MKURUGENZI wa klabu ya Juventus, Beppe Marotta, amesema hawana mpango wa kuwauza nyota wao, Paulo Dybala na Paul Pogba kwa kipindi cha hivi karibuni.
Wachezaji hao kwa sasa wamekuwa na mchango mkubwa katika klabu hiyo tangu kuondoka kwa nyota wao, Carlos Tevez, Andrea Pirlo na Artulo Vidal, hivyo klabu imesema itaendelea kuwakumbatia wachezaji hao.
Dybala, mwenye umri wa miaka 22, raia wa Argentina, ameitumikia klabu hiyo tangu Juni mwaka jana kwa kucheza michezo 34 na kufunga mabao 16, wakati huo Pogba akionekana kuwindwa na klabu ya Barcelona.
Marotta, akizungumza na radio Gr Parlamento ya nchini Italia, amesisitiza kwamba klabu hiyo kwa sasa inawatolea macho wachezaji hao.
“Klabu imefanya maamuzi ya kubaki na wachezaji wenye umri mdogo ambao wanaonekana kuwa na viwango vya hali ya juu, ambao watakuwa na mchango mkubwa baadaye.
“Kutokana na hali hiyo, klabu haina mpango wa kuwauza wachezaji hao kwa kipindi cha hivi karibuni kwa kuwa bado tunawahitaji,” alisema Marotta.