Na Mwandishi Wetu
MNADHIMU Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Mathew Mkingule, amesema wameunda Kamati Maalum kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa gofu jijini Dodoma ili kukuza mchezo huo.
Luteni Jenerali Mkingule ameyasema hayo jana wakati wa hafla ya kufunga shindano la gofu la Lugalo Open 2021 iliyofanyika viwanja vya Lugalo.
Amesema kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo,wapo tayari kushirikiana na klabu kuendeleza mchezo huo na kuliletea heshima Taifa kupitia gofu.
“Mashindano ya Lugalo Open 2021 yanadhihirisha nia ya Jeshi la Ulinzi kuendeleza mchezo huu wa gofu na sio huu tu ni pamoja na michezo mingine. Kwa hiyo naomba niwahakikishie kuwa sisi tupo tayari kuendeleza mchezo huu.
“Tumekuwa tukiahidi, tumehamia Dodoma tutajenga uwanja wa gofu kwa maelekezo ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, lengo ni kuhakikisha kwamba Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania liko tayari kushiriki na kuliletea heshima Taifa hili katika mashindano ya ndani na nje,” amefafanua Luteni Jenerali Mkingule.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, Brigedia Jererali Mstaafu, Michael Luwongo amesema klabu hiyo ipo tayari kupeleka wakufunzi Dodoma baada ya uwanja huo kukamilika.