|Bethsheba Wambura , Dar es Salaam
Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), limeanzisha mchakato kuhamasisha wadau wote muhimu kuhakikisha mchakato wa mabadiliko ya katiba na sheria za uchaguzi unafanyika.
Aidha, Jukwaa hilo limesema uchaguzi wa serikali za mitaa umebakiza mwaka mmoja kufanyika na miaka miwili tu imesalia kuelekea katika Uchaguzi Mkuu hivyo ili kufanya uwe wa amani, haki na demokrasia mabadiliko madogo katika katiba na sheria yanaohusiana na uchaguzi hayaepukiki.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Agosti 8, Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda amesema wamefikia uamuzi huo kutokana na tamko la Rais John Magufuli kuwa mchakato wa katiba mpya si kipaumbele cha Serikali anayoiongoza kwa sasa na labda kipindi chote cha mwaka 2015-2020.
“Kutokana na kauli hiyo, tumetafakari kwa kina juu ya namna ya kuivusha nchi yetu salama katika uchaguzi wa Serikali ya za Mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 na kuona kuwa mabadiliko ya katiba na sheria za uchaguzi ni muhimu na yasiyoepukika,” amesema Mwakagenda.
Amesema yanahitajika mabadiliko katika Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi ambapo wanapendekeza mamlaka ya uteuzi wake yasiwe mikononi mwa Rais, iwe na wafanyakazi wake binafsi wasio makada wa chama chochote cha kisiasa na kuwepo na uhuru kamili wa tume hiyo na ile inayosimamia uchaguzi Zanzibar huku vyama vikiruhusiwa kuungana kwenye uchaguzi kwa kusimamisha mgombea mmoja.
Pamoja na mambo mengine, Mwakagenda amesema kuna haja ya kuwepo kwa uwiano sawa wa kijinsia katika uongozi na Jukata limependekeza kuwa katika kila jimbo la uchaguzi litakapokubaliwa achaguliwe mwanamume na mbunge mwingine mwanamke ili kuleta maana na kuunga mkono mkubaliano ya Beijing na Mkataba wa Maputo wa kupigania usawa wa jinsia na Haki za Wanawake .
“Kuingiza katika Katiba na kwenye sheria za uchaguzi uwakilishi sawia kati ya wanawake na wanaume katika vyombo vya maamuzi kama vile mabaraza ya madiwani, Bunge na Baraza la Wawakilishi kutasaidia kuakisi na kutekeleza dhana na nia iliyomo katika mikataba ya kimataifa iliyoridhiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu usawa wa jinsia,(50/50),” amesema.