23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Kagera yaja na mikakati ya kudhibiti Udumavu

Renatha Kipaka, Kagera

Mkoa wa Kagera umeweka mikakati mitano ya kuhakikisha kuwa inakabiliana na udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano ambao unafikia asilimia 39.8.

Hayo yamebainishwa na Afisa Lishe wa Mkoa, Yusufu Mriri, wakati akizungumza na Mtanzania Digital ofisini kwake na kufafanua kuwa kiwango cha lishe duni bado ni kikubwa nakwamba kama mkoa wameweka mikakati ya kuondoa tatizo hilo.

Mriri ameameitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kutoa elimu kupitia vituo vya kutolea huduma za afya ikiwamo Zahanati, Hospitali ambapo kupitia huduma za baba, mama na mtoto za kliniki akina mama watapatiwa elimu ya makuzi kwa watoto hasa juu ya lishe bora na namna yakuwalisha watoto.

“Kwa upande wa mama wajawazito wanapokwenda kliniki nao wanapatiwa elimu ya lishe kuanzia mama anapokuwa mjamzito, mpaka mtoto anapozaliwa, wakati wa kunyonyesha hadi anapofikisha miaka miwili ambacho ni kipindi muhimu sana cha kuhakikisha mtoto hapati udumavu.

“Ukiacha hiyo, mkakati mwingine tulionao nipamoja na kutumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii kutembelea kaya na kutoa elimu ya lishe bora, lakini wakiwa wanalenga akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano ili kuhakikisha wanafikisha elimu sahihi ya ulishaji,” amesema Mriri.

Amefafanua kuwa mkakati mwingine ni ule unaohusisha Wakurugenzi wa Halmashauri ambao wameingia mkataba na watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha kuwa kunakuwa na siku ya afya na lishe ya kijiji kila baada ya miezi mitatu ambapo watendaji hao watakuwa wanashirikiana na watoa hudumu za afya kwenye vituo vinavyowazunguka ili kuhakikisha wanatoa elimu ya lishe.

Mriri amesema katika kutoka elimu wanatumia vipeperushi na vyombo vya habari na kutoa matibabu ya utapiamlo hospitalini kwa watoto wale ambao wanachangamoto hiyo ili kuhakikisha elimu inawafikia wanajamii.

“Kimsingi ili kuondoa udumavu huu jamii kwa maana ya wazazi na walezi wanatakiwa kufuata Maelekezo ya kuwarisha vizuri watoto wao ili kuwakinga na udumavu na kuwafanya watoto kuwa na Afya bora.

“Tunahamasisha jamii kuwapatia watoto vyakula mchanganyiko ambavyo vina virutubisho ili wasiendelee kula chakula cha aina moja ambapo jamii imeitikia swala hilo na pale mtoto anapokuwa na tatizo wazazi wamekuwa wakiwajulisha watoa huduma wa afya na kuwapatia ushauri,” amesema.

Kutokana na utafiti uliofanyika mwaka 2018 mkoani hapa na Taasisi ya Chakula na Lishe ni asilimia 19 pekee ya watoto wanaokula vyakula mchanganyiko Mkoa wa Kagera.

Kwa upande wake Janeth Rugemarila ambae ni Muuguzi Mstaafu na mkazi wa Karagwe amesema kuwa ili mtoto awe na Afya njema inatupaswa mama kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya kwa kuwapeleka watoto kliniki kwa uaminifu wa hali ya juu.

“Akinama wa sasa hatupendi kujituma na kufuatilia kwa karibu maandalizi ya vyakula vya watoto na badala yake tumewaachia wadada wa kazi kufanya shughuli zote za malezi ya watoto kitu ambacho sio sahihi kabisa,” anasema Rugemarila.

Janeth ambaye ani mama wa watoto watano amesema kuwa kuna akina mama ambao wamekuwa wakiwapa watoto wao chipsi kama mlo bila kujali umri wa mtoto jambo ambalo ni hatari kwa afya.

“Tukumbushane akina mama wenzangu, mtoto anapofikia umri wa kuanza kunywa vitu vya ziada anatakiwa kunywa uji ambao umechanganywa mahindi, ulezi, soya, mbegu za maboga, ngano yenyewe sio unga na mchele pia katika mchanganyiko huo ulezi unatakiwa kuwa mwingi kuliko vitu vingine,” ameshauri Janeth na kuongeza kuwa mtoto anatakiwa kunywa kikombe kimoja asubuhi mchana na jioni kulingana na uwezo wa familia husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles