Upendo Mosha – Moshi
Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro, linamshikilia aliyekuwa mgombea udiwani wa Kata ya Mawenzi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), African Mlay kwa tuhuma za kuchapisha habari za uongo mtandaoni kuhusiana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu Aprili 6, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, James Manyama, amesema mtuhumiwa huyo anashikiliwa tangu Aprili 4 mwaka huu alipokamatwa Mtaa wa Market saa tisa alasiri mjini hapa.
Amesema mtuhumiwa huyo anashikiliwa na Jeshi hilo baada ya kuchapisha habari za uongo zinazohusu ugonjwa huo katika mitandao ya Instagram, Twitter na WhatsApp.
Mtuhumiwa huyo alichapisha habari inayosomeka “Ni kwanini serikali ya Tanzania inaficha sana takwimu za ugonjwa wa corona? Kumekuwa na usiri mkubwa mno wa ugonjwa huu wa corona… ukweli uliopo mpaka sasa Tanzania kuna wagonjwa 200 na zaidi wa corona na mpaka sasa waliokufa na corona ni wagonjwa wanne na hii yote imefanywa siri ya serikali na idara zake za takwimu.”
“Taarifa hii ilisamba katika mitandao ya kijamii jambo ambalo limelenga kupotosha umma na jamii juu ya ugonjwa huu hatari lakini pia kufifisha juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kupambana na corona,” amesema