28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kaburi la aliyezikwa na kuku tumboni lafukuliwa

Pg 2Na Kadama Malunde, Shinyanga
SIKU chache baada ya Benadetha Steven (35) aliyefariki dunia na kuzikwa na kifaranga cha kuku tumboni kwa madai ya kuondoa mikosi katika familia, kaburi lake limefukuliwa na watu wasiojulikana.
Benadetha (35) aliyekuwa mkazi wa Mtaa wa Mapinduzi, Kata ya Ndala, Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga, alifariki Januari 1 mwaka huu katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga alikokuwa amelazwa akitibiwa uvimbe tumboni na kuzikwa katika makaburi ya Masekelo.
Mazishi yake yalileta utata baada ya ndugu yake kutoka mkoani Mara kuingia kaburini na kumchana tumbo kwa wembe kisha kuchinja kifaranga cha kuku na kukiingiza kwenye tumbo lake.
Taarifa ambazo zimethibitishwa na Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Shinyanga (RCO), Musa Athuman Taibu, zimeeleza kaburi la marehemu huyo limefukuliwa na mwili kuchukuliwa huku sanda na jeneza vikiachwa.
Taarifa hizo zimemeeleza kuwa katika eneo hilo la makaburi kulikuwa na alama za nyayo za binadamu na za mnyama aina ya fisi.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, wanaelezwa kuwa hali hiyo ilibainika juzi jioni ambapo jana asubuhi uongozi wa eneo husika ulifika katika makaburi hayo na kuhakikisha taarifa za kufukuliwa kaburi hilo.
Akizungumzia hali hiyo mkazi wa eneo hilo, Makaranga Mabula (60), alisema tukio hilo la kufukua kaburi linatokana na imani za kishirikina na kwamba haliwezi kutendwa na binadamu mwenye akili timamu.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Masekelo, Kata ya Masekelo, Josephine Kishiwa (Chadema), alisema alipokea taarifa za kuwapo kwa tukio hilo juzi saa 1 usiku na ndipo jana asubuhi walipolazimika kwenda kuhakikisha taarifa hizo na kukuta hali hiyo.
“Tulipofika hapa, tulikuta jeneza na sanda ya marehemu ikionekana, ndipo tulipolazimika kuwaita polisi kwa ajili ya hatua zaidi za kiuchunguzi, naamini kitendo hiki kimefanywa na binadamu kwani fisi hawezi kufukua na kama angeweza, basi makaburi mengi yangekuwa yakifukuliwa,” alisema.
Aliongeza kuwa kuwapo kwa nyayo za fisi kunatokana na kuvutiwa na harufu ya maiti, hivyo kulaani kitendo hicho ambacho alieleza kuwa siyo cha kibinadamu.
Mjumbe mwingine wa Serikali ya Mtaa wa Mapinduzi katika kata hiyo, Deogratius Masanja, alisema jambo hilo ni tata kwa vile zipo taarifa kwamba baadhi ya ndugu walikuwa katika harakati za kufukua mwili huo na siku tatu kabla ya tukio hilo walionekana makaburini hapo.
“Huenda ndugu wa marehemu wanahusika, kwani kuna taarifa zinazodai baadhi ya ndugu walionekana polisi hivi karibuni wakiwa wanafuatilia kibali cha kutaka kufukua kaburi hilo,” alisema.
Polisi walifika jana saa 6 mchana eneo hilo na kuagiza uongozi husika kaburi hilo lifukiwe tena kwani Jeshi la Polisi halina mamlaka ya kufukua mwili bali mahakama.
Aidha akizungumza katika eneo la tukio RCO, Musa Athuman Taibu, alieleza kusikitishwa na tukio hilo alilodai linatokana na masuala ya imani za kishirikina, hivyo kuwaomba wananchi kutulia wakati wakiendelea kufuatilia.
“Ukiangalia kaburi hili halionyeshi kutitia, inaonyesha limefukuliwa na watu ambao hatujajua ni akina nani pamoja na nia yao kwa kitendo hiki, hali hii haiwezi kuvumiliwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles