30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TUWEKANE SAWA, FAIDA NA HASARA ZA UKAWA…

Na JULIUS S. MTATIRO

 

ukawa

NIMESOMA mawazo ya Ado Shaibu, nimeona mambo kadhaa ya kufafanua kwa muktadha wa hoja yake.

Moja, anasema “…Julius Mtatiro, ambaye naye anajitambulisha kama Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Cuf…” Ado Shaibu anasema mimi Mtatiro najitambulisha kwa cheo hicho.

Ukweli ni kuwa sijitambulishi ila natambulishwa hivyo na chama changu.  Agosti 28, mwaka huu, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama cha Wananchi (Cuf) likihudhuriwa na theluthi mbili ya wajumbe wa Bara na theluthi mbili ya wajumbe wa Zanzibar, kwa kauli moja liliunda Kamati ya Uongozi ya Cuf ikiwa na wajumbe wawili na mwenyekiti mmoja wa kamati hiyo.

Kwenye uenyekiti walinipendekeza kwa kauli moja kuongoza kamati hiyo, kwa hiyo sijitambulishi kwa wadhifa huo bali ndiyo hali halisi.

Kati ya watu ambao hawakupendezwa na kukubali kwangu kupokea wadhifa huo ni pamoja na Mwalimu wangu Kitila (Profesa Kitila Mkumbo), ndugu yangu ZZK (Zitto Kabwe, kupitia kwa watu wake wa karibu), Komredi Habib Mchange (ambaye alitumia muda mwingi kuniponda).

Kaka Ezekiel Kamwaga (sympathizer mkubwa wa ACT) na mwandishi wa habari, mwalimu wangu Omar Ilyas na watu wengine kadhaa, ambao kwa kweli nawapenda na napenda changamoto zao na ni rafiki zangu.

Hoja yangu ya kueleza hayo yote ni nini, ni kumkumbusha Shaibu na ACT kuwa kwenye hizi siasa wanao ‘determine’ nani ni kiongozi wao ni wenye chama na vikao vyao, kwamba Cuf haiwezi kupangiwa viongozi na dola na vyombo vyake, na CCM na viongozi wake.

Namkumbusha Shaibu kuwa mimi Mtatiro ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Cuf na najivunia nafasi hiyo, sana. Silipwi hata senti tano kwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi.

Natumia walau saa tatu kila siku ku ‘deal’ na masuala ya uongozi wa chama na hiyo si kitu kwangu, hii ni nafasi ya kujitolea na kwa kweli ninao wajibu wa kuungana na wenzangu Bara na Zanzibar kukilinda chama dhidi ya uvamizi wa sasa ambao ACT wanauona kama ‘mchezo’.

Kwa hiyo nimuombe Shaibu mara nyingine aniite ‘Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Cuf’ bila kujificha na anaweza kumuita Lipumba kama ‘Mwenyekiti wa Cuf anayetambuliwa na Msajili wa Vyama’ maana ndani ya Cuf hatambuliki. Nilitaka kufafanua hilo.

Nikumbushe na kusisitiza kuwa, mgogoro ulioletwa na Lipumba ndani ya Cuf (kwa kutumiwa na Dola) utakapokwisha nitakikabidhi kijiti cha uongozi wa Cuf kwa watu wengine.

Jambo la pili, nakubaliana na hoja za Shaibu, lakini sielewi kwa nini amedhani kuwa andiko la Lugone lilikuwa linaishambulia ACT, sijui!

Ninachojua ni kuwa, Lugone ameandika uchambuzi mzuri sana na hata Shaibu ameandika waraka mzuri, lengo lao wote ni kutufumbua macho zaidi.

Jambo moja ambalo nataka niwakumbushe Ado Shaibu na watu wanaofikiri kwa mtazamo wake, NCCR ilikuwa na ‘base’ kubwa Kigoma (siasa za Kigoma zilivyobadilika na kuharibika kwa sababu ya upepo wa Zitto siyo ACT) ndipo ngome ya NCCR ikaondoka.

Kwa vyovyote vile, kama Ukawa ingelikuwa inavimaliza vyama ni lazima Cuf ingeanguka, lakini Cuf ya leo imetamalaki zaidi kiushindi, imeongeza madiwani na wabunge.

Ukweli ni kuwa, bila ule ushirikiano wa mwaka jana, Cuf ingejikongoja, kwa hiyo kama NCCR ingekuwa na ngome eneo jingine tofauti na Kigoma iliyobebwa na upepo wa Zitto, huenda ingefanya vizuri.

Ndani ya Ukawa kulikuwa na matatizo, ilisababisha tukakosa majimbo kama Segerea, lakini pamoja na makosa hayo bado vyama vilipanda kiushindi, Cuf imelikosa Jimbo la Segerea kwa sababu ya Ukawa, lakini imepata majimbo mengine tisa kwa sababu ya Ukawa.

Mimi ndiye muathirika wa Segerea, lakini maumivu ya Segerea si kitu kwa ushindi ambao Cuf iliupata mwaka jana kihistoria.

Baadhi ya vijana ambao mimi mwenyewe nimewakaribisha Cuf na kuwapa kadi za uanachama, leo wengine ni wabunge, mimi si mbunge, najivunia hao kadhaa kuliko mimi mmoja.

Hao ndiyo faida ya Ukawa na kwa uwazi kabisa mimi najivunia Ukawa.

Mwisho, nataka kujadili kichwa cha habari cha andiko la Shaibu “Kifo cha NCCR, msingi wake ni Ukawa,” nimkumbushe Shaibu na mashabiki wa ACT kuwa kabla NCCR haijafa nadhani ACT itakufa kwanza.

Leo Zitto akiondoka ACT ‘automatically’ chama kitakufa bila mjadala, Lipumba aliondoka Cuf mwaka jana lakini Cuf ilisimama imara na ikapambana.

Mimi huviogopa vyama ambavyo kwa hakika vinajengwa juu ya misingi ya mtu mmoja mmoja, hivyo ni vyama hatari sana na kwa mtazamo wangu uhai wa vyama hivyo hutembea kwenye mfuko wa mtu husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles