29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wachambua matumizi ya fedha CCM

Askofu KilainiNa Waandishi Wetu
SIKU moja baada ya mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru kuzungumzia matumizi ya fedha kwa watu wanaotajwa kuwania nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), baadhi ya wasomi na wanasiasa wamemuunga mkono, huku wengine wakitaka uandaliwe utaratibu wa matumizi ya fedha.
Pamoja na hilo, pia makada wa CCM wanaolalamikia matumizi ya fedha ndani ya chama wametakiwa kutoa ushahidi au kupeleka ushahidi kwenye vyombo vinavyohusika.
Akizungumzia suala hilo mbele ya waandishi wa habari nyumbani kwake mjini Dodoma jana, mwanasiasa mkongwe nchini na kada wa CCM, Pancras Ndejembi, amekemea vitendo vya baadhi ya wanachama wa chama hicho wanaotangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu kwa kuwatuhumu wenzao badala ya kuelezea vipaumbele vyao.
Ndejembi alisema anashangazwa na madai yanayotolewa sasa ya matumizi ya fedha ndani ya chama, huku suala hilo likijitokeza kila inapofika wakati wa uchaguzi.
Alisema pamoja na kuwapo madai hayo, hakuna mtu aliyejitokeza na kwenda mahakamani kuyathibitisha zaidi ya malalamiko yanayojitokeza kila wakati.
Aidha alisema akiwa mmoja wa waasisi wa CCM, anahoji hatua ya kuibuka kwa wimbi la wagombea urais katika kipindi hiki hata kama demokrasia inawaruhusu kufanya hivyo.
“Hata kama wameamua kufumuka, wafuate utaratibu, waondoe moyo wa chuki, kwa sasa kila anayetangaza nia anataka awe peke yake, anamchukia mwenzake anayetangaza.
“Kama unaona unastahili kugombea nafasi hiyo fuata taratibu zako, usifanye kampeni ya kumchukia mwenzako, mara unamwita mwenzako fisadi, maneno ya ajabu ajabu, kama ni fisadi ulimpelekea mahakamani?” alihoji Ndejembi.
Aliwataka wanachama wote waliotangaza nia kuacha kuchafuana, kwani mwisho wa siku chama ndicho chenye uamuzi wa mwisho, ikiwamo kupitisha jina la mgombea wa nafasi ya urais ambaye kila mwanachama ana wajibu wa kumuunga mkono.
“Mimi sijikombi kwa mtu, naona tunakoelekea si kuzuri, viongozi wa chama wafuate utaratibu, watumie vikao, maandalizi ya uchaguzi yafuate vikao, hadi mwisho tutapata kiongozi bora.
“Atakayempokea Rais Jakaya Kikwete ni mmoja tu ambaye atateuliwa kutokana na sifa zake za uongozi na sio ukabila wala dini. Wapo wengine hata historia katika chama hawana halafu wanataka urais, wanachama hawawezi kukubali kukupa tu kwa sababu unataka,” alisema.
Aliwataka wanaoutaka urais wasimsahau Mungu kwa kuwa kazi hiyo siyo lelemama, lazima uwepo mkono wake katika kumchagua kiongozi wa kitaifa ambaye atakuwa mchungaji wa Watanzania wote.
Akizungumzia mwelekeo wa chama hicho, Ndejembi alisema kwa sasa ni mbaya, hali inayotoa mwanya kwa vyama vya upinzani.
Akitoa mfano kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba, mwaka jana, alisema hakukuwa na maandalizi ya kichama katika ngazi zote hali iliyosababisha CCM kufanya vibaya baadhi ya maeneo.
“Huwezi ukashinda bila maandalizi na kujipanga kujua huyu anafanya nini, chama lazima kiwe na utaratibu ikiwamo vikao vya maandalizi.
“Viongozi wa CCM wengi hawasikilizani, wana chuki, kwa mtindo huu hatuwezi kujenga chama cha kuongoza nchi, mambo haya yananishangaza kidogo, mifarakano hii itafika wapi, matokeo yake yatakuwa ni nini baadaye?
“Tumeona Kenya, KANU iko wapi, Zambia UNIP iko wapi, kwanini sisi tunafanya mchezo wakati uwezo wa kuimarisha chama tunao? Tuna ujuzi wa miaka mingi, sielewi, napata maumivu kweli.
“Kwa kujifunza kutoka vyama rafiki vya nchi za jirani ambavyo vilikuwa vikubwa na vyenye nguvu, lakini leo havisikiki, CCM ni vyema kimkakati ikajiandaa kwa uwezekano wa kuwa chama cha upinzani, hili ni jambo lisilopendeza kufikiria, lakini hakuna lisilowezekana,” alisema.
Alisema ni vyema Baraza la Wazee linaloundwa na marais wastaafu na makamu wenyeviti na mabaraza ya wazee wakae wajadili hali hii.
“Zipo kila dalili za wanaCCM na wananchi kukata tamaa, hivyo lazima chama kiwe na mkakati wa kurejesha matumaini kwa umma,” alisema.
Alisema kazi nzuri inayofanywa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ya kutafuta ufumbuzi wa kero za wananchi ifanywe na viongozi wengi zaidi wa ngazi ya kitaifa badala ya kumwachia peke yake.
Akizungumzia mchakato wa kura ya maoni ya Katiba inayopendekezwa inayotarajiwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu, Ndejembi alishauri mchakato huo uahirishwe hadi mwakani.
Alisema hali hiyo itawezesha kutoa muda ili kuhakikisha Katiba inapatikana katika hali ya maridhiano ya kitaifa kwa kuwa Katiba inayopendekezwa ilipatikana bila maridhiano ya wadau muhimu.
Ndejembi alisema mwaka jana, vyama vya upinzani vimenufaika katika shughuli ya Bunge Maalumu la Katiba lililozaa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao umeweza kushinda maeneo mengi ya mjini katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Dk. Bana
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, amesema kwa sasa suala la matumizi ya fedha kwa watu wanaotajwa kuwania nafasi ya urais linatajwa kwa sababu za kisiasa tu, huku akihoji kwanini wanaolilalamikia hawalifikishi kwenye vyombo vinavyohusika.
“Wanaosema fedha zinatumika kwanini hawafanyi jitihada za kuripoti Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kama wana ushahidi watu hao wafikishwe mahakamani?
“Matumizi ya fedha ni suala la kawaida na haliepukiki, kama mtu ameonekana akitoa rushwa na tuna ushahidi, basi afikishwe mahakamani kwa sababu maneno hayatusaidii wala hayalisaidii taifa, na hata tufanye nini fedha zitatumika tu,” alisema Dk. Bana.

Profesa Kitila
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Profesa Kitila Mkumbo, alisema suala la uchaguzi kwa ujumla kokote duniani ni fedha.
Alisema vyama vyote vinapaswa kufanyiwa ukaguzi wa hesabu zake kila mwaka, lakini utekelezaji wa sheria hiyo unasuasua hali inayofanya udhibiti wa hesabu za vyama kuwa mgumu.
“Ndani ya CCM ni kweli kuna watu wanawatuhumu wenzao kwamba wanatumia fedha, suala hilo bado haliko wazi, lakini ukweli ni kwamba hakuna mgombea asiyetoa fedha, huwezi kuzunguka nchi nzima kutafuta wajumbe bila fedha, unaweza kuona hapo kwamba hili halikwepeki.
“Tatizo CCM wameweka soko huria katika siasa, kila mtu anajifanyia lake analotaka bila kujali, hilo ni kosa lao wenyewe,” alisema Profesa Kitila.

Askofu Kilaini
Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini, alisema si jambo baya fedha kutumika, lakini ni nyema sheria ya vyama vya siasa ikafuatwa na Msajili wa Vyama vya Siasa ahamasishe sheria hiyo kufanya kazi.
“Si jambo baya fedha kutumika, lakini ni vema sheria zifuatwe pamoja na msajili wa vyama vya siasa nchini ahamasishe ili sheria hiyo ijulikane kwa umma badala ya kulalamika,” alisema Askofu Kilaini.
Akizungumza juzi, Kingunge alisema ndani ya CCM, watu waliojitokeza kuwania urais, kila mmoja anafanya faulo na hata wananchi wanajua.
“Badala ya kutafuta mchawi, tutazame namna ya kushughulikia hilo la maadili kwa sababu hakuna msafi,” alisema Kingunge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles