Zainab Iddy, Dar es Salaam
KIUNGO wa Mkenya wa Simba, Francis Kahata amesema endapo watafanikiwa kuichapa Yanga, safari yao ya kusaka ubingwa itakuwa imesalia hatua chache kuikamilisha.
Simba inakamata usukani ikiwa na pointi 68, baada ya kucheza michezo 26, ikishinda 22, sare mbili na kuchapwa mara mbili.
Wekundu hao, kesho watashuka dimbani kuumana na Yanga, katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kahata ambaye anatarajia kuwapo kwenye kikosi cha Simba kitakachoshuka dimbani katika mchezo huo, amehusika kupatikana mabao 10 ya timu hiyo, kati ya hayo akifunga manne na kutoa pasi sita za mwisho zilizozaa matunda.
Kwa ujumla Simba imepachika mabao 55 msimu huu wa Ligi Kuu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kahata alisema wanakazi kubwa ili kupata ushindi dhidi ya Yanga, ambayo kimahesabu inahitaji pointi tatu zaidi kuliko wao.
“Yanga inaonekana kuhitaji alama tatu zaidi ya sisi, hii ni kwasababu nafasi ya kuwa bingwa haina, lakini na sisi tunazihitaji pia ili kupunguza safari ya kutetea taji letu.
“Kama tutachukua pointi tatu kwa Yanga, tutakuwa tumepunguza safari kwa sababu hakutakuwa na mechi nyingine ngumu,”alisema Kahata aliyesaliwa na Simba msimu huu akitokea Gor Mahia ya kwao.
Timu hizo zilipokutana mzunguko wa kwanza, dakika 90 zilikamilika kwa sare ya mabao 2-2, Simba ilianza kufunga kabla ya Yanga kusawazisha.