MSANII wa Bongo Fleva nchini, Juma Mussa ‘Jux’ na Benald Paul ‘Ben Pol’, wamesema ili muziki wa Tanzania ufike katika kiwango cha juu wasanii wenyewe kwa wenyewe wanatakiwa kupendana katika kazi zao kama wafanyavyo wao.
Wasanii hao wawili walisema hayo jana walipotembelea Ofisi za New Habari (2006) Ltd zinazochapisha magazeti ya Mtanzania, Bingwa, Rai, Dimba na The African.
“Sisi muziki wetu unafanana lakini tunapendana, ila wasanii wengine wenye muziki unaofanana huchukiana, tunawaomba wapendane kwa kuwa muziki wa sasa unataka ushirikiano wa wasanii kwa kuwa tunategemeana,” alisema Jux.
Naye Ben Pol alisema wasanii wengi wanashindwa kufika mbali kutokana na kuendekeza malumbano kwa kuwa wanapopata fedha zinazotokana na kazi zao hujisahau kuwekeza katika muziki wao na wengi wao hukimbilia kununua magari.
“Wanamuziki wengi unakuta wanakimbilia kununua bajaji wanasahau kuwekeza katika muziki wao, sasa wakiona wenzao wamefanikiwa wanaanza majungu na kulumbana jambo ambalo linatakiwa waliache wapendane kwa kuwa muziki unataka upendo na si ugomvi,” alisema Ben Pol.
Wasanii hao wametoa wimbo wa pamoja unaoitwa ‘Nakuchana’ ambao kwa sasa umeanza kufanya vizuri katika vituo mbalimbali vya redio.