HAKUNA uhusiano ambao ulipendeza kwa watu maarufu hasa kwenye tasnia ya muziki nchini Marekani kama ilivyo kwa Chris Brown na aliyekuwa mpenzi wake Rihanna.
Uhusiano wao ulipendeza kutokana na wawili hao kuwa na umri mdogo huku wakifanya vizuri katika muziki, walianza kuwa katika uhusiano mwaka 2007 ambapo Chris aliachia wimbo wake ambao ulijulikan kwa jina la ‘With You’ Baada ya Chris kuachia wimbo huo, Rihanna alikuwa hana jinsi kwa kuwa ulimgusa sana na kushindwa kuzuia hisia zake na kuanza kumtafuta msanii huyo kwa lengo la kuanzisha uhusiano, mambo yakawa hivyo kila kona watu walijua uhusiano wao na kuvutiwa nao.
Hata hivyo baada ya miaka kadhaa, wawili hao waliachana na kila mmoja kufanya mambo yake.
Mbali na wasanii hao, wapo wasanii wengine Justin Beiber na Selena Gomez, ambao waliufanya uhusiano wao kuwa wazi kila kona na kutokana na umri wao kuwa mdogo mambo yalikuwa sawa.
Beiber alizaliwa mwaka 1994, wakati Selena akiwa amezaliwa mwaka 1992, lakini baada ya miaka kadhaa wawili hao waliachana na kuweka gumzo kubwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Hata hivyo japokuwa waliachana lakini walionekana kuwa wanapendana ila kila mmoja alikuwa anashindwa kumwambia mwenzake jinsi ya kurudisha uhusiano wao, lakini Beiber aliumiza kichwa na kufanikiwa kumrudisha mpenzi huyo kwa kutumia nyimbo zake. Beiber anatarajia kuachia albamu yake mpya ambayo
inajulikana kwa jina la ‘Purpose’, ndani ya albamu hiyo kuna baadhi ya nyimbo ambazo zinazungumzia uhusiano.
Nyimbo hizo ni kama ‘What Do You Mean?, Baby, Am Sorry na nyingine nyingi, lakini katika nyimbo hizo zimeonekana kumlenga Selena.
Habari zilizoenea mitandaoni hivi sasa zinasema kuwa, wawili hao wamesharudiana. Hata hivyo katika mahojiano tofauti kwa wasanii hao, Beiber alipoulizwa kama nyimbo hizo zinahusiana na mipango ya kumrudisha mpenzi wake, hakukataa.
“Bado ninampenda Selena lakini kwa sasa kila mmoja anafanya mambo yake, kuhusu nyimbo ambazo nimezifanya ni wazi kwamba zinawahusu wapendanao, hivyo kama bado ananipenda basi zinatuhusu,” alisema Beiber.
Kwa upande wa Selena, naye alisema kuwa, ataendelea kumpenda Beiber kwa kuwa ni mpenzi wake wa kwanza katika maisha yake.
“Beiber ni mvulana wangu wa kwanza katika uhusiano wangu, hivyo hata kama niliachana naye siwezi kumchukia, nitaendelea kumpenda na nitakuwa karibu naye kwa kumsaidia kama atahitaji msaada wangu,” alisema Selena.
Ni wazi kwamba wawili hao kwa sasa wamerudi katika uhusiano, kwa kuwa hata mwishoni mwa wiki iliyopita walikutwa pamoja kwenye tamasha la utoaji wa Tuzo za America Music Award (AMA), pia kwenye kumbi
mbalimbali za starehe.
Hivyo kutokana na uhusiano wa wasanii hao kuonekana kupendeza, kuna baadhi ya mashabiki wamewataka waendelee kudumu ili kuweza kutengeneza muziki wao.
Hata hivyo wawili hao bado hawajaweka wazi kama wapo katika uhusiano japokuwa wanaonekana wakiwa pamoja kwenye kumbi za starehe na kuondoka pamoja, hivyo inaonesha wazi kwamba wapo kwenye uhusiano.
Hapo ndipo inapomaanisha kwamba muziki ni dawa, kutokana na ubora wa nyimbo hizo za Beiber zimemfanya Selena kurudisha moyo wake kwa msanii huyo ambaye anatamba na wimbo wake wa ‘Am Sorry na What Do You Mean’.