Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Mshambuliaji wa timu ya Simba ya Dar es Salaam, Meddie Kagere amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Agosti Ligi Kuu ya Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2018/2019.
Kagere anayecheza nafasi ya ushambuliaji, alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Joseph Mahundi wa Azam na Ompar Mponda wa Kagera Sugar alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali, ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.
Taarifa iliyotolewa leo  na Afisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini(TFF),  Cliford  Ndimbo imesema kwa mwezi huo wa Agosti timu zilicheza michezo miwili, isipokuwa Mbao na Singida zilizocheza mechi tatu, wakati Kagera Sugar na Yanga zenyewe zilicheza mechi moja.
Katika michezo hiyo miwili ambayo Simba ilicheza, Kagere raia wa Rwanda alitoa mchango mkubwa kwa kupata pointi sita na kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi, akifunga mabao matatu, ambapo moja alifunga mchezo wa kwanza dhidi ya Prisons katika ushindi wa bao 1-0 na mawili alifunga mchezo dhidi ya Mbeya City katika ushindi wa mabao 2-0.
Kwa upande wa Mahundi naye alitoa mchango mkubwa kwa Azam kufanikisha kupata pointi sita na kushika nafasi ya pili katika msimamo, akifunga mabao mawili, ambapo mchezo wa kwanza alifunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City na lingine alifunga katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Ndanda.
Kuhusu Mponda alitoa mchango mkubwa kwa Kagera iliyocheza mechi moja na kushinda mabao 2-1 dhidi ya Mwadui, mabao yote akifunga Mponda.
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ina utaratibu wa kuwazadiwa wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka 2017/2018 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kada mbalimbali.
Kagere atazawadiwa tuzo na sh. 1,000,000 Â kwa kuibuka Mchezaji Bora wa mwezi.