NA AZIZA MASOUD – DAR ES SALAAM
ALIYEKUWA Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi katika Jimbo la Mji Mkongwe, Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu (CUF), ameibua mjadala katika mitandao ya kijamii baada ya kumtolea maneno makali Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliyeandika ujumbe wa kuipongeza timu ya mpira wa miguu ya Zanzibar (Zanzibar Heroes).
Juzi kupitia ukurasa wake wa twitter, Kikwete aliandika ujumbe uliosomeka: “Nawapongeza Zanzibar Heroes kwa kututoa kimasomaso na kutinga fainali. Nawatakia kila la kheri katika mechi ya fainali waibuke na kombe na watupe raha ambayo Watanzania tumeikosa kwa muda mrefu.”
Baada ya ujumbe huo, Jussa alijibu kupitia ukurasa huo huo kwa kuandika: “Wakupe raha wakati wewe uliwapa karaha kwa kuifisidi #Zanzibar wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kupindua uamuzi wa Wazanzibari na kuyavuruga maridhiano yao? Ati Zanzibar Heroes wakutoe kimasomaso. Wanachofanya Zanzibar Heroes ni kuwatusi wote walio na hasadi na Zanzibar yao.”
Baada ya kuandika hivyo na Kikwete kutojibu, aliibuka Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), aliyeandika ujumbe ukimwita jina Jussa, naye akajibu “naam”.
Dakika chache baadaye, Zitto, akaandika neno moja kwa lugha ya Kiingereza: “Please (tafadhali)” na Jussa akajibu tena kwa kuandika ujumbe uliosomeka: “What? (nini). Mimi sikuzoea kuwa na ndimi mbili.”
Pia Zitto akaandika ujumbe mwingine uliosomeka: “Acha tufurahie mpira Bwana lo!.” Kisha Jussa naye akajibu kwa kuandika: “Of course tunafurahi na mpira! Lakini hilo halifuti tuliyotendewa na tunayoendelea kutendewa.”
Timu ya taifa ya Zanzibar iko nchini Kenya inakoshiriki mashindano ya Chalenji na leo inatarajiwa kucheza fainali na wenyeji baada ya juzi kuwachapa mabingwa watetezi Uganda mabao 2-1 katika mchezo wa nusu fainali.