufai kwa sababu watakuwa wanafuja fedha za umma wakijua hakuna hatua yoyote itakayochukuliwa dhidi yao,” alisema Zitto.

Akirejea historia ya tukio hilo, alisema Kampuni ya Wallis ilisaini mkataba na ATCL Oktoba 2007 wa ukodishwaji wa ndege kwa kipindi cha miaka sita kwa malipo ya dola 370,000 kila mwezi, ikiwa ni gharama za kukodi ndege na Serikali iliridhia kutoa dhamana.

Alisema baada ya ndege kuwasili ilifanya kazi kwa kipindi cha miezi sita tu na ilipofika Desemba 2008, Mamlaka ya Usafiri wa Anga iliifungia ATCL kwa kushindwa kutekeleza matakwa ya usafiri wa anga, ikiwemo kurekebisha vitabu vinavyoeleza mambo ya usalama wa ndege.

Alisema ndege hiyo ilipelekwa Mauritania kwa ajili ya matengenezo ya kawaida mwezi Machi mwaka 2009 na ilipofika Julai 2009 ilipelekwa Ufaransa kwa ajili ya matengenezo makubwa baada ya kutimiza miaka 12 tangu ilipotengenezwa kwa mujibu wa taratibu za matengenezo ya ndege.

Zitto alisema mkataba wa ukodishwaji na matengenezo yote yalipaswa kufanywa na ATCL, lakini kwa sababu ya hali mbaya ya kifedha ya serikali, ndege hiyo ilishikiliwa na aliyeifanyia matengenezo hadi mkataba wa ukodishwaji ulipovunjwa Oktoba 11 mwaka 2011.

“Mbaya zaidi Wallis alimwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kumweleza nia ya kutaka kuishtaki Serikali kwa kushindwa kulipa deni hili.

“Katika kikao cha majadiliano kati ya Serikali na Kampuni hiyo Oktoba 26, 2011 walikubaliana kiasi hicho kilipwe kwa awamu kwa kipindi cha miezi sita, yaani kuanzia Oktoba 31, 2001 hadi Novemba 26, 2013,” alisema Zitto.

Alisema serikali ilifanikiwa kulipa dola milioni 1.5 tu na baadaye iliandikwa barua nyingine ya kusudio la kushtakiwa kabla ya kufanyika kwa mazungumzo mengine yaliyoiwezesha serikali kulipa dola 10,000,000 hadi Desemba, 2013.

Awali akiwasilisha taarifa ya ATCL, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Monica Mwamunyange, alisema kati ya changamoto kubwa inazolikabili shirika hilo ni pamoja na vitendea kazi na madeni makubwa ambayo yanaongezeka kutokana na riba ya wadai na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania, kwa kuwa mengi yapo katika fedha za kigeni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles