UJENZI holela ni hali ambayo imeendelea kuwapo katika maeneo mbalimbali nchini licha ya hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa kudhibiti hali hiyo.
Ujenzi wa aina hiyo ni pamoja na kujenga katika maeneo ya shule, sehemu za wazi na maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za maendeleo kama vile masoko na kadhalika.
Kwa sababu hiyo ni jambo zuri na lenye mwelekeo unaotakiwa zinapochukuliwa hatua kukabili ujenzi wa aina hiyo kama ilivyofanya majuzi Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Halmashauri hiyo imezuia kaya 18 ndani ya eneo la Shule ya Msingi Kanindo katika Kata ya Kishili kutoendeleza makazi au kuanzisha ujenzi mpya hadi yatakapotolewa maelekezo mengine.
Ujenzi holela ulikithiri nchini kutokana na mamlaka husika katika upimaji ardhi, kwa maana ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokuwa na kasi ya kutosha kupima ardhi mijini na vijijini.
Ukosefu wa kasi inayotakiwa katika kupima ardhi umekuwa ukielezwa kuwa ni kwa sababu ya upungufu wa watumishi wa upimaji, ukosefu wa fedha na uhaba wa vitendea kazi yakiwamo magari.
Na kwa vile watu wamekuwa wakiongezeka kila kukicha, wamekuwa wakihitaji sehemu za kujenga na huduma nyingine hivyo kujikuta wakijenga popote wanapoona kuna eneo la wazi.
Maana yake ni kwamba hivi sasa zaidi ya asilimia 70 ya maeneo ya miji nchini hayajapimwa na yamejengwa holela.
Hata hivyo katika miaka ya karibuni Wizara ya Ardhi, hasa katika uongozi wa Waziri William Lukuvi, umeanzisha mkakati maalumu wa kuharakisha upimaji ardhi kwa kuhusisha watu na taasisi mbalimbali.
Vilevile, utaratibu wa kuhamasisha wananchi kupimiwa maeneo yao kwa mpango wa  urasimishaji ardhi nao umechangia kwa kiasi chake kuondoa tatizo sehemu zisizopimwa hasa mijini.
Pamoja na hatua hizo, hali bado haijawa ya kuridhisha. Sehemu kubwa za nchini, mijini na vijijini bado hazijapimwa na katika baadhi ya maeneo ni wananchi kukosa uwezo wa kulipia upimaji huo.
Pengine ingefaa uangaliwe utaratibu mwingine ambao utasaidia kuharakisha upimaji wa ardhi kuchangia kuokoa sehemu nyingi zinazotakiwa kutumika kwa huduma za jamii, ambazo sasa zimevamia na watu, ziweze  kukombolewa.
Ni vema pia wananchi wakaendelea kuelimishwa umuhimu wa kupima maeneo yao na kuacha kuvamia na kujenga katika maeneo yasiyotakiwa yakiwamo viwanja vya shule.
Tunasema jukumu bado ni kubwa na safari bado ni ndefu hivyo zinatakiwa juhudi za kila mhusika kuhakikisha tatizo la ujenzi holela linapunguzwa kwa kiwango kikubwa kama siyo kumalizika.
Ieleweke kwamba suala la upimaji ardhi ni muhimu na linachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo katika maeneo ya nchi yoyote.
Hivyo basi, viongozi na watendaji, ikiwamo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na halmashauri za miji na majiji nazo hazina budi kusimama kidete na kushiriki kwa ukamilifu katika suala hilo muhimu nchini.