*Asema Chadema ni taasisi kubwa, imara
*Adai Escrow imebaki kuwa alama ya kushindwa
Na ELIZABETH HOMBO
ULIANZA kama utani na uzushi wa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini David Kafulila, amerejea ndani ya chama chake cha zamani Chadema, lakini baadaye haikuwa uzushi tena.
Katika mitandao hiyo, Kafulila alijadiliwa kwa pande mbili kuhusu uamuzi wake wa kutoka NCCR -Mageuzi kurejea Chadema ambavyo ni vyama shiriki katika muungano wao wa kisiasa (Ukawa).
Baadhi ya wachambuzi walikosoa uamuzi wake huo huku wengine wakiusifu kwamba hajaihama familia yake ya kisiasa (Ukawa) bali amerudi nyumbani.
Baadhi ya mahasimu wa Kafulila kisiasa walieleza wazi wazi kwamba, Kafulila ameshinikizwa na mke wake, Jesca Kishoa ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) ili ajiunge na chama hicho.
MTANZANIA limefanya mahojiano na Kafulila ambapo pamoja na mambo mengine, anajibu hoja mbalimbali kuhusiana na uamuzi wake huo.
MTANZANIA: Baada ya kutangaza kujiondoa NCCR-Mageuzi, zilisambaa taarifa mbalimbali katika mitandao ya jamii kuwa umeshinikizwa na mke wako, wasomaji wagependa kupata ukweli wa jambo hili.
KAFULILA: Kwanza ifahamike Chadema sikuwahi kufukuzwa, bali mwaka 2009 nilitoka mwenyewe na ninarudi mwenyewe. Lakini pia Chadema ndicho chama kilichonitengeneza kuwa na spirit ya mapambano, ujenzi wa hoja na namna ya kusimamia hoja.
Ni spirit ambayo haikuniondoka hata nilipokuwa NCCR-Mageuzi, zaidi nimekuwa na uhusiano wa karibu na Chadema miaka yote nikiwa bungeni hata kabla ya Ukawa na kabla ya kuoa. Nimeshiriki matukio mengi yaliyoandaliwa na viongozi wa Chadema hususani vijana.
Itakumbukwa kuwa hata huu mtandao wa kizazi cha kuhoji uliasisiwa kwa mara ya kwanza na vijana wanaharakati wa Chadema kwa lengo la kuniunga mkono kwenye harakati za sakata la Escrow na ndio hatimaye kwenye mtandao ikaanzishwa ajenda ya BRING BACK OUR MONEY ambayo ilisimamiwa na vijana wa Chadema.
Walikuwa wakiniunga mkono katika sakata la Escrow na zaidi vijana hawa hawa ndio walitengeneza mpaka fulana na wakahudhuria mahakamani siku zote ambazo nilitakiwa Mahakama Kuu kwenye kesi niliyoshtakiwa na mmiliki wa IPTL, Harbinder Sethi.
Hata juzi kwenye maadhimisho ya siku ya vijana duniani mwaka huu, vijana wa Chadema waliniomba mimi na Profesa Mwesiga Baregu kuwa watoa mada na nikashiriki. Nimeshiriki harakati za Chadema Morogoro kabla ya Ukawa kwa mwaliko wa Suzan Kiwanga (MB), nimeshiriki harakati za Chadema kwa kufanya ziara na Godbless Lema na Tundu Lissu katika mikoa ya Arusha na Shinyanga.
Achilia mbali Mkoa wa Mbeya ambako nilialikwa na viongozi wa Chadema nikafanya mikutano. Mke wangu Jesca nimemchangia kuandaa Jimbo la Iramba kupambana na Mwigulu Nchemba wakati wote wa kampeni na kutoa ushindani mkubwa akiwa Chadema mimi nikiwa NCCR-Mageuzi.
Hivyo ninachoweza kusisitiza ni kwamba, mke wangu hakunizuia kurudi Chadema kama ambavyo mimi sikumzuia kugombea Iramba kupitia Chadema nikiwa Katibu Mwenezi wa NCCR-Mageuzi na ni hakika amefurahi sana si kwa sababu nimejiunga rasmi na chama chake bali kwa kufanya uamuzi sahihi.
MTANZANIA: Je, unakwenda Chadema kutokana na nguvu ya Lowassa?
KAFULILA: Siendi Chadema kwa sababu ya nguvu ya Lowassa. Nakwenda Chadema kwa sababu ya nguvu ya taasisi ambayo ni Chadema. Hii ni taasisi imara na ndio sababu Lowassa, Sumaye na wengineo waliamua kuunganisha nguvu zao na wanaweza kufikia malengo ya kubadili mfumo wa utawala wa taifa hili kwani ndiyo imekuwa ajenda ya Chadema kwa miaka yote.
Ndio maana ni wito wangu kwa kila anayeamini katika haja ya kubadilisha mfumo wa utawala aunganishe nguvu kwenye Chadema kwa kuwa mwanachama au mfuasi kokote alipo kwa lengo la kufupisha safari ya mabadiliko ambayo ndiyo kilio cha Mtanzania kwa zaidi ya nusu karne sasa.
MTANZANIA: Unadhani Chadema bila Lowassa mwaka 2015 hali ingekuwaje?
KAFULILA: Chadema bila Lowassa 2015 ni jambo ambalo sina uhakika kulitolea majibu kwa sababu linahitaji utafiti. Jambo moja ni wazi kwamba, Chadema imekuwa na rekodi ya kukua kila uchaguzi.
Tangu mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na hivyo mwaka 2015 ilitarajiwa kuwa itafanya vizuri zaidi ya 2010, sasa kwa kiasi gani bila Lowassa siwezi kuwa na majibu mafupi yasiyo ya kisayansi.
MTANZANIA: Ni kitu gani kimekukimbiza NCCR-Mageuzi?
KAFULILA: Kuhusu kitu gani kimenikimbiza NCCR-Mageuzi ni wazi kilichonipeleka Chadema ndicho kilichonitoa NCCR-Mageuzi. Hivyo sababu ya mimi kujiunga Chadema ndiyo sababu ya mimi kutoka NCCR-Mageuzi.
MTANZANIA: Unazungumziaje nafasi ya NCCR-Mageuzi ndani ya Ukawa?
KAFULILA: Nafasi ya NCCR ndani ya Ukawa pia ni jambo ambalo wanaweza kulijibu wenyewe lakini kwa maoni yangu, NCCR- Mageuzi wanatakiwa wajue Ukawa ni fursa ambayo hakika wanapaswa kuitumia kama ambavyo mbali na Chadema kuitumia, CUF pia wameitumia na kupata matokeo tofauti na ya miaka yote chini ya Profesa Ibrahim Lipumba, ingawa analalamikia Ukawa.
Wameshinda majimbo 10 kwa sababu walitumia vema fursa ya Ukawa. Hivyo ni wito wangu kwa NCCR -Mageuzi, itumie vema fursa ya Ukawa kama vyama vya Chadema na CUF vilivyofanya.
Wakitumia fursa ya Ukawa kupata majimbo mengi zaidi na madiwani zaidi ni furaha ya Ukawa kwani mafanikio ya kila chama ndio mafanikio ya jumla ya Ukawa na ndiyo sababu ya kuasisiwa Ukawa.
MTANZANIA: NCCR-Mageuzi ni miongoni mwa vyama ndani ya Ukawa. Inakuwaje wewe unatoka kwenye chama mshirika wa Ukawa?
KAFULILA: Ukawa si chama ni ushirikiano. Kama ilivyo ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ukawa ni fursa ya kila chama kuitumia kufanya vizuri kwa maana ya kuongeza wabunge na madiwani na kushinda urais kwa pamoja.
Lakini fursa hiyo peke yake haina maana sana kama chama husika hakiitumii kufanikisha malengo. Ni kama vile Tanzania ina fursa kwenye Afrika Mashariki lakini inaogopa hata nchi ndogo kama Rwanda, sababu kubwa ni kwamba kuwepo kwa fursa ni jambo moja na kuitumia ni jambo jingine.
Na fursa ikiwepo usipoitumia haina maana kwa sababu hufaidi tija ya fursa hiyo. Sasa Chadema imeonesha na imejipambanua kuonesha dhamira, mipango na mikakati ya kuitumia fursa hiyo ya Ukawa kuleta mabadiliko ambayo ni malengo kwa kila chama ndani ya Ukawa.
Sasa binafsi kama mwanasiasa ninaona nitakuwa na tija sana nikiweka nguvu na akili yangu Chadema ambayo ni wazi imeweza kujipambanua. Ni wito wangu kuwa tuunganishe nguvu si tu za kila mwanasiasa mwenye dhamira kwenye chama kimoja bali tuunganishe nguvu ya mdau wa maendeleo ndani na nje ya taifa hili kwenye chama kimoja kwa kuwa mwanachama au mfuasi ili kufupisha safari ya mabadiliko tuliyoamini kwa muda mrefu.
Mabadiliko ya kuondoa mfumo uliodumu kwa nusu karne bila tija kwa maisha ya Mtanzania, mfumo ambao pamoja na kubadili sura za marais lakini kila siku inakuwa afadhali ya jana.
MTANZANIA: Unadhani wananchi wa Kigoma wamekichoka NCCR-Mageuzi? Kwa sababu Moses Machali naye amekihama?
KAFULILA: Hoja kwamba wananchi wa Kigoma wamekichoka NCCR-Mageuzi kwa sababu Machali alitoka sina hakika, kwa sababu sijui kwanini yeye alitoka akaenda ACT-Wazalendo wala sijui kwanini alitoka ACT kwenda CCM.
Lakini kifupi chama ni taasisi ambayo uhai wake ni kufanya kazi za ndani ya chama na jamii. Sasa kiasi gani NCCR inatimiza hilo pengine ni swali wanaloweza kulijibu wenyewe NCCR kwa sababu mimi si msemaji wao tena.
MTANZANIA: Ni kweli mkono wa birika ndio ulisababisha ushindwe katika uchaguzi uliopita?
KAFULILA: Mimi sikushindwa uchaguzi 2015, wala sikuibiwa. Bali nilinyang’anywa baada ya kushinda, ndio sababu fomu za matokeo Na 21B zilizoletwa na tume ya uchaguzi mahakamani za vituo 382 zilizopo mahakamani, ambazo nilipewa kwa amri ya Jaji Mkuu niliongoza.
Baada ya Jaji Wambali ambaye alihukumu kesi yangu Mei 17, 2016 na kupandishwa cheo siku chache kuwa Jaji Kiongozi kukataa nisipewe fomu hizo wala nisione na akamwelekeza Msajili wa Mahakama ya Tabora ambaye alinijibu kwa maandishi kuwa ameelekezwa na Jaji Ferdinand Wambali asinipe fomu hizo, kinyume cha sheria.
Kwani Jaji akihukumu kesi hapaswi kuingilia hatua za rufaa ya hukumu yake. Hivyo mimi siku zote ninawashukuru wananchi wa Kigoma Kusini kwa kuendelea kuniamini hata kama mfumo umeamuliwa watawaliwe na mtu asiye chaguo lao.
MTANZANIA: Pia kuna taarifa kwamba kushindwa kwako ubunge kulichangiwa na Zitto Kabwe, je, taarifa hizi zina ukweli wowote?
KAFULILA: Hoja kwamba kushindwa kwangu ubunge kulikuwa na mkono wa Zitto siwezi kulijibu kwa sababu sikushindwa. Nilishinda na fomu za kila kituo zilizopo mahakamani zilizoletwa na tume, fomu za kila kituo 21B niliongoza.
Nimejibu mapema kuwa mimi nilishinda, nikaibiwa hazikutosha kuzuia ushindi lakini kwa sababu wenye mamlaka walinihofia kwa uchafu wao walishinikiza nisitangazwe.
Sasa kama Zitto alishiriki kwa namna yoyote katika msukumo huo wa mimi kunyang’anywa ni jambo ambalo siwezi kulitolea maelezo.
MTANZANIA: Unazungumziaje nguvu ya mwanamke katika familia na hata maamuzi ya kisiasa? Unafikiri ni wakati mwafaka wa 50/50?
KAFULILA: Hoja ya 50/50 mimi ninaunga mkono siku zote, lakini katika mfumo utakaofanya wapatikane wanawake wenye uwezo wa kuchaguliwa moja kwa moja kwa wananchi.
Ni maoni yangu kwamba kila halmashauri iwe jimbo na halmashauri husika wananchi wapigie kura mwanamke na mwanamume ili kupata 50/50 kwa namna ambayo wanawake wanaopatikana watakuwa wamechaguliwa na wananchi wenyewe.
Katika familia mke ni msaidizi mkuu wa mume na ni nguzo ya malezi na makuzi ya watoto. Ndio maana nimefurahia maisha ya ndoa siku zote tangu mwaka 2014, kwa kuona nina mke ambaye zaidi ya majukumu ya kifamilia pia ni rafiki yangu katika masuala ya kisiasa.
MTANZANIA: Taarifa zilizopo ni kwamba Chadema ina mpango wa kuua Ukawa ili kibaki pekee chenye nguvu. Je, kuondoka kwako NCCR unaweza kuwa ndiyo maandalizi yenyewe?
KAFULILA: Hoja kwamba Chadema ina mpango wa kuua vyama vyote ibaki yenyewe haina mashiko hata kwa akili ya kawaida. Chukua mfano wa CUF ilivyovuna majimbo mengi Bara katika historia yake kwa kushirikiana na Chadema mwaka 2015.
Hii peke yake inathibitisha upotovu wa hoja hiyo. Bahati mbaya hoja hiyo inasukumwa zaidi na CCM pamoja na washirika wake ambao kwa vyovyote hawawezi kutamani mafanikio ya upinzani.
Kama nilivyosema awali, Ukawa ni fursa, kama ilivyo fursa ya ushirikiano wa EAC, sasa ukiona Kenya inafaidi zaidi ushirikiano wa EAC si kwamba Kenya inataka kuimaliza nchi yoyoye mwanachama bali Kenya inatimiza wajibu wake katika kuitumia fursa ya ushirikiano huo.
Hivyo Chadema kuonekana imefaidika zaidi na Ukawa kuliko chama kingine sababu ni moja tu kwamba Chadema ilijiandaa zaidi ya wenzake kutumia fursa ya Ukawa, lakini ni ukweli ulio wazi kwamba fursa ya Ukawa ipo sawa kwa vyama vyote washirika ingawa kila chama kinavuna kilichopanda.
MTANZANIA: Awali uliondoka Chadema ukikosoa mambo mbalimbali ikiwemo ubinafsi kwa viongozi. Je, hali hiyo imebadilika?
KAFULILA: Sababu zilizonifanya niondoke Chadema mwaka 2009, kwa sasa zimebaki historia kwani practically zilikwishakufa, ndio sababu awali nimetoa maelezo kwa kirefu kuhusu mahusiano yangu ya muda mrefu na Chadema nikiwa NCCR- Mageuzi.
Binafsi kama mwanasiasa na kiongozi sifungwi na historia zaidi ya malengo, lengo ni kuunganisha nguvu ya kila mwenye dhamira ya mabadiliko ajiunge Chadema. hilo lengo ni kubwa kuliko historia iliyokufa.
MTANZANIA: Una maoni gani juu ya mgogoro wa CUF na hatima ya Ukawa bila CUF ya Lipumba?
KAFULILA: Mgogoro unaoendelea ndani ya CUF ni state sponsored, ni mgogoro uliojengwa kwa mkono wa dola kwa lengo ya kuitoa CUF kwenye reli hususani mkakati wa kudai haki ya wananchi wa Zanzibar baada ya matokeo yaliyofutwa kihuni kabisa na ni aibu kwa taifa la Tanzania.
Leo Tanzania haina uhalali wa kukosoa madikteta wanaopora chaguzi katika nchi mbalimbali Afrika kwa sababu ya boriti ya uchaguzi wa Zanzibar. Ninatambua weledi wa CUF ya Maalim Seif. Huyu ni mwanasiasa nguli aliyedumu katika kilele cha siasa kwa miaka mingi.
Msimamo wa Ukawa upo wazi na umesemwa mara kadhaa na viongozi wa Ukawa akiwamo Freeman Mbowe kwamba CUF ya Maalim Seif ndiyo CUF halali ndani ya Ukawa.
Na niseme jambo ambalo huko mbele huenda likatokea, kadiri dola inavyozidi kuisambaratisha CUF ndivyo inaisukuma CUF kwenye uamuzi ambao siku moja itajutia na nguvu ya uamuzi huo kwa siasa za Tanzania haitazuilika na utakuwa mwisho na anguko la mfumo wa CCM bara na visiwani. Muda utaongea.
MTANZANIA: Je, unadhani nini kifanywe na wapinzani ili kujihakikishia ushindi mwaka 2020 na unadhani upinzani ulikosea wapi hadi kushindwa mwaka 2015?
KAFULILA: Kinachopaswa kufanywa na wapinzani ni hiki kinachofanyika sasa. Ndio maana ulimsikia Lowassa akisema mikutano ya ndani mitamu sana. Umma tayari unaunga mkono upinzani.
Hivyo kinachopaswa kufanyika na ambacho Chadema inafanya ni kujenga nguvu ya ndani ya chama ili ngazi zote ziwe na uwezo wa kusimamia, kulinda na kutetea matokeo yake bila kujali ukubwa wa nguvu za dola ambazo hutumika siku zote kuhujumu matokeo halali kwa faida ya CCM.
MTANZANIA: Vipi kuhusu tuhuma uliyowahi kuibua kuhusu kuchotwa kwa mabilioni katika Akaunti ya Escrow?
KAFULILA: Escrow imebaki kuwa alama ya kushindwa kwa mfumo katika vita dhidi ya ufisadi. Imebaki kuwa kielelezo kwamba mifumo yetu haina ubavu wa kushughulikia ufisadi hasa pale ofisi kuu inapokuwa imehusika kwa namna yoyote.
Kwangu binafsi imeniachia alama ya ushujaa na maumivu. Na sijutii kwa maumivu ninayopitia ambayo najua hakika ni matokeo ya msimamo wangu thabiti katika sakata hilo. Ni mfano mbaya wa namna Bunge lilivyopuuzwa maazimio yake na Serikali na bado Bunge lisione tatizo.
Ni kielelezo cha aibu kimataifa kwani inathibitisha kuwa bado tuna Serikali ndogo kukabili mambo makubwa hasa ikizingatiwa kuwa ufisadi huu ni wa kimataifa.