25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

KAMATI YA BUNGE YAMTAKA DED IGUNGA KUACHIA NGAZI

Na SARAH MOSES – DODOMA


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga, Revocatus Kuuli, kuachia ngazi kutokana na kukaidi kutekeleza maagizo ya kamati hiyo yaliyotolewa tangu Machi, mwaka huu baada ya kugundulika kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha.

Pia kamati hiyo ilishindwa kupitia hesabu za halmashauri hiyo na kuamua kuitimua kwa madai imedharauliwa kwa sababu maagizo matatu waliyokuwa wameyatoa hayajafanyiwa kazi na hakuna majibu ya kuridhisha.

Akizungumza mjini hapa jana Mwenyekiti wa LAAC, Vedasto Ngombale, alisema mara nyingi Kuuli amekuwa hapatikani ofisini kwake na badala yake hujikita katika shughuli zake binafsi za uwakili.

Alisema maagizo waliyokuwa wameyatoa kwa halmashauri hiyo ni pamoja na kufanyika ukaguzi maalumu katika Mradi wa maji Bulangamirwa unaonekana kuna ubadhirifu na kuchukuliwa hatua kwa msimamizi wa mradi huo ambaye kwa sasa amehamishiwa Nzega.

Ngombale ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CUF), alisema kamati ilibaini kuwa wakuu wa idara ya fedha na mipango walifanya uzembe wa kutowasilisha vitabu vya miradi ya maendeleo kwa mkaguzi hivyo wakaagiza wafunguliwe mashtaka jambo ambalo halmashauri hiyo haijatekeleza kwa muda wa miezi mitano sasa.

“Viongozi wa halmashauri hii hawana dhamira ya dhati ya kushughulikia maagizo ambayo tumewapa, mkurugenzi tumekuwa tukimuuliza mara kadhaa lakini utetezi wake ni kwamba mara nyingi hayupo ofisini anaenda kwenye kazi nyingine hivyo anawaachia ofisi wasaidizi wake jambo ambalo tunaona ni mzaha.

“Kama mkurugenzi unaona kazi hii haikufai jiuzulu ili uache wanaotaka kufanya kazi ya kuwatumikia wananchi wafanye, haiwezekani uwe unajibu kwamba ulienda kwenye kazi ya TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania) unaacha ofisi na wasaidizi kila mara,” alisema.

Kwa upande wake, Kuuli, aliiambia LAAC kuwa bado anahitaji kufanya kazi na kufafanua kuwa hoja zote zilizotolewa walizijibu na kuzifanyia kazi huku akionyesha vielelezo katika vitabu jambo ambalo Ngombale alilipinga na kueleza kuwa halipo katika vitabu vya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kama taratibu zinavyotaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles