20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Kalaghe: Madiwani Maswa simamieni mapato

Na Samwel Mwanga,Maswa

MADIWANI katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wametakiwa kuwa wakali katika kusimamia mapato na kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato hayo kwani huo ni mojawapo ya wajibu wao katika halmashauri hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa akisoma taarifa ya miradi mbalimbali iliyotekelezwa katika halmashauri hiyo hadi kufikia Mwezi Juni mwaka katika kikao Cha baraza la Madiwani kilichofanyika mjini Maswa.

Akitoa salamu za Serikali katika kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Maswa, Athuman Kalaghe amesema kuwa ni wajibu wa madiwani kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha wanasimamia mapato yote yanayokusanywa na halmashauri hiyo.

Amesema kuwa ni vizuri wakasimamia vizuri mapato hayo na kuhakikisha hayapotei na kuwaonya wasiwe sehemu ya watu watakaosababisha mapato hayo kupotea.

“Kuweni wakali katika kusimamia mapato yenu,msiwe kimya maana mnajua mianya ya mapato kupotea ni wajibu wenu kuhakikisha mapato yenu hayapotei.

“Nanyi madiwani msiwe sehemu ya miongoni mwa watu wanaosababisha mapato kupotea kuweni wakali kabisa katika jambo hili,” amesema Kalaghe.

Amesema kuwa hizo kamati wanazoziunda kwa ajili ya kukusanya mapato ya halmashauri hiyo kwa mujibu wa kanuni zao ni vizuri zikafanye kazi kwa uadikifu kwa lengo la ustawi wa wilaya hiyo.

Pia, amewataka wasimamizi wa miradi yote ya maendeleo kuwapa wananchi taarifa za miradi hiyo katika kila hatua ya utekelezaji wake.

Aidha, amewataka watendaji kushirikiana kwa karibu na waheshimiwa madiwani katika kusimamia mapato ya Halmashauri ili kuweka wazi kila mapato yanayoingia.

Akitoa taarifa ya mapato na matumizi katika halmashauri hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Maswa, Maisha Mtipa amesema kuwa hadi kufikia Mwezi Juni mwaka huu wameweza kukusanya kiasi Cha Sh bilioni 3.6 kupitia vyanzo vya ndani sawa na asilimia 87 ya makadirio yao ya kukusanya kiasi cha Sh bilioni 4.1

Amesema kuwa kwa sasa wataanza kutekeleza Mradi wa ujenzi wa jengo jipya la Utawala la halmashauri hiyo litakalokuwa na ghorofa Moja katika eneo la Ng’hami kwani tayari wameshapokea kiasi cha Sh bilioni moja.

“Ujenzi wa jengo jipya la Utawala katika halmashauri yetu ya Maswa utaanza Mwezi huu Septemba tayari tumeshampata fundi na zile changamoto tulizokuwa nazo zimemalizika pia katika kiwanda chetu cha chaki tumeshafunga mitambo yote na Mwezi huu tukipata fedha tulizohaidiwa na serikali tutaanza majaribio ya uzalishaji mara moja,”amesema.

Awali, wakijadili taarifa ya Fedha, Mipango na Utawala kulizuka majadiliano makali kufuatia kitendo cha madiwani kuingizwa kwenye timu ya ukusanyaji ushuru wa pamba ya halmashauri hiyo huku wakitaka kujua ni kanuni,sheria na mwongozo gani uliotumika.

“Mheshimiwa Mwenyekiti nataka kufahamu ni kanuni, sheria na mwongozo uliotumika kuwaingiza waheshimiwa madiwani katika timu ya ukusanyaji wa mapato ya halmashauri na tumeshampata taarifa kuwa tayari wamelipwa kiasi cha Sh milioni 12 niombe na vyombo vya usalama viko humu vilijue jambo hili ambalo lina harufu ya rushwa, tunataka fedha hizo zorudishwe kama kamati ya fedha ilivyoazimia kwenye kikao chake.

“Hata kama ni ushauri ulitolewa na Mkuu wa wilaya au ni agizo lake ninaomba nionyeshwe hiyo barua maana huko ni kinyume cha kanuni na sheria kwa Diwani kuwa sehemu ya timu ya watendaji wa halmashauri kwa ajili ya kukusanya mapato,” amesema Witness Philipo ambaye ni diwani wa viti maalun CCM.

Ameendelea kueleza kuwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge aliwahi kutoa ushauri kupitia baraza hilo la Madiwani mahali ambapo panafaa kujengwa jengo jipya la Utawala la Halmashauri hiyo lakini Mwenyekiti wa Halmashauri, Paul Maige aliukataa ushauri huku akihoji inakuwaje alikubali ushari huo ambao ni kinyume na miongozo ya halmashauri hapa nchini.

Akijibu hoja hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Paul Maige amesema kuwa kwa taarifa alizopata ni kuwa Mkuu wa wilaya aliteua madiwani wawili kwa lengo la uwakilishi wa wananchi kwa majimbo mawili ya Maswa Mashariki na Maswa Magharibi kuingia kwenye timu hiyo ya makusanyo ya halmashauri ili kuona kila kitu kinachoendelea.

“Mkuu wa wilaya ni kiongozi wetu wa wilaya na pia ni Mwenyekiti wa kamati ya mazao ya Wilaya aliona ni vyema akawaingiza madiwani wawili ili kuweka sura ya wananchi katika timu hiyo ya ukusanyaji mapato ya ushuru wa pamba katika halmashauri yetu na si vinginevyo,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge akizungumza kwa njia ya simu amesema kuwa ni kweli iliteua madiwani wawili ili waweze kuingia kwenye timu hiyo kwa ajili ya kuangalia jinsi mapato ya ushuru wa pamba unavyokusanywa katika halmashauri ya Wilaya hiyo.

Moja ya Maazimio katika kikao cha Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango kwa mujibu wa Hansard za kikao kilichopita kiliagiza kupatiwa kanuni,sheria na mwongozo uliotumika katika kuwaingiza waheshimiwa madiwani hao kwenye timu ya ukusanyaji wa ushuru wa pamba.

Pia waliagiza kuanzia Juni 30, mwaka huu madiwani hao waache mara Moja kujihusisha na suala la ufuatiliaji wa ushuru wa pamba kwani ni kinyume cha sheria,kanuni na taratibu za halmashauri hiyo na fedha zote walizolipwa kama posho za kujikimu wazirudishe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles