24.8 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

Umoja wa Ulaya (EU) yaikubali “Talaka” na Uingereza

BAADA ya miaka 45 kuwa pamoja, Umoja wa Ulaya (EU) umeikubalia Uingereza isiwe tena mwanachama wa jumuiya hiyo. Wakuu wa nchi na serikali za Umoja huo (Jumapili) huko Brussels, Ubelgiji, waliukubali mkataba wa kujitoa Uingereza kutoka ushirika huo kuanzia Machi 2019.

Baada ya mkutano huo wa kilele, Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, alisema: “mkataba huo uliokuwa mezani ni bora kabisa kuweza kufikiwa na ulio wa pekee,”

Wakuu wa nchi na Serikali 27 zilizobakia ndani ya Umoja huo waliliunga mkono Azimio la Kisiasa kuhusu uhusiano wa baadaye baina ya Umoja wa Ulaya na Uingereza. Mkataba huo wa kujitoa Uingereza umefikiwa baada ya mashauriano magumu baina ya Brussels na London yaliyodumu miezi 17. Licha ya kufikiwa tamati, lakini hisia za pande mbili si changamfu.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alisema: “Hii ni siku ya kihistoria ambayo inatoa hisia tafauti,” Naye Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Junker, alisema hivi kuhusu kujitoa Uingereza: “Huu ni wakati wa huzuni,” Hata hivyo, alisema kwamba licha ya wasiwasi wote uliokuwapo, mkataba huo ndio ulio bora kabisa kuweza kufikiwa.

Aliendelea kusema: “Ni wajibu wetu kuhakikisha Uingereza inaweza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya kwa njia ya mpangilio. Hivi sasa tumeweka misingi ya uhusiano wetu wa siku za mbele,”

Mshauri wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya kufikia mwafaka huu, Michel Barnier, alisisitiza kwa kusema: “Mashauriano kabisa hayajaelekezwa dhidi ya Uingereza. Tutabaki tukifungamana na Uingereza kama washirika na marafiki,” Waziri Mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte, alisema: “Hamna yeyote aliyeshinda chochote, sote tumepata hasara,”

Mkataba huo unaweka kipindi cha mpito hadi mwisho wa mwaka 2020 ambapo Uingereza itaendelea kubaki ndani ya Soko Moja la Ndani la Ulaya na pia ndani ya Umoja wa Forodha. Pia umeweka utaratibu wa haki za raia wa Ungereza wanaoishi ndani ya nchi za Umoja wa Ulaya na zile za raia wa nchi za Umoja wa Ulaya huko Uingereza.

Licha ya hayo, Uingereza itabidi ilipe kiasi fulani cha fedha kutokana na kuipata talaka hiyo. Maafikiano hayo pia yanataja juu ya suala la mpaka wa siku za baadaye baina ya Ireland ya Kaskazini ( ambayo ni sehemu ya Ufalme wa Uingereza) na Jamhuri ya Ireland ( ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Ulaya).

Lakini hicho kilichokiukwa huko Brussels ni kizingiti kimoja tu. Kuna vingine. Hapo Desemba 10, mwaka huu Bunge la Uingereza litabidi liuidhinishe au liukatae mkataba huu. Hakuna tamaa kubwa kwamba wingi wa wabunge watamfuata Waziri Mkuu May, licha ya yeye mwenyewe kuupigia sana debe. Katika tamko lake kwa taifa ambalo lilichapishwa katika magazeti mengi ya nchi hiyo, alisema: “Ukurasa mpya wa maisha unaanza,”

Huko Brussels Theresa May alitaja mafanikio na maslahi iliyoyapata Uingereza kutokana na mkataba huo. Kwanza:

Hakutakuwepo uhuru, kama ilivyo ssasa, wa raia wa nchi za Umoja wa Ulaya kuishi na kufanya kazi Uingereza bila ya kupewa vibali. Uingereza itaamua yenyewe kama inataka wahamiaji, pili: Uingereza itakoma kulipa Euro milioni 441 kila wiki katika Mfuko wa Umoja wa Ulaya na badala yake fedha hizo sasa zitatumiwa kwa huduma za afya za nchi hiyo na tatu: Uingereza itakuwa na mamlaka ya juu kabisa kuhusu sheria zitakazotungwa na Bunge lake.

Haya ni matakwa yaliyotolewa na Waingereza waliotaka nchi yao ijitoe kutoka Umoja wa Ulaya wakati wa kampeni za Kura ya Maoni ya raia mwaka 2016. Matokeo ya kura hiyo ni kwamba wingi chupuchupu wa wapiga kura walitaka Uingereza iipe mgongo Ulaya.

Hivi sasa inakisiwa wabunge kati ya 40-60 wa Chama tawala cha Conservative cha Waziri Mkuu May wataupinga mkataba huo, licha ya kuwepo pia wengine 10 ambao wanahisi ni bora kwa Uingereza kubakia ndani ya Umoja wa Ulaya. Vyama vya Upinzani vya Labour, Liberal Democratic na vile vile vya kizalendo vya Scotland na Wales vimesema wabunge wao wataupinga mkataba huo.

Hakijulikani nini kitatokea baina ya sasa na Desemba 10, lakini Umoja wa Ulaya umeweka wazi kwamba mpira sasa uko upande wa Uingereza na kwamba Waingereza wanahitaji watumie busara katika kuucheza mpira huo. Pia Umoja huo umesisitiza kwamba ikiwa Waingereza wanafikiri, pindi wakiukataa mkataba huu wa sasa,watapata ulio bora zaidi hapo baadaye, basi wajue ‘wataula na chuya’

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles