KULWA MZEE -DAR ES SALAAM
MWANDISHI wa habari, Erick Kabendera anaendelea kusota rumande, huku kesi yake imeshindwa kuendelea kwa sababu hakimu anayeisikiliza ana udhuru.
Kesi hiyo ilikuja jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa kumaliza shauri baada ya majadiliano ya mwisho kumalizika wiki iliyopita.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Janeth Mtega amepata udhuru, hivyo anaomba mahakama iiahirishe.
Wakili wa utetezi, Reginald Martin aliomba mahakama ipange tarehe fupi kwa sababu wapo katika hatua za mwisho kukamilisha makubaliano ya kumaliza kesi hiyo.
Hakimu Mkazi, Vicky Mwaikambo baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 24.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Kabendera anadaiwa kujihusisha na genge la uhalifu, tukio analodaiwa kulifanya katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2015 na Julai, mwaka jana Dar es Salaam.
Katika shtaka hilo, Kabendera anadaiwa kutoa msaada kwa genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia masilahi.
Katika shtaka la pili, siku na eneo hilo, Kabendera anadaiwa kukwepa kodi, zaidi ya Sh 173,247,047.02.
Katika shtaka la tatu, Kabendera anadaiwa kati ya Januari 2015 na Julai 2019, katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, alitakatisha fedha kiasi cha Sh 173,247,047.02.