27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

JWTZ kufanya kazi za Polisi si kiroja

SIKU kadhaa zilizopita Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilitumika kufanya operesheni maalumu ya ukaguzi na udhibiti wa biashara haramu ya fedha za kigeni jijini Arusha.

Baada ya operesheni  kufanyika pameibuka hisia na mitazamo tofauti kutoka kwa wananchi mbalimbali wakiwamo viongozi ya kwamba inakuwaje Jeshi la Ulinzi linafanya shughuli ambazo kimsingi zinastahili kutekelezwa na Jeshi la Polisi.

Mitazamo ya namna hii ambayo imesababisha hadi hofu ya kufanyika Mapinduzi ya Kijeshi kwa siku za usoni,  inatokana na mazoea au ufahamu wa wananchi dhidi ya shughuli mahususi za JWTZ ambazo ni kulinda Katiba na Uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulinzi wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kufanya mafunzo na mazoezi ili kujiweka tayari kivita wakati wote, kufundisha umma shughuli za ulinzi wa Taifa.

Shughuli nyingine za Jeshi la Ulinzi ni kushirikiana na mamlaka za kiraia katika kutoa misaada ya kibinadamu na uokoaji wakati wa maafa, kutoa huduma mbalimbali za kijamii, kukuza elimu ya kujitegemea na uzalishaji mali kupitia Jeshi la Kujenga Taifa na kushiriki ulinzi wa amani kimataifa.

Katika shughuli zote zilizoorodheshwa, ulinzi wa mipaka ya nchi ndiyo ina umaarufu mkubwa kwamba Jeshi la Ulinzi liko tayari kumfyeka adui yeyote atakayethubutu kuichezea mipaka yetu kama ilivyotokea kati ya mwaka 1978/1979 pale Idd Amin Dada wa Uganda alipokipata cha moto.

Hata hivyo kutokana na dunia kuendelea kustaarabika huku diplomasia ikishika kasi, tishio la nchi moja kwenda kuvamia nchi nyingine limepungua sana katika karne hii zaidi tunachoshuhudia ni machafuko ya ndani ikiwepo vita ya wenyewe kwa wenyewe, uasi na ugaidi.

Hivyo katika muktadha huu wa nchi kutokumbwa na misukosuko ya kuvamiwa mipaka yake, si tukio  la ajabu JWTZ ambayo  kimsingi  ni kiranja wa vyombo  vyote vya ulinzi na usalama, kufanya kazi za kipolisi.

Mwaka 2012 bungeni Dodoma, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi aliwafafanulia wabunge nyakati ambazo JWTZ inaweza kufanya kazi za  Polisi ambapo alisema: “Hakuna wakati au mazingira yatakayolifanya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania  kufanya kazi za ndani badala ya Jeshi la Polisi isipokuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linaweza kusaidia pale Jeshi la Polisi linapoelemewa na kuoombwa kufanya hivyo,”

Sasa  kama kuna  kipengele cha sheria kinachoruhusu Jeshi la Polisi kuomba msaada kutoka JWTZ pale linapokuwa limeelemewa na majukumu, wasiwasi ni wa nini?

Si tu kwamba sheria inaruhusu kufanya hivyo bali pia walioko ndani ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi  wa Tanzania  si wanajeshi kutoka ng’ambo bali ni ndugu, jamaa na marafiki zetu wa karibu ambao wanatambua fika ya kwamba mtumbwi ukizama wote tunazama.

Haitoshi si  busara kuendelea kuwa na mtazamo hasi dhidi ya wanajeshi wetu ya kwamba wao wamefundishwa kuua tu na hivyo hawastahili kuchangamana na raia badala yake jamii itambue ya kwamba  JWTZ ni ulinzi wetu hivyo kukutana nao mitaani ni fahari kubwa.

Naamini kabisa JWTZ ya sasa imesheheni askari/maafisa wazalendo tena wenye viwango vya juu kitaaluma ambapo kwao suala la kufanya Mapinduzi ni kichefuchefu na  ndiyo maana limeendelea kupata heshima kimataifa ya kwamba lina nidhamu ya hali ya juu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles