25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Jussa amlilia Asha Baraki Makame

asha bakariKHELEF NASSOR, Z’BAR NA SARAH MOSSI, DAR

MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Asha Bakari Makame, amefariki dunia.

Asha (65) alifariki dunia jana alfajiri huko Dubai, Falme za Kiarabu alipokwenda kwa mapumziko kwa mtoto wake akitokea India kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo uliokuwa ukimsumbua.

Akithibitisha kifo cha mwanasiasa huyo ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Wanawake na Watoto Zanzibar, kaka wa marehemu Mbarouk Bakari Makame, alisema Asha alikutwa na mauti hayo akiwa katika maandalizi ya kurejea nchini.

Alisema baada ya kupokea taarifa ya kifo hicho, hivi sasa familia ipo katika maandalizi ya kusafirisha mwili wa marehemu kuletwa nchini ambapo unatarajiwa kuwasili leo saa 10 jioni kwa ndege ya Shirika la Qatar Air Ways.

Makame alisema baada ya kuwasili mwili wa marehemu utapelekwa nyumbani kwake eneo la Jang’ombe na mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho saa 4  asubuhi katika makaburi ya Kianga nje kidogo ya mji wa Unguja.

Asha aliyewahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi (Viti Maalumu) na Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, atakumbukwa kwa kuwa na misimamo isiyoyumba ndani ya chama chake cha CCM pamoja na kuibua maneno ya mipasho kwa wajumbe wa Kambi ya Upinzani ndani ya Baraza la Wawakilishi.

Kwa nyakati tofauti mipasho yake imeibua hisia kali ndani na nje ya baraza hilo na kusababisha kambi ya chama tawala na ile ya upinzani kutupiana vijembe.

 HISTORIA YA ASHA

Mwanasiasa huyo machachari visiwani Zanzibar atakumbukwa kwa uwezo wake wa kupambana na vyama vya upinzani, hasa Chama cha Wananchi (CUF), kupitia majukwa ya siasa na hata ndani ya Baraza la Wawakilishi.

Mwanzoni mwa mwaka 2000 akiwa ndani ya Baraza la Wawakilishi, aliibua msemo maarufu kwamba ‘Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haiwezi kutolewa kwa vikaratasi’.

Msemo huu aliurudia tena mapema mwaka juzi wakati wa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma lililokuwa likijadili utungwaji wa Katiba Mpya.

Ndani ya Bunge hilo, Asha aliibua hoja nzito ikiwamo kuibuka na msemo wa ‘kuufyatua’ wakati akijibu mapigo ya aliyekuwa mjumbe mwenzake, Ismail Jussa Ladhu.

JUSSA AMLILIA

Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, alisema chama chao kimepokea taarifa hizo kwa masikitiko na kusisitiza Asha alikuwa ni mwanasiasa mwenye uwezo wa kujenga hoja ndani ya Baraza la Wawakilishi katika kile anachokiamini.

“Alikuwa ni mhimili mkubwa ndani ya chama chao CCM, alikuwa mjengaji mzuri wa hoja ambazo zingeweza kuleta manufaa kwa chama chake,” alisema Jussa.

Alisema CUF kitashiriki kikamilifu katika mazishi ya mwanasiasa huyo, kwani chama hicho hakina tabia ya kuchanganya siasa na mambo ya kiutu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles