Na Derick Milton, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, amewaagiza Wakuu wa Wilaya zote mkoani humo, kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kuanza shule wanapelekwa kuanza na kwamba jambo hilo siyo hiari bali ni lazima.
Kafulila amesema kuwa wazazi na walezi wa watoto ambao wanatakiwa kwenda shule wanatakiwa kuelewa kuwa hawana hiari kwa watoto wao kwenda kuanza shule bali ni lazima.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa maagizo hayo leo Alhamisi Desemba 30, 2021 wakati akipokea madarasa 449 ya Uviko-19 kutoka kwa wakuu wa wilaya mkoani humo, ambapo ameeeleza kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule ni lazima wapelekwe shule.
“Wakuu wa wilaya baada ya ujenzi wa madarasa haya ya Uviko-19 kukamilika kwa asilimia 100 mkoa mzima, sasa hakikisheni wanafunzi wote ambao wanatakiwa kwenda kuanza shule wanapelekwa kuanza.
“Wazazi na walezi wanatakiwa kuelewa kuwa kupeleka mtoto shule siyo hiari ni lazima na kama serikali lazima tusimamie hilo, wakuu wa Wilaya hakikisheni hakuna mtoto atakayeshindwa kuanza shule, iwe shule ya msingi (chekechea) iwe Sekondari kidato cha kwanza,” amesema Kafulila.
Akizungumzia ujenzi wa madarasa hayo, Kafulila amesema kuwa mkoa wa Simiyu ulipewa kiasi cha Sh bilioni 8.9 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 449 yakiwemo ya Sekondari 380 na shule shikizi 69.
Amesema kuwa ujenzi wa madarasa hayo yote umekamilika na mkoa uko tayari kwa ajili ya kupokea wanafunzi wote ambao watatakiwa kuanza shule ambapo alizipongeza kamati zote zilizozohusika kusimamia ujenzi huo.
“Nizipongeze kamati zote ambazo ambazo zimehusika katika ujenzi wa madarasa haya, mmefanya kazi kubwa sana, tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa fedha hizi ambazo zimewezesha ujenzi wa madarasa yote haya,” amesema Kafulila.
Aidha, kiongozi huyo amewataka wananchi kwenye maeneo ambako madarasa hayo yamejengwa kuhakikisha wanayatunza na kuyatumia kwa kazi iliyokusudiwa huku akiwataka waone kama zawadi kutoka kwa rais.
“Kimsingi kama rais asingelifanya hivi, wananchi sasa hivi mgelikuwa naangaika kujenga madarasa lakini kwa fedha hizi hamjatoa mchango wowote na muda huu mnautumia kwa ajili ya maendeleo yenu, lazima tumpongeze rais wetu na kumshukuru,” amesema Kafulila.
Malimbo Buhalata mkazi wa mtaa wa sina amesema wanamshukuru Rais Samia kwa kuwajengea vyumba hivyo vya madarasa kwani awali watoto wao walikuwa wakitembea umbali wa kilometa sita kwenda mpaka shule.
Ameomngeza kuwa kwa sasa watoto wao watapunguza kuchoka kutokana na kutembea umbali mrefu na kuwahi shuleni kwa ajili ya kupata vipindi kwa wakati.
Nae, Ahadiel Mohamed, amesema madarasa hayo yanakwenda kuondoa vikwazo vyote vya wazazi kuwapeleka watoto wao shule na kuwasaidia watoto hao kutimiza malengo waliyonayo.