26 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Kabla ya 2020 mambo haya yarekebishwe

Na LEONARD MANG’OHA


KAULI ya Rais Dk. John Magufuli, katika kongamano la kujadili hali ya uchumi nchini lililofanyika Novemba mosi, mwaka huu, imethibitisha wazi azma yake ya kutoendeleza mchakato wa Katiba Mpya uliosimama tangu mwaka 2014.

Katika mazungumzo yake pamoja na kusifia kazi nzuri iliyofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Mstaafu, Joseph Warioba, amesisitiza kuwa hapendi kulizungumzia suala hilo kwa sababu hakulinadi katika kampeni zake alipokuwa anaomba kura, licha ya kukiri kuwa anafahamu hamu ya Watanzania ya kutaka Katiba Mpya.

Namnukuu: “Nafahamu hamu ya Watanzania ya kuwa na Katiba Mpya, sasa tunafanyaje, tunaendelea na hii Rasimu ya Katiba Iliyopendekezwa au tunakwenda kwenye ground work iliyofanywa na Jaji Warioba? Kwa sababu karibu miaka minne sasa imepita.

“Sasa badala ya kuanza ku-argue haya, ngoja tuchape kazi tusitumie fedha kuwapeleka watu bungeni wakalipane posho za kila siku, tunataka hizo fedha tuzitumie kujenga reli, tunataka hizo fedha zitumike kujenga Stigler’s Gorge, tunataka hizo fedha zikatumike kuinua kilimo.

“Ndiyo maana kuna mataifa mengine makubwa Katiba zao zimeundwa tangu mwaka 1800 na kitu. Wanafanya ‘amendment’ (marekebisho) tu mahali ambapo pameshindikana, lakini sisi tunafikiria Katiba kana kwamba ndiyo suluhisho la kila kitu, tutakaa tunabishana ‘we spend of money for nothing’ (tunatumia fedha nyingi bila sababu)”.

Anadai kuwa huu si wakati wa kuhoji bali ni wakati wa kufanya kazi na kusisitiza kuwa hategemei kutenga fedha kuwapeleka watu bungeni kula kwa sababu wengi wao wanaopiga kelele ni wale waliozoea kula fedha kwa madai ya kujadili Katiba na kwamba kama kuna mtu ana mpango wa kusaidia fedha kwa ajili ya kazi hiyo asaidie katika ujenzi wa reli mpya ya kiwango cha kimataifa (standard gauge).

Huo ndio msimamo wa Rais kuhusu jambo hilo hivyo matumaini ya kupata Katiba Mpya kwa kipindi hiki yamezikwa rasmi. Swali ni je, tunakwendaje katika chaguzi ndogo zinazotarajiwa kufanyika mwakani pamoja na Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Je, tuko tayari kuendelea na Katika ya Mwaka 1977 na mabadiliko yake mbalimbali yaliyowahi kufanyika kabla, ambayo wadau na vyama vya siasa wanailalamikia kuwa imekuwa na kasoro nyingi katika kulinda haki za kisiasa na kiraia, Katiba inayodaiwa kuwa inakipendelea chama tawala-Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kutokana na kasoro kadhaa zinazotajwa katika Katiba ya sasa, ipo haja ya kutafuta njia mbadala za kukabiliana na kasoro hizo kupitia vikao mbalimbali vya Bunge vitakavyoketi kabla ya chaguzi hizo kufanyika.

Miongoni mwa mikakati hiyo wadau mbalimbali likiwamo Jukwaa la Katiba (Jukata) wajipange kupeleka bungeni mapendekezo ya mabadiliko ya baadhi ya ibara za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na ile ya Zanzibar ya mwaka 1984 pamoja na Sheria ya Uchaguzi.

Baadhi ya maeneo yanayopaswa kutafutiwa ufumbuzi ni pamoja na kupatikana kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo muundo wake utaakisi majukumu yake aidha kwa kuwezesha kuwapo kamisheni itakayoongoza tume hiyo katika utendaji kazi wake, ikiwamo kuwajibika kwa mambo yote ya kisera na kimaamuzi, pamoja na kuundwa kwa sekretarieti ya tume itakayokuwa chini ya Mkurugenzi wa Tume, kama mtendaji mkuu.

Kwa sababu Rais anayekuwa madarakani, anaweza kuwa miongoni mwa wagombea katika uchaguzi au anakuwa kiongozi wa chama kimojawapo cha siasa ambacho kinasimamisha mgombea, basi ni vema kutoa mapendekezo ya namna ya kupunguzwa kwa mamlaka ya uteuzi kwa Rais tofauti na sasa ambapo mamlaka yote ya uteuzi yako chini yake.

Kama ambavyo Jukata imewahi kupendekeza ni vema mchakato wa kuwapata makamishna wa tume ya uchaguzi, utangazwe, ufanyike usaili kisha majina hayo yafanyiwe mchujo na kupatikana majina 20, yatakayopelekwa kwa Rais ambaye atapendekeza majina tisa yatakayopelekwa bungeni kufanyiwa uchambuzi na kujadiliwa na kasha yawasilishwe tena kwa Rais ili amteue mwenyekiti wa tume.

Baada ya Rais kumteua mwenyekiti wa tume atayawasilisha majina hayo kwa Jaji Mkuu ambaye atayatangaza na kuwaapisha makamishna wa tume. Pia Rais atamteua mkurugenzi wa tume kutokana na majina mawili yatakayopelekwa kwake na tume ya uajiri wa umma kutokana na mchakato huru na wa wazi wa uajiri.

Kwa mantiki hii ni kwamba, mkurugenzi wa tume ndiye atakuwa mtendaji mkuu wa tume hiyo, mkurugenzi wa uchaguzi na Katibu wa kamisheni ya tume (Bodi).

Upo pia umuhimu wa kupendekeza vyama vya siasa kuungana na kusimamisha mgombea mmoja na kutumia ilani moja ya uchaguzi. Pia viruhusiwe kujiunga na kuunda chama kimoja, bila kulazimishwa kufanya hivyo.

Kama ilivyo kwa matokeo ya ubunge na udiwani ni vema kutafuta namna ya kuwezesha matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani tofauti na sasa ambapo matokeo hayo hayaruhusiwi kuhojiwa baada ya kutangazwa na tume ya uchaguzi.

Kwa sababu sheria za nchi zinaitambua mahakama ndicho chombo cha mwisho cha kutoa haki, wananchi wanapaswa kupewa haki ya kuhoji. Kipengele hiki kinapaswa kuangaliwa upya, kwa sababu kinaweza kutoa mwanya kwa tume kumtangaza mtu kwa masilahi binafsi hata kama hakushinda na kupoteza haki ya walio wengi.

Mathalani kukiwa na kikundi cha watu wenye nia ovu, wakaamua kumpenyeza mtu kwa masilahi binafsi katika mchakato wa kumpata mwenyekiti wa tume na kwa bahati mbaya mamlaka ya uteuzi isiligundue hilo ni wazi kuwa taifa linaweza kutangaziwa Rais ambaye hajachaguliwa kwa kura nyingi.

Mabadiliko mengine yanayopaswa kufanyika ni kuitaka NEC kusimamia uchaguzi mdogo wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais kwa sababu ndicho chombo chenye utaalamu na weledi wa kusimamia uchaguzi.

Kitendo cha uchaguzi mdogo kusimamiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kunaleta hisia za unyonge kwa vyama ambavyo havijashika dola na kuvifanya kuamini kuwa havitendewi haki.

Kudhibiti hama hama

Kutokana na kushamiri kwa vitendo vya wabunge na madiwani kuhama vyama vyao na kujiunga na vyama vingine, hawa wapinzani kuhamia chama tawala, hali inayosababisha kurudiwa kwa uchaguzi katika majimbo na kata, ni vema pia yakafanyika mabadiliko ya sheria yatakayoruhusu wabunge kuhama bila kuhitajika uchaguzi wa marudio.

Hama hama ya viongozi hawa wa kisiasa si tu kwamba inawakera wananchi bali pia inaligharimu Taifa fedha nyingi pasi na ulazima. Ni vema kufanya mabadiliko ambayo yatamruhusu kiongozi aliyepo madarakani kuendelea na uongozi hadi hapo kipindi chake kitakapofikia ukomo, endapo atafukuzwa uanachama na chama chake na hii inaweza kuwa rahisi zaidi ikiwa mfumo wa mgombea binafsi utaruhusiwa.

Aidha, nafasi hiyo inaweza kuchukuliwa na mgombea aliyeshika nafasi ya pili katika uchaguzi uliomweka madarakani pale ambapo kiongozi husika atajiengua mwenyewe katika chama chake.

Mabadiliko haya yanapaswa kwenda sambamba na kizuizi cha kisheria kinachomzuia mtu anayejivua uanachama wa chama chake kwa makusudi kutogombea katika eneo hilo au jingine lolote kwa angalau vipindi viwili mfululizo.

Kwa mantiki hii ni kwamba, uchaguzi utarudiwa pale tu ambapo kiongozi wa eneo husika amefariki dunia.

Mchakato ulivyoanza, ulipokomea

Ikumbukwe kuwa mchakato wa Katiba Mpya  ulianza baada ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, kumteua Jaji Joseph Warioba, kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na baadaye kumwapisha pamoja na wajumbe wote 30 wa tume hiyo yaani 15 kutoka Tanzania Bara na 15 kutoka Zanzibar, Aprili 13 mwaka 2012, ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011.

Baada ya kuapishwa, mchakato ulianza kwa kukusanya maoni ya wananchi, mikutano 1,942 ilifanyika na wananchi milioni 1.365, walishiriki kutoa maoni.

Rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya ilizinduliwa rasmi Juni 3, mwaka 2013, jijini Dar es Salaam. Baada ya hapo liliitishwa Bunge Maalumu la Katiba ili kujadili rasimu hiyo, ambapo lilianza chini ya Mwenyekiti wake wa muda, Pandu Ameir Kificho, baadaye marehemu Samuel Sitta akachaguliwa kushika nafasi hiyo.

Licha ya rasimu hiyo kubeba mambo mengi mazuri, Bunge hilo lilitawaliwa na hoja ya muundo wa Serikali. Baadhi ya wajumbe wakitaka kuwapo kwa Serikali mbili, yaani Serikali ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano na upande mwingine ukitaka Serikali tatu yaani Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.

Bunge hilo lilikuwa na mvutano wa aina yake na kusababisha upande wa vyama vya upinzani kuanzisha muungano wao ambao waliuita Umoja wa Katiba ya Wananchi- Ukawa.

Wajumbe wa Bunge hilo walishindwa kupata mwafaka hata hivyo wajumbe wa upande mmoja walilazimika kupitisha Katiba Pendekezwa, kwa kuwa muda uliopangwa kwa jambo hilo ulikwisha.

Gharama zilizotumika

Tangu ilipoundwa Tume na baadaye Bunge Maalumu la Katiba zinakadiriwa kutumika Sh bilioni 120.

Fedha hizo ni pamoja na gharama za ukarabati wa Bunge ambazo zinakadiriwa kufikia Sh bilioni 8.2, posho za wajumbe 629 wa Bunge hilo kabla ya wale wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) hawajasusia vikao vya Bunge hilo.

Ikumbukwe kuwa posho ya mjumbe mmoja wa Bunge hilo kwa siku moja ya kazi ilikuwa Sh 300,000 huku kila mmoja akijikusanyia Sh 230,000 kwa siku zisizo za kazi. Inakadiriwa kuwa hadi mwisho wa vikao vya Bunge hilo kila mjumbe aliondoka na kitita cha zaidi ya Sh milioni 17.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles