30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Kairuki awataka walimu kua chachu ya kudhibiti ukatili dhidi ya watoto

Na Asha Bani, Mtanzania Digital

Walimu wametakiwa kuchukua hatua za makusudi na kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa watoto mashuleni wanapata elimu kuhusu ukatili ili waweze kujilinda wakiwa shuleni na nyumbani.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Angellah Kairuki katika kongamano la walimu lililofanyika jijini Dar es Salaam na kukutanisha walimu wa shule za msingi na sekondari kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah Kairuki (kushoto) akikabidhi Cheti cha Shukrani kwa Kampuni ya Sukari ya Kilombero kwa kudhamini kongamano ‘Mwalimu Conference’. Akipokea cheti hicho ni Meneja wa Mawasiliano na Mahusiano wa Kampuni hiyo, Willa Haonga (Kulia). Katikati ni Mercy Mchechu, mratibu wa kongamano hilo ambaye pia ni Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Shule za Rightway.

Akizungumza wakati wa kufungua rasmi kongamano hilo, Kairuki alibainisha kuwa walimu wana wajibu wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wana uelewa wa aina za ukatili, mbinu zinazoweza kutumika katika kujilinda dhidi ya ukatili na hatua za kuchukua ili kuripoti matukio hayo pindi yanapojitokeza.

“Mbali na kuelimisha wanafunzi kuhusu ukatili, nawaasa walimu kuendelea kutoa ushirikiano kwa wazazi na wadau wengine katika mikakati mbalimbali ya kupambana na ukatili,” amesema Kairuki.

Naye muandaaji wa Kongamano hilo ambaye ni Muasisi na Mkurugenzi wa shule za Rightway, Mercy Mchechu alitoa wito kwa walimu kulinda watoto walio mikononi mwao ili kunusuru kizazi.

“Ametokea mwalimu mwingine aitwae mitandao ya kijamii, naye amekuwa na nguvu kubwa kuliko sisi. Changamoto za ukatili zinazowakabili watoto ambazo zinachangiwa na mifumo ya malezi zinaweza kurekebishika, ila tu zinahitaji mbinu na mikakati, hivyo walimu tushirikiane kwa pamoja na wazazi na wadau katika kulinda watoto,” amesema.

Mercy Mchechu, Mratibu wa Kongamano ‘Mwalimu Conference’ ambaye pia ni Mwasisi na Mkurugenzi wa Shule za Rightway akizungumza katika kongamano la walimu lililofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha walimu wa shule za msingi na sekondari ili kujadili nafasi ya walimu katika kukomesha ukatili dhidi ya watoto.

Jessica Kusikula ni mwalimu wa Shule ya Msingi Kantui kutoka wilayani Kilosa mkoani Morogoro. Ameshiriki kongamano hilo akiwa na walimu wenzake kumi kutoka wilaya mbalimbali mkoani humo. Jessica ameelezea mtazamo wake kuhusu kongamano hilo kwa kusema:

“Nina furaha kushiriki kwenye kongamano hili na natarajia kuondoka hapa na elimu ambayo itanisaidia kuwaelimisha wengine katika jamii kuhusu ukatili dhidi ya watoto mashuleni na majumbani,” amesema.

Kongamano hilo la siku moja limefanyika katika ukumbi wa Oasis Village ulioko Mbezi Beach Beach jijini Dar es Salaam na kukutanisha walimu takribani mia tano kutoka mikoa mbalimbali Tanzania ikiwemo Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Mwanza, Shinyanga, Zanzibar na mingineyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles