27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, December 7, 2023

Contact us: [email protected]

Zitto: Escrow ni zaidi ya Muhongo

Zitto_Kabwe_2011Fredy Azzah na Nora Damian, Dar es Salaam
SIKU moja baada ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kutangaza kujiuzulu kutokana na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika Akaunti ya Tegeta Escrow, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imesema suala hilo bado ni bichi.
Pamoja na hali hiyo, PAC imesema hadi sasa Serikali imetekeleza maazimio manane ya Bunge kwa asilimia 35.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, alisema kati ya maazimio manane yaliyopitishwa na Bunge hadi sasa ni matatu pekee yaliyotekelezwa.
Alisema suala la Akaunti ya Tegeta Escrow ni kubwa kuliko Profesa Muhongo, hivyo watu waliodhani kuondoka kwake litakuwa mwisho wanajidanganya.
“PAC itaendelea kupaza sauti ili maazimio yatekelezwe. Watu waliodhani kuwa akitoka (Profesa) Muhongo basi suala hili limekwisha wanajidanganya. Suala hili ni kubwa zaidi ya Muhongo,” alisema Zitto.
Maazimio nane ya Bunge
Akifafanua maazimio yaliyopitishwa na Bunge, Zitto alisema la kwanza lilikuwa linamuhusu Singh Seth (Mmiliki wa Kampuni ya Kufua umeme ya Pan African Power Limited (PAP) na watu wengine waliotajwa na taarifa ya PAC.
Azimio hilo lilitaka watu hao kuchukuliwa hatua na vyombo vya sheria kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na Miamala ya Akaunti ya Escrow na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi unaoendelea kuhusika katika vitendo vya jinai.

Zitto alisema mpaka sasa ni vidagaa tu wamefikishwa mahakamani kuhusiana na suala hilo.
“Waliofikishwa mahakamani ni wapokeaji tu na sio watoaji, waliopewa fedha kupitia Stanbic hatujawaona mahakamani.
Alisema kuwa, ofisa mmoja wa PAP (jina tunalihifadhi kwa sasa) alitoa fedha nyingi sana kutoka Benki ya Stanbic hivyo anapaswa kuchunguzwa ili ijulikane ni wapi alipeleka fedha hizo.
Kuhusu umiliki wa mitambo ya IPTL ambayo Bunge liliazimia kuwa Serikali iangalie uwezekano wa kuichukua na kuimilikisha kwa Tanesco kwa mujibu wa sheria za nchi bado pia halijaguswa.
“Suala la msingi sana la umiliki wa IPTL bado kabisa kushughulikiwa, bado kabisa. PAC haikumaanisha utaifishaji bali ni kwamba hakuna haja ya IPTL wakati umeme wao hatutauhitaji kabisa,” alisema Zitto.
Alisema azimio la tatu ambalo lilihusu mapitio ya mikataba ya umeme kama ilivyoagizwa kwenye kamati teule ya Bunge iliyoshughulikia suala la Richmond, mpaka sasa hakuna taarifa yoyote ya utekelezaji wake.
Kuhusu azimio la nne lililohusu kuundwa kwa chombo maalumu cha kushughulikia rushwa kubwa kubwa na lile la tano la kuundwa kwa tume ya kuchunguza majaji waliohusishwa na kashfa hiyo, alisema utekelezaji wake ni bado ingawa kuna muda wa kulishughulikia.
Alisema azimio la sita lililohusu kuzitaja benki za Stanbic na nyingine zilizohusishwa na sakata hilo kuwa ni vyombo vya utakatishaji fedha, bado kabisa halijafanyiwa kazi.
Maazimio ya Bunge yaliyofanyiwa kazi mpaka sasa ni lile la saba ambapo Profesa Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, wameachia nafasi zao huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi, akiwa amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.
Pia Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco waliotakiwa kuwajibishwa, tayari muda wao ulishaisha na tayari bodi mpya imeteuliwa.
Pamoja na hilo azimio la nane lililokuwa likiwahusu wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge, William Ngeleja, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, Andrew Chenge aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Victor Mwambalaswa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, tayari Spika Anne Makinda alishatangaza nafasi zao kuwa ziko wazi.
Hata hivyo, azimio la kwanza limeanza kutekelezwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuwafikisha mahakamani watu waliohusika na kashfa hiyo, ingawa Zitto anasema bado ni vidagaa vinavyofikishwa mahakamani.
Juzi akitangaza mbele ya waandishi wa habari kuhusu uamuzi wake wa kujiuzulu, Profesa Muhongo alisema kutamaliza mjadala wa Escrow ambao ulisababisha shughuli za maendeleo kusimama.
Kutokana na mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, wadau mbalimbali wakiwemo wasomi na wanasiasa wametoa maoni yao kuhusiana na baraza hilo.
DK. LWAITAMA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Azavel Lwaitama, alisema mabadiliko hayo yanaashiria kuwapo kwa upungufu katika Katiba ya mwaka 1977 na Katiba inayopendekezwa.
“Rais anateua mawaziri na kuwaapisha bila majina yao kuthibitishwa na bunge, hali hii haisaidii kuwa makini katika utendaji.
“Angekubali mfumo uliopendekezwa kwenye rasimu ya Jaji Joseph Warioba ingemsaidia kupunguza uwezekano wa kuteua watendaji ambao si waadilifu,” alisema Dk. Lwaitama.
Hata hivyo, Dk. Lwaitama alishangazwa na kitendo cha kuachwa kwa mawaziri aliodai kuwa ni mizigo kwani hata Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilishapendekeza waondolewe.
Pia alitilia shaka uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, kwa kusema kuwa hawezi kuleta jipya kwani hata utaalamu wa madini hana.
PROFESA MPANGALA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alisema mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri hayawezi kuleta maajabu kwa sababu muda uliobaki ni mfupi.
“Mimi nilitarajia angeziba mapengo mawili ya waziri wa ardhi na waziri wa nishati na madini kwa sababu muda umebaki mfupi kuliko kupangua sehemu kubwa ya baraza,” alisema Profesa Mpangala.
Kuhusu kujiuzulu kwa Profesa Muhongo, alisema waziri huyo angejijengea heshima kama angejiuzulu mapema wakati bunge lilipopitisha maazimio manane.
“Alipaswa kujiuzulu mapema kwa sababu ilikuwa ni wazi kwa nafasi yake kashfa kubwa kama ile imetokea kwenye wizara yake alitakiwa kuwajibika…sasa anajiuzulu dakika za mwisho baada ya presha kubwa amechelewa sana,” alisema.
Dk. BANA
Mhadhiri wa UDSM, Dk. Benson Bana, alisema mabadiliko hayo hayawezi kuleta tija katika utendaji serikalini kwa sababu muda uliobaki ni mfupi.
“Imebaki miezi tisa tu ya kufanya kazi sasa utaleta mabadiliko gani katika wizara, wengine watatumia miezi mitatu hadi sita kujifunza kazi za uwaziri na kuielewa wizara,” alisema Dk. Bana.
Dk. Bana pia alikosoa uteuzi huo kwa kuhamishwa kwa baadhi ya mawaziri katika wizara nyeti.
“Mwakyembe alikuwa anafanya vizuri lakini kule alikopelekwa (Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki) ni kama amekwenda kupumzika tu. Kuna wizara nzito ambazo zinahitaji watu wazoefu siyo matamshi mengi kuliko matendo,” alisema.
Kuhusu kujiuzulu kwa Profesa Muhongo, alisema waziri huyo amejiuzulu baada ya kuwapo shinikizo kubwa hivyo haesabiki kama amejiuzulu kwa matakwa yake.
JUKWAA LA KATIBA
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (JUKATA), Deus Kibamba, alisema baraza hilo halina mwelekeo na limedhihirisha kuwa Rais ana washauri wabovu wa masuala ya kisiasa.
“Taifa letu linapitia wakati mgumu, nilitegemea Rais alete watu watakaomsaidia kupambana kwenye hali ngumu kama hii lakini sijaona.
“Kazi kubwa ya Rais ni kupanga timu nzuri ya watendaji lakini kwa mabadiliko haya hakuna mwelekeo, bunge linavunjwa Julai angefukuza walioshindwa kazi na kuleta wapya,” alisema Kibamba.
TUCTA
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Nicholas Mgaya, alisema mabadiliko hayo ni mazuri lakini baadhi ya mawaziri walipaswa kupumzishwa kwa sababu tayari wamechoka.
“Kuna watu wamechoka, wamezeeka wangepaswa kupumzishwa, wanawaacha wakati kuna vijana wengi makini wako nje,” alisema Mgaya.
MTATIRO
Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema: “Mawaziri ni walewale, hakuna jipya, tutegemee mambo yaleyale”.
Kuhusu kujiuzulu kwa Profesa Muhongo, alisema lazima waziri huyo asaidie kwenye upelelezi nani kasababisha taifa liibiwe mabilioni ya fedha za umma.
“Mimi binafsi nampongeza kwa kukubali kuwa cheo ni dhamana. Lakini najua hakujiuzulu kwa kutaka amelazimishwa ili mkuu wa nchi apate ahueni.
“Lakini lazima atusaidie kwenye upelelezi, nani kasababisha taifa liibiwe mabilioni ya fedha za umma, hivi sasa hatuangalii ikiwa anaamini fedha zile ni za umma au la,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles