29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JUHUDI ZA KUINUA SOKO LA PAMBA KITENDAWILI – 4

Na Andrew Msechu

Kila uchao, historia inaendelea kuandikwa. Matamko yanaendelea kutolewa. Ni nani anayejua hali halisi ya wadau wanaosimamia na kutekeleza uzalishaji na soko la zao hilo, bado kuna kilio kutoka kwa wazalishaji, wanunuzi na wasindikaji.

Historia inaonesha kuwa kati ya mwaka 2004 hadi 2009 kulikuwa na viwanda 79 vya usindikaji, ambazo kila moja ilikuwa na uwezo wa kuajiri watu 2000, ila kwa sasa kiwango cha juu kuajiri ni watu 1000.

Katibu wa Chama cha Wanunuzi  na Wasindikaji wa Pamba, Boaz Ogola anasema kwa sasa ni viwanda visivyozidi vitano vinavyoweza angalau kufanya kazi kwa msimu mmoja na msimu unapomalizika, viwanda hivyo hukaa bila kuzalisha kwa msimu muda wa hadi miezi sita mfululizo.

Anasema viwanda vingi vimelazimika kufungwa kabisa, pia vichache vinavyofanya kazi vinafanya chini ya uuwezo wake na kulazimika kuzima karibu nusu ya mitambo kutokana na uhaba wa pamba.

Ogola anasema uwezo wa kiwanda kimoja, kama kilivyo kiwanda cha Alliance Ginneries ni kuajiri ni watu 1500 iwapo watakuwa katika nafasia ya kutumia uwezo wao halisi wa uzalishaji kutokana na uwekezaji uliofanywa, lakini kwa sasa wanaweza kuajiri chini ya kiwango ambacho ni watu wasiozidi 300.

“Kwa sasa, uwezo wa viwanda vya kusindika pamba umeshuka kutokana na kutokuwepo kwa pamba ya kutosha. Kwa mfano, kiwanda cha Alliance Ginneries chenye mitambo ya kisasa na hitaji la nguvu kazi ya zaidi ya watu 500 ndani na zaidi ya 1500 nje kinatumia nguvu kazi ya watu 150 ndani na watu wasiozidi 100 nje. Kimelazimika kufunga nusu ya mitambo yake. Ipo haja ya kuangalia namna ya kuwa na kilimo cha umwagiliaji ili kufanya pamba ipatikane kwa vipindi vyote vya mwaka, hili linawezekana iwapo Serikali itaweka nia na kuwekeza ipasavyo kwenye eneo hili,” anasema.

 

Anasema tangu waanze shughuli ya uwekezaji katika eneo hili wamekuwa wakifanya kazi chini ya uwezo, hivyo kujikuta wakiwa na matumizi mengi ya fedha bila kuzalisha, kwa kuwa kuna wafanyakazi ambao huwezi kuwasimamisha kwa sababu tu kiwanda hakijapata malighafi za kuzalisha.

Anataja gharama za uendeshaji kwa ajli ya menejimenti, umeme, ulinzi, simu, televisheni, wataalamu washauri ambao wameshaingia nao mikataba, kwamba wote hao lazima wahudumiwe.

“Jambo jingine ni kwamba mfumo wa ununuzi wa pamba unaathiriwa sana na ulegevu wa sheria za kubana wahalifu, hasa mawakala tunaowatumia pale wanapotoroka na fedha zetu. Hawa mara nyingi ukiwapeleka mahakamani polisi wanadai lazima ufanyike uchunguzi, mwishowe wanaangukia kwenye kesi za madai badala ya jinai. Katika hili mtu anapoangukia katika kesi ya madai ambayo inaelekeza kwamba alipe kutokana na uwezo wake wa wakati huo, kwa kadiri ya maelezo yake mahakamani, hivyo inakuwa vigumu sana kurejesha fedha,” anasema.

Tatizo jingine linalowakabili wachambuaji na wasindikaji i wa pamba ni umeme usio wa uhakika na miundombinu mibovu vijijini hivyo kufnya ukusanyaji wa pamba kuwa wa gharama kuwa sana.

Ansaf na kujipima

Katibu Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Kilimo katika Sekta Isiyo Rasmi (ANSAF) Audax Rukonge anasema anasema kilio cha wadau kunatokana na Dira ya Uendeshaji wa sekta hiyo kutoshirikishwa ipasavyo kwa wadau na kubaki mikononi mwa Bodi ya Pamba, ambayo pekee imekuwa ikihodhi maandiko yake, japokuwa yamekuwa yakiwekwa katika mitandao yake.

“Wakuu na Wakurugenzi wa Wilaya wamekuwa wakiweka malengo lakini hawaweki mikakati katika kusimamia malengo hayo, na hata hivyo, malengo hayo hayawezi kufikiwa kwa kuwa hawayafikishi ipasavyo kwa wakulima na wataalamu wa kilimo katika maeneo yao. Hawa wakiwajibika ipasavyo kwa kuweka bajeti zinazotosheleza kuwafikia watendaji wakuu, ambao ni maofisa kilimo kuanzia ngazi ya kijiji (kama wapo) angalau tunaweza kuanza kuona tofauti,” anasema.

Anaongeza kuwa kutokana na matatizo yaliyopo kwa sasa, hata wawekezaji bado wanasita kuwekeza katika eneo hilo kwa kuwa hawaoni sababu na wanahisi watapoteza bure mitaji yao, lakini kilimo kikiboreshwa na kuwa na uhakika wa upatikanaji wa pamba ya kutosha, wataweza kuingia kwa wingi na kuwekeza katika sekta ya bidhaa za pamba ikiwemo nguo, mafuta, mashudu, uzalishaji wa vitebndea kazi mahopitalini na vifaa vya majumbani ikiwamo mazulia.

Akizungumzia kuhusu mfumo wa masoko, Mkuu wa Sera na Bajeti wa ANSAF, Joaseph Nyamboha anasema serikali imekuwa haiingilii kati mfumo wa bei ya masoko ya pamba kwa kuwa hata baada ya Rais John Magufuli kutangaza bei elekezi kuwa shilingi 1000 kwa kilogramu moja kutoka shilingi 600 ya awali, bado inaonekana kuwa bado haiwezi kumpa faida mkulima ikilinganishwa na gharama za uzalishaji, ambazo hufikia hadi shilingi 2000 kupata kilo moja ya pamba bora yenye kiwango kinachikubalika kimataifa.

Anasema mfumo huo wa bei unahitaji kumshirikisha mkulima wakati wa upangaji wake, kwa kujua gharama anayotumia mkulima katika kilimo tangu maandalizi ya shamba hadi mavuno, kisha kupanga bei ambayo itamsaidia mkulima na kuibua morali ya wakulina ili kuwarejesha katika kilimo halisi cha zao hilo.

Sheria ya Pamba ya mwaka 2001 inayounda Bodi ya Pamba inaeleza wazi kuwa bodi ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza bei baada ya kukaa na kujadiliana na wadau, wakiwemo wakulima, kisha kufikia makubaliano kuhusu bei ya ununuzi, kwa kuhakikisha wanatanguliza mbele maslahi ya mkulima, hasa suala la kumpa faida mkulima baada ya kurejesha gharama zake za uzalishaji.

Hata hivyo, Nyamboha anasema ni wakati wa kuivaa Sayansi na Teknolojia ipaavyo kwakuhakikisha kuwa kunakuwa na mitaala maalumu kwa ajili ya kuwanoa vijana wataalamu kwutokana na uhitaji wa sasa, ili kuwapata wabunifu watakaokuja na mawazo yenye tija yanayoweza kunasua kilimo cha pamba.

“Kwa sasa, ni wazi kwamba vyuo vingi kuannzia ngazi ya kati hadi vyuo vikuu vinavyowatengeneza wataalamu wetu wengi katika kilimo bado vimeegemea sana kwenye nadharia kuliko vitendo. Tunahitaji kuwa na vyuo vingi vya ufundi na vyuo vikuu ambavyo vitakuja na majibu kwa vitendo. Ambavyo vitaleta majibu kuanzia katika kilimo hadi kwenye uchakataji wa zao na bidhaa za pamba,” anasema.

Anasema suala muhimu ni serikali kuangalia upya bajeti yake kwa sekta ya kilimo inayoajiri zaidi ya asilimia 67 ya Watanzania, kwa kuwa kiasi kinachoelekezwa kwenye kilimo kwa sasa ni kidogo ikizingatiwa kwamba nchi zote zilizofanikiwa zilielekeza nguvu kwenye kilimo, hivyo angalau asilimia kumi ya bajeti ielekezwe huko, tofauti na sasa ambapo ni chini ya asilimia nne inayotumika, nayo haiwafikii wakulima moja kwa moja.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Uchumi na Kilimo katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Dk Damian Gabagambi anasema anasema litakuwa jambo la maana kama wadau watatilia mkazo uboreshaji wa mazingira ya uzalishaji katika sekta ndogo ya pamba kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili zao hili.

Baadhi ya changamoto hizi ni pamoja na ukame, matumizi duni ya teknolojia za kisasa zikiwemo mbegu bora na pembejeo zingine, mifumo duni ya ununuzi na usambazaji wa pembejeo, kukosekana kwa utafiti na huduma madhubuti za ugani, ubora duni wa pamba unaodidimiza bei, na kuingiliwa kisiasa kwa sekta ya pamba.

“Unatakiwa mkakati maalumu wa kujenga mnyololo wa thamani zao la pamba, hasa kwa Serikali kuamua kuwekeza kikamilifu katika sekta hiyo,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles