27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kagame kutua nchini

Paul KagameNa Jonas Mushi, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli amemwalika Rais   Paul Kagame wa Rwanda kutembelea Tanzania Julai mosi mwaka huu ambako pamoja na mambo mengine anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonyesho ya Sabasaba.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine Maige, alisema ziara hiyo ya siku moja ni mrejesho wa ziara ya Rais Magufuli nchini Rwanda.

Alisema Rais Kagame atawasili   Dar es Salaam asubuhi ambako kutakuwa na uwekaji saini  Mkataba wa Makubaliano (MoU) wa ushirikiano wa Tanzania na Rwanda katika sekta mbalimbali.

“Nimeagizwa na Rais Dk. Magufuli niutangazie umma kwamba amemwalika Rais Kagame  kutembelea Tanzania Julai mosi mwaka huu ikiwa ni mrejesho wa ziara yake aliyoifanya Rwanda hivi karibuni,” alisema Dk. Maige na kuongeza:

“Rais Kagame atawasili Ikulu asubuhi ambako kutakuwa na uwekaji saini wa makubaliano ya ushirikiano katika sekta mabalimbali na baadaye mchana wataelekea viwanja vya Sabasaba vya Mwalimu Nyerere kufungua maonyesho ya 40.

“Rais Kagame anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo na baada ya hapo jioni akiwa na ujumbe wake atakutana na viongozi mabalimbali katika dhifa itakayofanyika Ikulu”.

Hatua hii ya Rais Dk. Magufuli kumwalika Rais Kagame inaonyesha kuwapo  uhusiano mzuri  baina ya viongozi hao tofauti na ilivyokuwa wakati wa serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete.

Uhusiano wa Rwanda na Tanzania ulikuwa  shakani mwaka 2013 baada ya Rais Kagame kumshambulia kwa maneno Rais Kikwete   alipomshauri kukaa katika meza ya mazungumzo na waasi wa kikundi cha FDLR cha  Rwanda.

Mara ya mwisho Rais Kagame alikuja Tanzania Novemba 5 mwaka jana kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Magufuli na huo ndiyo ulikuwa mwanzo mwa uhusiano mzuri baina ya wakuu hao wa nchi.

Uhusiano ulionekana dhahiri kuwa mzuri baada ya Rais Magufuli kufanya ziara ya siku mbili ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alivyoingia madarakani na kufuta ziara za nje za viongozi wa serikali.

Rais Magufuli alifanya ziara hiyo Aprili 6 na Aprili 7 mwaka huu baada ya kupewa mwaliko na Rais Kagame.

Pamoja na kuwa na  mazungumzo binafsi, viongozi hao walizindua Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Rusumo kwenye  mpaka wa Tanzania na Rwanda.

Siku ya pili Aprili 7 mwaka huu walihudhuria maadhimisho ya Siku ya Mauaji ya Kimbari ambako waliwasha mwenge na kuweka mashada katika mnara wa kumbukumbu ya mauaji hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles