24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

KALONZO: MAREKANI INASAMBARATIKA, HAIWEZI KUTUSAIDIA

NAIROBI, KENYA


KINARA mwenza wa muungano wa upinzani wa NASA Kalonzo Musyoka, ameyashambulia mataifa ya magharibi hasa Marekani ambayo alisema inasambaratika na hivyo haina uwezo wa kuisaidia Kenya.

Akizungumza pamoja na vinara wenzake wa muungano huo kwenye Bustani ya Uhuru mjini hapa juzi, Kalonzo alisema Kenya haihitaji msaada wa mabalozi wa mataifa ya magharibi na kwamba mpango wake na Raila Odinga kuapishwa uko palepale.

Kiongozi huyo wa Chama cha Wiper, alimlaumu Balozi wa Marekani Robert Godec kwa kile alichosema kupenda kuingilia masuala ya Kenya ilihali kwao (Marekani) kuna waka moto.

“Balozi wa Marekani anapaswa kuisaidia nchi yake ambayo kwa sasa inachukuliwa kuwa imesambaratika. Wamarekani wanaandamana kila siku kwa sababu hawana imani na uongozi. Watu kote duniani wanalilia uhuru, ukweli na haki hali ambayo haina tofauti na hapa Kenya,” alisema.

Musyoka pia alisisitiza kuwa yeye na Odinga walishinda Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8 2017 lakini wakaibiwa kura.

“Tulishinda uchaguzi huo peupe lakini Mahakama ya Juu ilipoamuru Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ifungue kanza data, Jubilee iliwatisha wakakataa kufungua. Kama wanaamini hatujashinda, basi waagize kanza data zifunguliwe ili ulimwengu ujue ni nani msema kweli,” akasema.

Wakizungumza wakati wa mkutano wa Bunge la Wananchi katika bustani hiyo, Odinga alisema viongozi wa Jubilee wanarudisha Wakenya siku za giza kwa kutaka kuongoza wao na kubadilisha katiba.

Alimshambulia Kenyatta kwa hatua yake ya kuteua wakuu wa polisi akisema hiyo kinyume cha sheria.

“Wakenya wanapaswa kuwakataa Uhuru na Ruto na wapinge mipango yao ya kutaka kuturudisha siku za nyuma. Sisi tunaenda Kanaani nao wanataka kuturudisha Misri.”

Odinga alisema NASA itafanya mikutano Suswa eneo la Narok, Migori na Kisii kabla ya kuelekea Nairobi katika sherehe ya kuapishwa kwake.

Kalonzo pia aliishambulia Jubilee kwa kishindwa kutimiza ahadi zake, ikiwemo elimu ya bure ya sekondari.

“Waliiga mipango yetu ambayo ilikuwa tumeipanga vilivyo na sasa wameshindwa kuitekeleza. Mmeona elimu ya bure nyinyi?” akauliza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles