Na PENDO FUNDISHA-MBEYA
KAMATI ya uchunguzi wa sakata la ufisadi wa mradi wa ujenzi wa Soko la Mwanjelwa tayari imewasili jijini Mbeya mahsusi kwa kuwachunguza watuhumiwa 11 wanaodaiwa kutekeleza madudu hayo, hivyo kuisababishia Serikali hasara ya mamilioni ya fedha.
Taarifa ya ujio wa kamati hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kimo, wilayani Rungwe.
Katika maelezo yake alisema kamati hiyo imeanza utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya mkoani humo mwishoni mwa mwezi uliopita.
“Ugeni huu umewasili leo(jana) na tayari umeanza kuifanya kazi yake, ambapo kazi kubwa itakayofanywa na kamati hiyo ni kuchunguza na kuwahoji watuhumiwa na kisha kufungua mashitaka dhidi yao,” alisema.
Alisema, kwa mujibu wa maelezo ya kamati, kazi hiyo itafanyika ndani ya siku sita na baada ya hapo itaelekea wilayani Rungwe kwa ajili ya kuchunguza malalamiko ya wakulima wa chai yaliyotolewa kwa Waziri Mkuu.
Makalla alisema wakulima hao kwa sasa wametishia kutolima zao la chai kwa madai ya kutonufaika nalo, kutokana vitendo vya ukiritimba wa manunuzi unaofanywa na bodi ya chai, hivyo kulazimika kuuza zao hilo kwa mnunuzi mmoja na kwa bei isiyo na tija kwao.
Waziri Mkuu aliunda kamati hiyo baada ya kupokea taarifa maalumu ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo ilibaini kuwapo kwa ubadhirifu wa fedha zilizotumiwa kwenye ujenzi wa soko hilo.
Kwa mujibu wa Serikali, ujenzi wa soko hilo ulipangwa kutumia Sh bilioni 19, lakini gharama ya ujenzi huo ikapanda hadi Sh bilioni 26 na ghafla gharama ikapanda na kufikia Sh bilioni 63, hatua ambayo iliibua maswali mengi.
Kwa mantiki ya ufafanuzi wa ripoti hiyo, Waziri Mkuu aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mbeya, kufungua mashitaka kwa watuhumiwa hao, wanaodaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 63.448, huku akiunda kamati ya uchunguzi itakayosaidiana na Takukuru kuandaa mashitaka kwa watuhumiwa hao.