24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Muhimbili kufanya utafiti kwa njia ya damu

AVELINE  KITOMARY- DAR ES SALAAM

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) inatarajia kuanza utafiti wa kupima saratani kwa njia ya damu, hiyo ikitajwa kuwa njia rahisi zaidi katika utoaji wa huduma ya matibabu ya mapema kwa watoto wenye saratani ya damu.

Njia hiyo inatumika kuthibitisha endapo mtoto anashambuliwa na saratani ya damu (AI-Real)  kwa kupitia  uchunguzi wa vinasaba, ambayo itahusishwa na uchukuaji wa sampuli ya damu ili kusaidia upatikanaji wa majibu ya vipimo ndani ya siku moja.

Hatua hiyo ni tofauti na njia iliyozoeleka kutumiwa na wataalamu wa uchukuaji wa kipande cha nyama kutoka kwa mgonjwa ambapo majibu yake huchukua takribani wiki tatu.

Akizungumza jana katika uzinduzi wa mradi huo utakaowashirikisha watafiti kutoka nchini Uganda na Tanzania, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS), ambaye ni mhusika katika utafiti huo,  Dk. Clara Chamba alisema njia hiyo itakuwa mbadala wa kutoa majibu yatakayowezesha upatikanaji wa majibu kwa haraka yenye kuharakisha matibabu kwa mtoto.

“Kwa kawaida ugonjwa wa saratani ya damu unakuja kama uvimbe katika sehemu ya taya au maeneo ya tumbo, hivyo ili upime lazima uchukue kipande cha nyama upeleke maabara ikafanyiwe uchunguzi.

“Njia tunayoifanyia utafiti ni kugundua ugonjwa huu kupitia damu, njia ni rahisi isiyohitaji mlolongo mrefu kama ilivyo uchukuaji wa nyama, kupitia damu tunategemea kuugundua  ugonjwa huu mapema kupitia vinasaba.

“Kuna vipande vya saratani ambavyo vina vinasaba, katika vinasaba hivyo kuna mabadiliko tutayaona yenye kutuonyesha saratani inayomsumbua mtoto,” alisema Dk. Clara.

Alisema njia hiyo ni rahisi na haraka katika kumpatia mtoto mwenye saratani matibabu na kuokoa maisha yake mapema zaidi.

Dk. Clara alieleza kuwa ugonjwa wa saratani ya damu  huathiri zaidi watoto kutokana na kirusi cha ‘EBV lymphoma’ ambacho kina uhusiano zaidi na ugonjwa huo.

Alisema kirusi cha EBV hucheza na kinga ya mtoto.

“Katika umri wa mtoto kuanzia miaka minne hadi saba kuna  mabadiliko ya kinga, kwahiyo ndiyo maana watafiti wanaeleza kuwa mabadiliko hayo yanachangia kwa kiwango kikubwa saratani,” alisema Dk. Clara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tiba MNH, Dk. Hedwiga Swai, alisema upimaji wa saratani ya damu kupitia damu ni teknolojia mpya, huku akieleza kuwa kufanyika kwa mradi huo hapa nchini kutazinufaisha Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kaskazini (KCMC), MNH pamoja na Hospitali ya St. Marys na Locar za nchini Uganda kutokana na wataalamu wake kujengewa utaalamu.

Dk. Hedwiga alisema kwa watoto wanaougua saratani ya damu na kutotibwa mapema, kiwango cha kupoteza maisha ni asilimia 100.

“Kama mtoto atapata matibabu mapema, kupona ni zaidi ya asilimia 90, katika wodi zetu tuna watoto zaidi ya 150 wenye saratani na wenye saratani ya damu wapo 20,” alisema Dk. Hedwiga.

 Alisema mradi huo wa miaka minne unafadhiliwa na Taasisi ya Utafiti wa Marekani kwa thamani ya Sh bilioni 15.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles