27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Dhana ya uzalendo inasiginwa kunyamazisha wakosoaji

Na Dk. Ronald Ndesanjo


KATIKA kipindi cha miaka takribani mitatu sasa dhana ya uzalendo imepata umaarufu miongoni mwa Watanzania hasa viongozi wa kisiasa.

Umaarufu wa dhana hii unaweza kuwa umekaribia ama kulingana na ule wa dhana ya ufisadi ambayo ilikuwa maarufu katika kipindi cha karibu muongo mmoja na nusu kabla ya dhana ya uzalendo kushika hatamu.

Katika tafakari hii fupi ninaangalia nini hasa maana ya dhana hii ya uzalendo katika muktadha mpana wa maendeleo ya watu.

Hoja yangu ya msingi ni kwamba, maana ya dhana ya uzalendo imebadilika sana siku za hivi karibuni na kupewa tafsiri mbalimbali zinazojikita katika misingi ya mitazamo ya kisiasa baina ya wanasiasa na wananchi, nafasi ya kiuchumi ya makundi mbalimbali katika jamii na vigezo vingine vya kijamii kama utaalamu na taaluma.

Nitaanza kwa kuelezea japo kwa ufupi tafsiri niliyonayo ya dhana ya uzalendo na kufafanua hoja yangu ya msingi.

Uzalendo unatafsiriwa kama dhana ambayo mtu ama watu fulani wanakuwa na mapenzi ya dhati na taifa lao na wako tayari kwa lolote ili kulitetea taifa hilo kwa dhati na bila woga wala kificho (tafsiri yangu).

Hii ni tafsiri ambayo nimeifahamu kwa muda wote. Sina shaka ndiyo ambayo wengi wanaifahamu. Pamoja na hilo, uzalendo unaweza kutafsiriwa kama dhana ya uzawa; nikimaanisha ile sifa ya kuzaliwa katika taifa fulani.

 

Kwa mfano, tafsiri hii nimekuwa nikiisikia ikitumika katika maelezo yanayotolewa na viongozi juu ya ujenzi na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo…. “mradi huu umebuniwa na kujengwa na wazalendo”.

Kwa maoni yangu tafsiri hii humaanisha mambo makubwa mawili. Mosi, kuonesha dhana ya uzawa au asili ya wataalamu waliotekeleza mradi husika au kufanya jambo fulani kubwa la sifa.

Maana nyingine ni kuidhihirishia jamii na hata jumuiya ya kimataifa kuwa na sisi kama taifa tunao uwezo wa kusimamia na kufanya mambo makubwa.

Wakati nikiitazama tafsiri ya kwanza kama iliyo sahihi na kamilifu na hivyo kuitumia kama tafsiri rejea katika tafakari yangu.  Tafsiri ya pili ninaitazama kama ishara ya mwanzo kabisa ya kubadilika kwa dhana nzima ya uzalendo.

Hii naweza kuifananisha na zile zama za uzawa na wazawa iliyokuwa ikinadiwa na aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Iddi Simba.

Kadhalika, nimetumia mfano wa miradi ya maendeleo kwa makusudi nikielewa kuwa hili ni eneo ambalo dhana ya uzalendo imekuwa ikitumika sana. Baada ya kuweka msingi wa tafakari yangu sasa nitajikita katika kufafanua hoja ya msingi.

Ni dhahiri kuwa dhana ya uzalendo imekuwa ikitumika katika nyanja ya siasa za Afrika (ikiwemo Tanzania) kwa muda mrefu. Nakumbuka nikiwa shule ya msingi, mwishoni mwa miaka ya themanini na mwanzoni mwa miaka ya tisini, harakati za ukombozi kule Kusini mwa Afrika zilikuwa zimepamba moto.

Wakati ule tulikuwa tukisikia maneno kama mashujaa na wazalendo wa Afrika yakihusishwa na harakati zile na vinara wa harakati hizo kama Mwalimu Nyerere na Nelson Mandela.

Tangu wakati ule nilielewa uzalendo kama hali ya kupigania haki zako na za wale unaodhani ni wenzako bila kujali tofauti za rangi, kabila au jinsia, miongoni mwenu. Hivyo basi ieleweke kuwa matumizi yake katika siasa si jambo jipya hata kidogo bali tafsiri mpya za kisiasa ambazo zimeongezwa katika dhana ya uzalendo.

 

Dhana hii siku hizi imekuwa ikitumika hasa katika mashindano ya kisiasa baina ya vyama mbalimbali vya siasa nchini.

 

Tafsiri mpya (ya uzalendo) ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika kauli nyingi za wanasiasa hasa wa chama tawala ni zile zinazoashiria kuwa uzalendo na kuwa mzalendo ni pale tu mtu anapokuwa mfuasi au muungaji mkono wa sera za chama hicho.

Kutokana na kushamiri kwa tafsiri hii mpya, vyama vya upinzani na wafuasi wao wamekuwa wakijengewa picha kuwa wao ni wapinga maendeleo na hivyo kukosa uzalendo kwa nchi yao.

Wakati chama tawala kimekuwa kikijitanabaisha kama cha kizalendo (na wafuasi wake kama wazalendo), vyama vya upinzani, viongozi wake na wafuasi wao wamekuwa wakionekana kukosa uzalendo eti kwa sababu wao wanapinga tu.

Baadhi ya wanasiasa wa upinzani, kwa mfano Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki- Chadema) si tu wamekuwa wakishutumiwa kwa kukosa uzalendo bali hata kuhusishwa na hila za mabeberu za kuididimiza Tanzania.

Kwa hali ya kawaida kitendo kama hiki (endapo tuhuma hizi ni za kweli) ni kukosa uzalendo kwa hali ya juu. Swali la msingi la kujiuliza; je, uzalendo maana yake ni kuwa mfuasi wa chama tawala na kuunga mkono pasi na kudadisi, kuhoji na kutafakari yale kinachosimamia?

Uhusiano kati ya siasa za vyama vingi na tafsiri ya uzalendo hauishii kwa wanasiasa peke yao bali na kwa wafuasi na wapenzi wa vyama na viongozi wake.

Ni katika muktadha huu ambapo tumeanza kushuhudia kuibuka kwa matabaka ya wazalendo na wasio wazalendo. Hii ni kufuatana na upande upi wa jamii unaunga mkono chama na mwanasiasa gani kati ya chama tawala (cha kizalendo) na vyama vya upinzani (visivyo vya kizalendo).

Kwa mfano, katika chaguzi za ubunge na madiwani zinazoendelea kutokana na wimbi la wanasiasa wa upinzani waliokuwa na nafasi za kuchaguliwa kuhamia chama tawala, zimeanza kusikika kauli za wanasiasa kutoka chama tawala wakiwatahadharisha wananchi kutowachagua wanasiasa wa upinzani. La sivyo wataadhibiwa kwa kunyimwa maendeleo.

 

Kumbe kwa nyakati hizi unaweza kuwa mzalendo kwa sababu ya kuunga mkono chama tawala na viongozi wake na kuonekana kukosa uzalendo endapo unaunga mkono vyama na viongozi wa upinzani na pengine kuadhibiwa kwa kukosa uzalendo.

Katika hali inayofanana kwa karibu na niliyoielezea hapo juu ni kuhusishwa kwa masuala ya kitaalamu/taaluma na dhana ya uzalendo.

Ni ukweli usiopingika kuwa utaalamu ni kiungo muhimu katika kusukuma mbele gurudumu la maendelo kwani mipango ya maendeleo na utekelezaji wake vinategemea sana wataalamu katika fani au taaluma mbalimbali.

Katika eneo hili tafsiri nyingine ya uzalendo imeanza kuibuka hasa pale ambapo wataalamu wanaingia katika mgongano na wanasiasa (watawala).

Jukumu na lengo la mtaalamu ni kufanya jambo kwa kuzingatia miiko na taratibu za taaluma yake. Kwa upande mwingine lengo la mtawala ni kutekeleza yale aliyoahidi ama anayodhani yanawafaa wapiga kura wake. Hivyo basi, kufanya kazi pamoja baina ya makundi haya mawili ni suala lisiloepukika.

Changamoto huja pale makundi hayo mawili yanaposimamia misimamo inayokinzana; mtaalamu kusimamia taaluma yake na mwanasiasa au mtawala kusimamia sera zake.

Katika hili, misimamo ya wataalamu katika miiko ya taaluma zao imeanza kutafsiriwa na watawala na wanasiasa kama hali ya kukosa uzalendo.

Si jambo la kushangaza, kwa mfano, kusikia mwanasheria akishutumiwa kwa kukosa uzalendo eti kwa sababu tu anamuwakilisha mtuhumiwa wa ufisadi.

Katika nyanja ya uchumi pia pamekuwepo na matumizi mapya ya dhana hii ya uzalendo. Hivi karibuni kumekuwa na msukumo mkubwa wa wananchi kulipa kodi na kujenga mazoea ya kupenda kufanya hivyo.

Hili ni jambo la msingi kabisa na la kuungwa mkono ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya watu. Ulipaji kodi ni kigezo kikubwa kwa sasa cha kupima uzalendo wa watu kwa nchi yao.

Katika hili kuna mtazamo ambao umeibuka kuwa kulikuwa na ukwepaji wa kodi uliokithiri hapo nyuma hasa miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa katika sekta binafsi.

Pia katika hili kumeibuka kasumba ya kuwaona watuhumiwa wa ukwepaji kodi hasa matajiri kama watu wasio na uzalendo na nchi yao.

Pamoja na kwamba ni vigumu kwa mwananchi kukwepa kabisa kulipa kodi swali la msingi hapa ni je, wananchi wengi ambao wako katika mfumo usio rasmi wa kiuchumi (na hivyo kutolipa kodi moja kwa moja, kwa mfano, kodi ya mapato) nao si wazalendo?

Ikumbukwe kwamba kuwepo katika mfumo usio rasmi wa uchumi nako kunahusishwa na dhana hii kwa zile lugha za “unyonge na umaskini” kwa upande mmoja na “utajiri na ushetani” kwa upande mwingine kana kwamba kuwa mnyonge ama masikini ni sifa mojawapo ya mtu kuonekana mzalendo na utajiri na mafanikio kinyume chake.

Jambo la msingi hapa ni mazingira anayowekewa mwananchi ili apate hamasa ya kulipa kodi na kukidhi kigezo kimojawapo cha uzalendo.

Swali jingine ni je, wananchi wanaona kazi ya kodi katika maisha yao ya kila siku? Hili ni swali muhimu sana. Lina umuhimu wa kujibiwa hasa na wananchi wenyewe endapo tunataka wengi wawe wazalendo (kwa kulipa kodi na si kwa kuwa maskini na wanyonge).

Jamii ya Kitanzania ninaitazama katika muktadha wa matabaka makubwa mawili; tabaka la wenye kipato cha kati na kikubwa (wenye nacho) na tabaka la wenye kipato kidogo (wasio nacho).

Kama ambavyo nimetangulia kusema hapo juu; dhana ya uzalendo inajitokeza pia katika taswira ya matabaka haya makubwa mawili miongoni mwa jamii ambapo wenye kipato kikubwa wameanza kuonekana kama watu wasio wazalendo.

Ninasema hivi kwa sababu hali ya unyonge na umasikini inaendelea kupewa uhalali (kisiasa) kama hali ambayo inakubalika machoni pa watawala.

Hali ya kuwa na ukwasi inaanza kuhusishwa na ufisadi, ukwepaji kodi, ubeberu (ama kutumiwa na mabeberu) na mambo kama hayo ambayo kwa kweli ni vigumu kuyatenganisha na dhana ya kukosa uzalendo (hasa katika muktadha inamotumika sasa).

Kumbe basi, unyonge na umasikini vinaweza kuchukuliwa kama uzalendo dhidi ya wao wachache wasio wazalendo. Hii inatokana na ukweli kwamba wanyonge na masikini (wazalendo) ndio wanaoonekana kupendwa na watawala kuliko hali ilivyo kwa wenye kipato (wasio wazalendo machoni mwa baadhi yetu).

Kuweza kujibu swali la uzalendo ni nini na nani ni mzalendo inaweza kuwa changamoto kwa wengi wetu hivi sasa. Maana na tafsiri ya uzalendo na mzalendo vimebadilika sana siku za hivi karibuni.

Kwa kifupi dhana ya uzalendo imepoteza maana yake kwa kiasi kikubwa na inatumika kisiasa zaidi kufanikisha na kuhalalisha matakwa yao na kuwanyamazisha wale ambao wanadhani ni wapinzani wao.

Uzalendo kwa sasa unatumika kama karatasi ya litimasi ya kupima wale wanaounga mkono watawala au wanasiasa hasa wa chama tawala na wale wanaokaidi.

Tafsiri ya uzalendo kwa sasa kumbe ni kushangilia na kuimba mapambio ya watawala. Kumbe si lazima itafsiriwe katika msingi wa kuipenda nchi yako na kuipigania pale inapobidi hata ikimaanisha kwa kuwanyooshea kidole watawala pale unapodhani hawaenendi katika namna ambayo italeta faida kwa watu na taifa lao.

Mwandishi wa makala haya ni msomaji wa gazeti hili na mshauri mtaalamu katika masuala ya mazingira, jamii na maendeleo. Anapatikana kwa baruapepe; [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,406FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles