Nora Damian, Nzega
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amewaomba wakazi wa Nzega Mjini wamchague tena Hussein Bashe kutokana na kazi kubwa alizozifanya jimboni humo.
Akizungumza leo Jumatano Septemba 2 katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Parking Nzega Mjini, Dk. Magufuli ameyataja mafanikio yaliyopatikana katika jimbo hilo miaka mitano iliyopita kuwa ni pamoja na ujenzi wa wodi ya wazazi katika hospitali ya wilaya, kujenga kituo cha afya Zogolo na zahanati tatu na kwamba wameanza ujenzi wa kituo cha afya Kitengwe.
Amesema pia zimejengwa shule, madarasa, maabara, mabweni, mabwalo pamoja na mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria ambao utanufaisha wananchi 55,000.
“Hiki si kitu kidogo mtu mwingine anaweza akasema ni kazi rahisi…ni kazi kubwa imefanyika.
“Mlimchagua Bashe anafanya kazi nzuri kwa manufaa ya wananchi hasa wanyonge, ninamuombea kura Bashe mumpe kura zote ndugu zangu wa hapa ili aendelee kuchapa kazi. Ninyi watu wa Nzega ni mashahidi hata suala la pamba, sasa nitashangaa mumnyime kura.
“Nitashangaa kama haya yote mazuri tuliyoyafanya shukrani yake iwe ni kuninyima kura, niwaletee maji nihangaike usiku na mchana pamoja na wabunge leo mseme hapana.
“Kila mmoja akaguswe na Mwenyezi Mungu, tunachokiomba kutoka kwenu mtulete tena nawahakikishia mtaona maajabu,” amesema Dk. Magufuli.
Naye Bashe amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita juhudi kubwa zimefanyika kwa kushirikiana na halmashauri katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kwa mujibu wa Bashe zaidi ya Sh bilioni 6 zimetolewa na halmashauri huku yeye mwenyewe akitumia zaidi ya Sh milioni 935 kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Uliniteua na kunipa dhamana ya naibu waziri wa kilimo, kwa wananchi wa Nzega hii ni heshima kubwa tunakushukuru sana.
“Waliompinga Yesu, Mtume Muhamad hawakukosekana, wapo watakaopinga kazi hizi unazofanya lakini sisi tunaoelewa tupo pamoja na wewe kuhakikisha unashinda kwa kishindo. Tumejipanga kuhakikisha Oktoba tunakuchagua kwa zaidi ya asilimia 90,” amesema Bashe.