Na TERESIA MHAGAMA-KIGOMA
WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amesema wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme katika Kijiji cha Kidahwe wilayani Kigoma, watalipwa fidia kabla ya ujenzi kuanza.
Dk. Kalemani aliyasema hayo jana wakati wa ziara ya kikazi wilayani Kigoma na Uvinza ambapo alikagua eneo kitakapojengwa kituo cha kupoza umeme wa gridi ambao utatoka Tabora hadi Kigoma kwa msongo wa kilovoti 132.
“Tunawapongeza wananchi kwa kupokea mradi huu kwa mikono miwili, lakini tunajua kuna wananchi wanaopaswa kulipwa fidia kwani ni haki yao ya msingi.
“Kwa hiyo, hatutaweza kuanza ujenzi mpaka mtakapolipwa fidia kwanza, kwani Serikali imetenga Sh milioni 722 kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi na makadirio yameshafanyika na taratibu za uhakiki zinaendelea ili wananchi wapate kile wanachostahili.
“Kwa ujumla, ujenzi utaanza wakati wowote baada ya malipo hayo kukamilika,” alisema Dk. Kalemani.
Akiwa wilayani Uvinza, Waziri wa Nishati alikagua kazi ya usambazaji umeme vijijini katika Kijiji cha Kazuramimba na Nyanganga, ambapo mkandarasi wa Kampuni ya CCCE Etern anaendelea na kazi.
Katika Kijiji cha Kazuramimba, Dk. Kalemani alikuta mafundi wakiendelea na kazi ya ufungaji wa transfoma, ambapo msimamizi wa mradi huo kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), alimweleza kuwa kazi hiyo inakamilika leo na baada ya hapo, wataanza kuunganisha umeme kwa wananchi.
Akiwa katika Kijiji cha Nyanganga, Dk. Kalemani alimwagiza mkandarasi kuhakikisha kijiji hicho kinapata umeme Machi 31, mwaka huu na pia aliiagiza Tanesco watoe elimu kwa wananchi ili wahamasike kuunganisha umeme kwenye nyumba zao.