27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

Rungu la Magufuli latua kwa Bakhresa

Screen Shot 2015-07-16 at 8.18.52 PM*TRA yazuia makontena yake bandari kavu

*Polisi yasema uchunguzi mzito unaendelea

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imezuia kampuni ya Said Salim Bakhresa & Co. Limited kupeleka makontena yake katika Bandari yake Kavu (ICD), baada ya kugundulika kuwa baadhi ya makontena yalipitishwa bila kulipiwa kodi.

Kwa mujibu wa barua ya TRA ya Novemba 17, mwaka huu,  iliyosainiwa na Wolfagang Salia kwa niaba ya Kamishina wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa, kampuni hiyo imezuiwa kutumia bandari yake hiyo- Namba 03 hadi kesi hiyo inayoshughulikiwa na mamlaka hiyo itakapotatuliwa.

“Unafahamu kwamba uondoaji wa bidhaa kutoka eneo linalodhibitiwa na forodha, ambalo kodi na ushuru wa serikali haujalipwa ni kinyume na sheria kwa mujibu wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Usimamizi wa Forodha ya mwaka 2004 na kanuni zake kwa vile husababisha upotevu wa mapato ya Serikali.

“Kwa sababu hiyo, imeamuriwa kukuzuia kupeleka makontena katika bandari yako kavu kuanzia tarehe ya barua hii, hadi suala hili litakapotatuliwa. Pande zote zinazohusika zinapaswa kutii amri hii.

“Kutokana na sababu hizo, tunasimamisha upelekaji wa makontena katika bandari yako kavu. Usitishaji unaanza mara moja. Hata hivyo utoaji wa bidhaa zilizopo katika bandari hiyo tajwa utaendelea,” ilisema taarifa hiyo.

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard
Kayombo, alipoulizwa alikiri mamlaka hiyo kumwandikia barua mfanyabiashara huyo huku akisisitiza kuwa hawezi kuzungumzia kwa undani suala hilo kwa sababu lipo katika uchunguzi.

“Ni kweli barua ile ni ya kwetu, lakini mambo mengine bado yapo kwenye uchunguzi, huyo (Bakhersa) ni kati ya wengine ambao tunaendelea kuwafanyia kazi na tukikamilisha tutawajulisha” alisema Kayombo.

Kova kutoa tamko leo

Gazeti hili lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, ili kujua watu ambao wamekamatwa kutokana na agizo la Rais Magufuli, alisema taarifa alizonazo bado hazijakamilika.

“Leo sina chochote cha kusema bwana, kesho (leo) nitatoa taarifa kwa vyombo vya habari ambayo ndiyo itakayofafanua kila kitu,” alisema Kova.

Alipofanya ziara ya ghafla katika bandari ya Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliwasimamisha kazi baadhi ya vigogo waliohusishwa na upotevu wa makontena 349 ambayo yameisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 80 kutokana na ukwepaji kodi na kuagiza wengine wakamatwe.

Taarifa ambazo gazeti hili imezipata, tayari maofisa kadhaa wa Bandari na wale wa TRA wamekamatwa kwa mahojiano zaidi.

Wahusika hao wanaendelea kushikiliwa na polisi huku uchunguzi wa akaunti zao pamoja na mali wanazomiliki ukifanywa.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wameshaanza kuhakiki mali za maofisa kadhaa wa mamlaka hizo.

Kutokana na hali hiyo MTANZANIA ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba, ambaye alisema kwa sasa bado wako kwenye uchunguzi wa watuhumiwa  wa TRA walioagizwa kuchunguzwa.

“Tupo kwenye uchunguzi mzito ambao unakusanya mambo mengi sana na hata inaweza kuongezeka idadi ya watu. Sasa ninachoweza kusema Watanzania watupe muda kila kitu kinakwenda sawa na tutatoa taarifa ya uchunguzi wetu,” alisema Advera.

Bakhresa kuchukua hatua

Kwa upande wake Kampuni ya Said Salim Bakhresa & Co. Limited kupitia Idara ya Ushirikiano, ilieleza kuwapo kwa ushirikiano baina yake na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika uchunguzi unaoendelea.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kampuni hiyo itachukua hatua dhidi ya wahusika. “Wale wote wanaohusika na upotevu huo watachukuliwa hatua na kodi yote ya Serikali inalipwa na wamiliki wote wa makontena yaliyo husika katika upotevu huo,” ilieleza taarifa hiyo.

Hata hivyo kampuni hiyo ilishangazwa na taarifa za kujumuishwa katika upotevu wa makontena 349 yaliyoripotiwa hivi karibuni kuwa yametolewa bandarini bila kulipiwa ushuru.

Novemba 27, mwaka huu Rais Dk. John Magufuli, alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade, muda mfupi baada ya ziara ya kushitukiza ya Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa aliyofanya Bandari ya Dar es Salaam.

Taarifa ya Ikulu iliyomnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, imeeleza kuwa hatua hiyo ya Dk. Magufuli imechukuliwa baada ya kubaini kupitishwa kwa makontena zaidi ya 300 bandarini bila kulipa kodi na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 80.

Baada ya kusimamishwa kazi kwa Bade, Rais Magufuli alitangaza kumteua Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk. Philip Mpango, kukaimu nafasi hiyo hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.

Pamoja na hali hiyo pia Rais Magufuli, aliiagiza maofisa wote wa TRA kutosafari nje ya nchi, hadi uchunguzi dhidi yao utakapokamilika.

Majaliwa alitangaza kuwasimamisha kazi maofisa watano na watumishi watatu wa TRA, kutokana na upotevu wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 80.

 

Majaliwa alichukua uamuzi huo baada ya kuzungumza na viongozi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) pamoja na wa TRA, ambapo pia alimtaka Bade na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Lusekelo Mwaseba, washirikiane na polisi kufuatilia upotevu huo na kuhakikisha fedha hizo zinapatikana na kurudishwa serikalini.

Kutiwa jela, kukaguliwa akitangaza uamuzi huo baada ya kufanya kikao na baadhi ya viongozi wa Serikali bandarini hapo, waziri mkuu aliwataja maofisa waliosimamishwa kazi kuwa ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya.

“Hawa wanasimamishwa kazi. IGP ninaagiza hawa watu wakamatwe na kuisaidia Polisi. Hati zao za kusafiria zikamatwe na mali zao zikaguliwe kama zinaendana na kipato cha utumishi wa umma,” alisema Majaliwa.

Maofisa wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari (hakutaja ni wa idara gani) na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD In-Charge), Eliachi Mrema.

Pia aliagiza watumishi watatu wa mamlaka hiyo wahamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani, ambao ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni ambao baadaye walitangazwa kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yao

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles